SEHEMU YA TATU
Kamanda alitoa taarifa yake ya uchunguzi kwa Mkuu wake Madam S na kumuomba kama anaweza kumtuma haraka Dr Jasmine au mwili wa Msesema upelekwe Dar es salaam, cha muhimu alichokitaka ni uchunguzi tu wa kina wa kitabibu juu ya mwili ule kutokana na utata mdogo ambao yeye ameuona na labda mganga mkuu wa mkoa hajauona. Madam S alilipokea na kumuahidi kulifanyia kazi mara moja na kumpa majibu yatakayopatikana juu ya hilo.
Kamanda Amata alitulia kimya kabisa pale alipoketi katika moja ya viti vilivyo katika baa ya Srafina pembezoni kabisa mwa reli ya kati na barabara ya Iringa, alikuwa akijaribu kutafakari hatua ya kufanya, akiwa ndani ya tafakuri hiyo mara simu yake ilitoa mlio wa taratibu sana akaipokea na kuisoma kwenye kioo ‘Mama’, akainyakuwa mara moja na kuiweka sikioni.
“Ndiyo mama…” aliitikia ile sauti ya upande ule, “…Ok, nimekupata (…) hiyo ni nzuri zaidi, oka bye,” alimaliza kuongea na ile simu, akaikata na kuirudisha katika mfuko wa ndani wa koti lake.
§§§
Wakati Amata Ric au Kamnda Amata kama alivyozoeleka akimalizia bia yake aina ya Safari iliyokuwa chupani, tayari Dr. Jasmine, mganga wa idara maalum ya usalama wa Taifa, TSA, alikuwa akielekea uwanja wa ndege kuondoka asubuhi hiyo kuelekea Dodoma kwa kazi hiyo iliyoita maalum.
Ilimchukua dakika arobaini tu tayari alikuwa akipumulia Dodoma, makao makuu ya nchi, alipokelewa na Kamanda Amata na moja kwa moja walielekea katika hospitali ya mkoa wa Dodoma baada ya kupewa kibali na serikali cha kuendelea na uchunguzi huo
“Niambie Kamanda,” Dr. Jasmine alivunja ukimya uliokuwa baina yao wakiwa wanatembea kwa miguu yao kuelekea katika ofisi ya mganga mfawidhi wa hospitali hiyo.
“Niliona ufike, kuna mambo yananitatanisha kidogo katika taarifa ya uchunguzi na siwezi kumwambia mtu mwingine yoyote zaidi yaw ewe,” Wakati Kamanda akimaliza kuongea hayo tayari walikuwa wamekwishafika katika mlango wa ofisi ya Mganga Mkuu.
“Oh, karibu sana daktari,” yule Mganga mfawidhi akawakaribisha.
Baada ya maamkiano mafupi moja kwa moja yule mganga alimwongoza Dr. Jasmine na Kamanda Amata mpaka chumba cha uchunguzi na kuwaacha yeye mwenyewe akitoka ndani ya chumba hicho.
Dr. Jasmine na muuguzi mmoja walisaidiana kuutoa mwili wa hayati Msesema na kuulaza vizuri juu ya kitanda tupu cha chuma na Jasmine akaianza kazi yake mara moja, akichukua hiki na kile akikata hapa na pale kwa utulivu wa hali ya juu sana, wakati huo Kamanda Amata alikuwa ameketi mbali kidogo akisubiri kuona ni nini ambacho atakigundua.
Baada ya ukimya kama wa dakika arobaini na tano hivi, Dr. Jasmine alifungua kinywa chake, “Kamanda Amata,” akaita.
“Nipe taarifa,” kamanda akaitika huku akiinuka mahali alipokuwa ameketi na kabla na kusogea pale kwa Dr. Jasmine.
“Hapa kuna utata kidogo naugundua, sijui kwa upande wako, kifo cha huyu marehemu kimetokana na nini?” alimtupia swali Amata ambaye alibaki kimya kwa nukta kadhaa.
“Ajali ya gari,” akajibu.
