Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Jumanne Muliro ametangaza kuanza kwa operesheni maalumu dhidi ya Makundi ya matapeli wanaojihusisha na vitendo vya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, akisema Jeshi la Polisi limetangaza “kiama cha kisheria” dhidi yao.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Agosti 4, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa Central Police Jijini Dar es salaam, SACP Muliro amesema matapeli hao hutumia mbinu mbalimbali kuwalaghai Wananchi, ikiwemo kujifanya Wafanyabiashara wa madini, Wauzaji wa magari na viwanja, Wanunuzi wa mazao kama korosho na dengu, pamoja na watoa huduma za usafirishaji wa mizigo, kisha kutoweka baada ya kupokea fedha kutoka kwa waathirika.
Amesema Jeshi la Polisi limeendelea kupokea malalamiko kutoka maeneo mbalimbali Nchini, yakiwemo Newala, Kibondo, Kasulu na Mbinga kuhusu Wananchi waliopoteza fedha kupitia udanganyifu huo.
Kutokana na hali hiyo, Muliro amesema operesheni hiyo itaendelea hadi Watuhumiwa wote watakapobainika na kufikishwa kwenye Vyombo vya Sheria, akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi halitavumilia vitendo vinavyowaumiza wananchi na kuhatarisha usalama wa uchumi.
Aidha, ametoa wito kwa Wananchi kuendelea kutoa taarifa kuhusu viashiria vya uhalifu ili kusaidia kuzuia na kudhibiti matukio ya kihalifu kabla hayajatokea.