“Hapana, impact ya ajali na majeraha yake yasingeweza kumletea mauti huyu marehemu, kuna kitu cha ziada ninachokigundua hasa upande wake wa kichwani, huyu bwana Msesema ameuawa, tazama hapa kichwani ukiachana na majeraha ya vioo huku usoni, tazama hapa kwenye paji la uso, hili sio jeraha la kioo, nimejaribu kupitisha kitu nikaona kinazama bila ukinzani, ina maana tuntu hili limepita kwenye fuvu, (kisha wakamgeuza upande wa nyuma) unaona hii kisogoni? Hili ni jeraha lenye uwiano kabisa na lile katika paji la uso, naweza nikasema kapigwa risasi, lakini risasi gani hii?” Dr. Jasmine akamliza maneno yake kwa swali. Amata Ric au Kamanda Amata akamtazama daktari huyu makini wa usalama wa Taifa, akatikisa kichwa chake kuashiria amekubaliana na hilo.
“Well done doctor,” Kamanda Akampongeza huku akimpigapiga begani, “Hata mimi nilipata wasiwasi na hilo jeraha, sikuliona kabla lakini kwenye ripoti ya awali walisema amekufa kwa kuumizwa kisogoni nilipoenda kuchunguza gari hakuna alama yoyote ya mabaki ama ya damu au hata unywele wa kisogo isipokuwa mbonyeo hafifu wa paa la gari, nikachukua hatua ya kukuita nawe umenipa mwanga,” Amata akasogea na kwa kutumia saa yake akapiga picha za ukaribu wa jeraha lile nyuma na mbele na sura nzima ya mwili wa Msesema. Akatoka na kuketi pembeni, akafungua simu yake kubwa na kuzirusha zile picha kwa kutumia Bluetooth kutoka kwenye saa kwenda kwenye simu kisha akazituma kwa Chiba, mtalaama wa kusaka siri za kitu kwa kupitia mitandao anuai ulimwenguni. Chiba alikuwa na sifa ya kipekee ya uwezo wa kukariri mitandao mingi duniani bila kuichanganya na kupata njia ya ufumbuzi wa haraka wa jambo kwa mtandao pasina shaka.
Walipojiridhisha na uchunguzi huo, ule mwili ulirudishwa katika jokofu. Dr. Jasmine aliandika taarifa ya uchunguzi wake na akaisaini na kugonga mhuri wake maalum kisha akaitia bahashani. Zoezi hilo lote lilichukua kama masaa manne hivi kukamilika.
§§§§§
“Enhe Bwana Matata hebu tuambie maana umetuita hapa ki-kuku kuku,” aliongea Kagosho
“Leo nimemwona yule mpelelezi mtata wa serikali pale katika ofisi za zetu akitoka kwa Mheshimiwa,” Matata aliongea huku akionekana kuwa na wasiwasi.
“Kwa hiyo?” Aliuliza mjumbe wa tatu.
“Nahisi kuna kitu, wasije kugundua udhalimu huu,” Matata aliongea kwa kusema huku uso wake ukijawa na wasiwasi.
“Aaaaaa Matata hebu acha matata yako, Obobo ni profesheno katika kazi hizi, hawawezi kugundua lolote zaidi ya ajali,” alibisha Kagosho, akakohoa na kuongeza, “Yule jamaa anakuua wakati unakata roho, ni mtaalamu, sasa hapo hata wapimeje ajali ni ajali tu”.
Pumzi ndefu zikasikika kutoka katika tundu kubwa za pua ya Matata, “Mi sio mtoto, na mkumbuke niliwahi kuwa kepteni wa jeshi hapo nyuma, nayajua haya mambo, yule kijana ni intelligent, yuko smart, ukimuona katua hapa ujue Ikulu imemtuma, nina wasiwasi”.
Kimya kifupi lakini chenye mshindo mkuu kikapita kati yao, hakuna aliyeongea.
“Ngoja tuone!” alimalizia Kagosho, “Na sasa Obobo amesemaje kuhusu hao waliobakia na zile dokumenti zenyewe?” akauliza.
“Amesema ‘kazi ya pili ni kuziiba hizo dokumenti ofisini’ halafu baada ya hapo ndipo atamaliza kazi,” Matata aliwaelewesha.
Baada ya mazungumzo hayo marefu sana, waliafikiana kutulia na kutazama kinachoendelea katika shughuli hiyo ya mazishi kwanza, kusikia kama kuna tashtiti zozote zinazoweza kuvuruga mpango wao, waliachana na kila mmoja alirudi kwenye majukumu yake kwa wakati wake.
§§§§
Muda uleule kikao kile kikiendelea, huko Dar es salaama nako Madam S alikuwa na kikao kifupi na Chiba wakijadiliana juu ya taarifa ile ya Dr. Jasmine pamoja na ile ya kwanza wakichanganya na ile ya polisi ili kutanabahi ukweli uliopo. Bila shaka wote wawili waligundua kuwa marehemu kauawa kwa silaha maalum inayotumiwa na majasusi,silaha hiyo huwa na umbo la peni ambayo huweka mfukoni kama peni za kawaida, lakini ina uwezo wa kubeba risasi ndogo zenye ncha kali tatu na kufyatuliwa pindi tu aliyeishika akibofya kinibu cha juu ya peni hiyo kama mtu anayetaka kuandika, risasi yake huweza kumpanya mlengwa na kutopkea upande wa pili bila kuleta madhara ya kutisha, daima inahitaji wataalam sana kuchunguza vifo kama hivyo.
Tafutishi za Chiba zilimpa jibu hilo lisilo utata mwanamama huyu aliyeanza kufunikwa na mvi kichwani mwake.
“Chiba, hii mbona kali, ina maana sakata hilihili ndilo limfanye aondolewe maisha au kuna lingine nyuma yake?” Madam S aliuliza na Chiba alibaki kamkodolea macho akiwa hajui la kufanya.
“Na kwa nini wafanye hivyo?” akauliza kama mtu aliyegutushwa usingizini.
“Mi na wewe tutajuaje? Cha muhimu ni kumsaka muuaji yeye ndiye atatupa jibu la haya yote,” Madam akaongea huku anagonga-gonga kwenzi katika meza yake ya ofisi.
“Wanataka kupoteza ushahidi, si unajua huyu bwana Msesema na wenzake wameshikia bango lile swala la upotevu wa mabilioni!” Chiba alikazia huku akinyanyuka.
“Una uhakika Chiba au na wewe unaamua kupiaga ngumi kichakani,” Madam aliongea kwa sauti ya chini.
“Vyovyote vila Madam S, itakayempete huyohuyo, watu lazima waangalie, wewe unajibebea mabilioni wakati mahospitali ahayna dawa wala vifaa tiba, mashule hayana mahabara wala madarasa yanayokidhi mahitaji, watu vijijini wanakunywa maji pamoja na ng’ombe maana hawana miundo mbinu, barabara mbovu nchi nzima, reli tangu ajenge Mjerumani miaka hiyo. Huu ungekuwa wakati muhimu wa kuboresha haya yote lakini wachache na sijui wana matumbo ya aina gani wanajikusanyia mabilioni yote hayo, uroho umewajaa,” Chiba alilalama.
“Kama ni kweli,” Madam alidakia.
“Ee kama ni kweli,” Chiba akamalizia.
“Mi sina uhakika,” madam akaongeza.
“Hata mimi pia, sina uhakika,” Chiba akamalizia.
“Kamanda mimi nimemaliza,” Dr. Jasmine alimwambia Amata huku akishuhsa glasi yake iliyokuwa tupu.
“Najua, na asante sana, lakini inabidi uwasilishe taarifa hiyo kunakohusika haraka sana ili taratibu nyingine zichukue nafasi,” Kamanda alieleza.
“Sawa boss.”
Wote wakanyanyuka na kuiacha meza wazi, wakatembea taratibu kuifuata barabara inayoelekea ukumbi mkubwa wa Bunge huku wakiendelea kuongea na vicheko vikitawala. Wakiwa wanatembea kandokando ya barabara eneo la Jamatini, mara ghafla bahasha iliyokuwa katika mkono wa Jasmine ambayo ilibeba taarifa ya vipimo vile ilinyakuliwa na mtu mwenye mkono mwepesi kama Kipanga. Jasmine hakuelewa kilichotokea wakati ile pikipiki ikipita kasi juu yake kukiwa na watu wawili ikielekea barabara ya Dar es salaam. Kamanda Amata akili yake ikalielewa vyema tendo hilo, akatazama kushoto na kulia, akakuta kuna pikipiki zilizoegeshwa pembeni, akaivuta moja na kukaa juu yake, akachomoa pini iliyobana tai yake na kuipachika katika tundu la ufunguo, akapiga stata na kuingia barabarani, waendesha bodaboda wote wakaanza kushangilia.
“Kamandaaaaaa!!!!” Jasmin aliita, Kamanda Amata akaweka mguu chini na kusubiri mwanadada huyo aliyeirukia pikipiki hiyo aina ya boxer kwa usatdi wa hali ya juu; kisha wote wakaondoka kwa kasi. Walifika kwenye mzunguko wa stendi kuu, Kamanda Amata akapepesa macho kutazama watu wale wameelekea wapi, akawaona wakipotelea kwenye barabara kuu ya kwenda Morogoro, naye akawafuata. Ulikuwa ni mfukuzano wa aina yake. Kamanda vAmata alihakikisha hawapotezi watu hawa, “Jishike Jasmin !” alipiga kelele, na Jasmin akalikamata tumbo la Amata barabara akivishakanisha kiganja vya mikono yake kwa mbele, Amata alionesha umahiri wake katika kuiongoa pikipiki hiyo akiyapita magari makubwa na madogo. Lorikubwa la mizigo lilikuwa mbele yao, wale jamaa wakawa wanalipita lile lori ili wapate nafasi ya kuendelea na safari yao, Kamanda Amata aliuona uzembe wao wa kuamua kunyoosha na barabara hiyo. Walikuwa wakikaribia mataa ya njiapanda ya Area C mbele kidogo ya chuo cha CBE.
“Jishike vizuri Jasmine, nafanya manuva,” alimpigia kelele Dr. Jasmine aliyekuwa nyuma naye akamshika sawasawa; Kamanda Amata aliyumba ghafla na kuingia upande wa kushoto wa lile lori wakati wale jamaa wakiwa upande wa kulia wa lile lori, pikipiki aliyokuwa nayo Kamnda Amata ilikuwa ikiongeza mwendo kulipita lile lori na wakati huo huo upande wa pili wa lori wale jamaa nao walikuwa wakiongeza mwendo kuwahi taa za kijani. Amata alipolimaliza lile lori tu akarudi kulia na kusababisha mtafaruku, maana dreva wa lori alifunga breki kali na kusababisha kelele na harufu kali ya mipira kusambaa eneo hilo, nukta hiyo hiyo Jasmine alikuwa kama aliyezinduka, aliutoa mguu wake kwenye pedo maalumu ya kuegeshea mguu upandapo pikipiki na kumpiga teke la kukanyaga yule dereva wa ile pikipiki nyingine, yule bwana akayuba vibaya, alipojaribu kuiweka sawa pikipiki akarudi tena upande wa Amata, na wakati huo kamanda Amata alikuwa katika uelekeo wa kukatisha barabara, akamgonga kwenye tairi la mbele na ile pikipiki ikaanguka barabarani, gari zilizokuwa zikipita hapo zililazimika kufunga breki kali na kusababisha mtafaruku mkubwa, kizaazaa. Dr. Jasmin tayari alkikuwa amekwisharuka chini na kusimama imara, alivuta teke kali lililotua usoni mwa dereva wa ile pikipiki, akarudi chini kinyumenyume, yule aliyekuwa kama abiria akiwa anajiokotaokota alipata teke la mbavu na kabla hajatulia alikanyagwa mgongoni, Dr. Jasmine alikuw amefura kwa hasira, mishipa shingo ikiwa imemdinda, aliinama na kuiokota ile bahasha. Amata aliicha pikipiki ile, na kusimama chini kwa miguu yake miwili, almkamata yule jamaa aliyekuwa dereva ambaye alikuwa kainuka kwa minajiri yan kukimbia, alimkwida shati lake na kumtazama huso, alimshushia ndosi mbili za katika paji la uso.
“Wewe ni kibaka ee?” akamuuliza.
“Ha- ha- hapana,” yule jamaa akajibu huku akionekana wazi kuwa kichwa chake kilipoteza mtandao.
“Sasa nani aliyekutuma ufanya hili mlilofanya?”
“Tajiri mmoja, tajiri katupatia pesa tumpelekee hiyo bahasha,” akajibu huku bado akiwa katika himaya ya Kamnda Amata.
“Unajua ndani ya bahasha hiyo kuna nini?”
“Si – si – juuuiiii,” alijibu huku kamasi lililochanganyika na damu likimdondoka. Kamanda alimtikisa kwa nguvu na kumuachia akajibwaga chini kama mzigo na wakati huohuo gari ya polisi ilifika eneo lile.
“Afande, kamata hawa niwakute kituo cha kati, msiwahoji lolote mpaka nifike,” akatoa amri huku akimuonesha yule afande upande wa ndani wa koti la suti yake ambapo macho ya afande huyo mdogo police constable yalikutana na nembo ya dhahabu ya usalama wa taifa. Alimgeukia Gina ambaye tayari alikuwa kamuacha yule bwana nusu mfu kwa kichapo cha maana.
“Vipi?” Amata alimuuliza Gina.
“Nilishakwambia sipendi kupiga maana mi nikipiga huwa nakuua au nakuacha kwenye coma,” alimjibu Kamanda Amata huku wakitoka nje ya barabara akiikokota ile pikipiki.
KITUO CHA POLISI DODOMA
“Nani aliwatuma kuchukua ile bahasha?” lilikuwa swali kutoka kwa polisi mmoja aliyekuwa akiwapa kichapo wale jamaa ndani ya chumba maalumu cha kuhojiana kwa shuruti. Hali za watu hao zilikuwa taabani kwa kutotoa ushirikiano na jeshi la polisi.
“Unawaonaje hawa?” Jasmine alimuuliza Amata kutoka chumba cha pili.
“Hawa ni majambazi, sio madereva bodaboda, tazama walivyo majeuri kujibu,” Kamanda Amata akajibu huku akiishusha mikono yake kutoka kifuani alipoikutanisha, “Wanaleta mchezo.” Akazunguka na kuingia katika kile chumba alichokuwa yule mtuhumiwa, akamwomba yule askari asogee pembeni. Amata akamtazama yule jamaa kwa jicho baya.
“Sasa ongea na mimi na kama hutaki basi hapa utataka tu,” akakohoa kidogo, “ Naimbie nani aliwatuma kuipora ile bahasha?” akamtazama lakini yule mtu hakuonekana kujibu. “Unajifanya sugu si ndiyo?” Amata akasimama na kumpa ishara yule askari, akatoka nje na kuja na kitu kama banio lililobana jiwe la mviringo katika miisho yake, Kamanda akamwambia yule mtu aoneshe viganja vya mikono yake, avifungue, naye huku akitetemeka akafanya hivyo, lile jiwe likawekwa katika kiganja cha mkono wake wa kushoto, lilikuwa ni jiwe la moto sana lililotoka kwenye jiko la mkaanga chipsi.
“Aaaaaaaiiiiigggghhhhhrrrrr!!!! Nasema afande, nasema,” alilia kwa uchungu huku mkono wake ukiwa umeshikwa kwa nguvu na mkono wa Amata.
“Sema!”
“Ni tajiri, ni tajiri, ni tajiri!” alilalama.
“Tajiri nani?”
“Tajiri mgeni, uuuuiiiii mama, simjui, simjui jina lake,” alilia kama mtoto. Baada ya kibano cha maana kutoka kwa Kamanda Amata yule bwana, akaeleza tu kuwa alikabidhiwa hiyo kazi na mtu asiyemjua, ambaye alimkuta kijiweni kwake. Zaidi ya hapo hakuwa na maelezo yoyote zaidi ya kulia kama mtoto, mkono wake ulikuwa umeungua vibaya kwa moto wa lile jiwe.
Kamanda Amata alitoka nje ya chumba kile, “Mpakieni kwenye gari huyo, akatuoneshe mtu aliyemtuma,” akamwambia askari aliyekuwa eneo hilo la mapokezi. Yule bwana akachukuliwa akiwa na pingu mikononi na kupakiwa kwenye gari ndogo yenye vyoo vya giza, gari inayotumiwa na polisi kitengo cha upelelezi katika kutimiza majukumu yao.
Dakika chache baadae walikuwa tayari katikati ya mji wakielekea kijiweni kwake, kijiweni anakoegesha pikipiki yule bwana. Walipofika na kuonesha kuwa ni hapo, nje tu ya lango la hospitali ya mkoa, Dr Jasmine aliteremka na kuwaendea wale waendesha bodaboda, akasimama kimya akiwaangalia wale vijana waliojipanga wakisubiri abiria.
“Dada hii hapa!” mmoja aliita huku akiwa tayari amemfikia.
“Hii huku ina muziki dada ‘angu,” mwingine alidakia.
“Hapana, kuna mtu namtafuta mnamjua Kaduma?” akawauliza.
“Ndiyo tunamjua, lakini hayupo hapa katoka kama saa hivi imepita,” wakamjibu.
“Kaenda wapi?”
“Alipata mteja akaondoka naye,” Yule kijana akaeleza.
“Kaduma leo kawini maisha, wale jamaa walikuwa na mahela bwana, mmoja akaenda naye mwingine akabaki,” kijana mwingine akadaki.
“kwa hiyo atarudi kumchukua aliyebaki?” Jasmine akauliza.
“Hapana, Yule mwingine alimleta mwenzake yeye aliingia hapo café” Yule kijana akaeleza.
Wakati wote wa mazungumzo hayo; Kamanda Amata alikuwa akisikiliza ndani ya ile gari, aliposikia tu kuwa huyo mtu kaingia hapo café, akashuka kwenye ile gari na taratibu akapita palepale walipo wale vijana na kuvuka barabara hadi kwenye café hiyo iliyotajwa. Akazikwea ngazi na kuingia ndani ya mgahawa huo, akavuta kiti na kuketi nyuma kabisa karibu na mlango akisikiliza maelekezo wanayoampa Jasmine.
“Alivaaje huyo mtu? Unaweza kukumbuka,” jasmine aliendelea.
“Shati kama la kitenge Fulani hivi, yale mashati ya kisasa, kama kitenge hivi lilikuwa la rangi nyeusi na maua meupe, chini alikuwa na suruali nyeusi,”
“Sio nyeusi ni kijivu ya kitambaa,” mwingine akadakia.
“Basi asanteni nilitaka nijue tu kama aliondoka nae au la, asanteni,” Jasmine aliwashukuru.
Kamanda Amata aliangaza macho na kuona mtu aliyevali kadiri ya maelekezo hayo, akainuka na kukiendea ile meza ambayo Yule bwana alikuwa ameketi akipata sharubati.
“Naomba Coke baridi na bilauri tafadhali,” Amata alimwambia mhudumu. Uso kwa uso alikuwa ameketi na Obobo aliyevalia kofia pana kichwani mwake. Aliinua uso wake na kukutana macho na Amata aliyeonekana kuwa na utulivu usio na waa lolote.
“Habari,” Amata akamsalimia mwenyeji wake, lakini Yule mtu hakujibu kasha akaendelea na hamsini zake huku Kamanda Amata akinywa taratibu kinywaji alicholetewa muda huo. Obobo alionekana kutazama saa yake kila wakati, na kugeuka geuka nje mara kadhaa, alikuwa mwenye wasiwasi Fulani.
Baada ya dakika kadhaa alisimama na kulipa chakula chake kasha taratibu akatoka ndani ya mgahawa ule huku mkononi akiwa na gazeti la The Citizen.
“Mfuate anakoelekea, niko nyuma yako,” Kamanda akajisemea na Jasmine akaupata ujumbe uloe moja kwa moja kupitia heleni yake aliyokuwa ameivaa sikioni mwake. Akajitoa pale kwa waendesha boda boda na kuingia katika taksi mojawapo iliyokuwa maegeshoni.
“Ifuate ile gari, ileee ya njano,” Jasmine alimwambia dereva. Wakatoka maegeshoni na kuifuata hiyo gari.
“Unamjua Yule mtu?” dreva akauliza.
“Ndiyo, tupo pamoja,” Jasmine alijibu wakati ile gari ikichukua barabara kuelekea upande wa sokoni.
“Hakikisha hapotei machoni pako. Niko nyuma yenu nakuja,” sauti ya Amata ikalifikia sikio la Jasmine.
“Vipi bado au tayari, maana naona ukimya unaingia,” Yule dereva sksmwuliza Jasmine.
“We nimekwambia ifuate. Dhida yako nini!” Jasmine alimjibu kwa hasira.
§§§§§