SEHEMU YA PILI
OBOBO alitulia kwenye kibaraza kilichojengwa upande wa pili wa chumba chake. Lakini macho yake yote yalikuwa ni kuangalia wanaofika katika hotel hiyo, miwani aliyovaa ilimuwezesha kuona vizuri kabisa watu waliokuwa wakifika hotelini hapo. Obobo alikuwa akitaka kutekeleza lile alilotumwa usiku huo. Aliitazama saa yake ilikuwa yapata saa tano usiku, na alimuona huyo anayemchunga akiingia ndani mwake na kimada ambapo bila shaka ni changudoa kwa jinsi alivyovaa, alitega sikio pindi atakapotoka tu atamsikia hivyo hapo angejua afanye nini.
Bwana Msesema alikuwa na shughuli nzito na mwanmke aliyempata siku hiyo, mchaka mchaka haukuwa wa kawaida, kelele za kitanda nazoz zikajitahidi kunogesha burudani hiyo. Zikapita dakika kama kumi na tano hivi za ukimya, mara ukasikika mvutano kati ya wawili hao.
“Nilikwambia laki moja,” sauti ya kike ikasema.
“We mwanamke usiniletee nuksi mi nilisema elfu hamsini kama utapitisha usiku mzima na mimi, sasa haya masaa mawili tu unataka laki moja!?” akasikika Msesema akiunguruma kwa sauti yake ya kiume.
“Haya yaishe acha ubahili, we una minoti ya eskro halafu mi kunipa laki tu unawaka, tutaona utafika wapi na hiyo mihele yako, wizi tu umekujaa, Watanzania wanakufa nyi mnajichotea tu,” akaendelea kulalama yule mwanamke, “Haya nipeleke mimi,” akaongeza.
Kama kuna sentensi ambayo ilikuwa ikisubiriwa na Obobo basi ni hiyo, akaivuta bastola yake kubwa yenye kiwambo cha sauti, akaitia ndani ya koti lake kisha akanyanyuka na kutoka mlangoni kwake, akashika korido ya kuteremka chini, huku nyuma yake Msesema akaifuatana na yule binti anayelingana na mwanaye kiumri.
Alifika chini na kusimama pembezoni mwa ua kubwa nje ya hotel hiyo, akasubiri aone kitakachoendelea.
Msesema na kidosho wake wakaingia ndani ya V8 kubwa la kisasa wakajifungia milango na gari ile ikaondoka taratibu.
Obobo alijaribu kufikiri jinsi ya kummaliza Msesema lakini hakupenda kumdhuru binti huyo. Akatazama huku na kule na kuiona gari moja iliyokuwa haijafungwa kioo cha mbele, ‘Bingo!’ akajisemea kisha akaiendea na kuitoa lpki za milango akaketi ndani yake akafunga mkata na kuitekenya gari hiyo kwa funguo zake za bandia, akaiweka barabarani, akawa nyuma ya gari mbili na mbele kabisa ilikuwa ile ya Msesema. Wakaifuata barabara ya Bahi kuja Dodoma mjini, walipokaribia mzunguko wa kugawanya njia, Obobo akaongeza mwendo na kuchomoka kushoto. Kwa mwendo wake hakuweza kuipita ile V8 kwa jinsi ilivyokuwa ikikimbia, akajaribu kutafuta usawa mzuri akalenga tairi la mbele kwa bastola yake. Risasi iliyoachiwa haikufanya makosa, ilifumua tairi la mbele kushoto, Obobo akapunguza mwendo alipoiaona ile V8 ikiyumba na kukosa muelekeo. Msesema alijaribu kuiokoa huku na kule, alipoirudisha kwa nguvu kulia, ikamzidi nguvu, ikagonga nguzo ya taa, ikarudi barabarani ikapitiliza na kuingia kwenye ukuta wa round about ikapanda na kunyanyuka ikajibwaga juu yake ikiwa chali. Obobo akavaa sox usoni kwa haraka, akaegesha gari yake pembeni na kushuka, akaelekea katika ile V8, akachumgulia na kumku Msesema akiwa kabanwa na mkanda wa gari, akachomoa bastola yake kwa mara nyingine, akafyatua na kumpiga risasi Msesema pembeni kidogo mwa kifua chake. Obobo akatoka na kurudi garini wakati huo watu walikuwa wakija kwenye eneo la tukio ingawaje ilikuwa ni usiku. Obobo akawasha gari na kuondoka mpaka chuo cha mipango, akaiacha ile gari na kurudi akitembea kwa miguu yake miwili.
Alipohakikisha ameiacha mbali ile gari akasimamisha tax na kurudi tena mpaka pale ilipotokea ajali, akajifanya kushangaa, wakapita na kuelekea mpaka hoteli ya Bahi, Obobo akalipa pesa na kurudi chumbani kwake.
“One down two to go,” akasema kwa sauti ya chini, kisha akajipumzisha kitandani kusikiliza kinachoendelea.
Taarifa mbaya kama hizo husafiri haraka kama pepo za kusi. Haikuchukua dakika ishirini viongozi wa chama na serikali walikwishapata taarifa za ajali hiyop mbaya kila mmoja alichanganyikiwa kwa namna yake. Hakuna aliyeweza kujizuia kuangusha chozi lakini ukweli ndio ulikuwa huo, Msesema alikufa kwenye ajali ile.
Mheshimiwa Matata akapigiwa simu usiku huo na kujuzwa juu ya taarifa hiyo mbaya, alikurupuka na kukiacha kitanda akajiandaa harakaharaka na kuingia katika gari kuelekea hospitali ya serikali ya mkoa wa Dodoma. Alifika na kukutana na maswahiba zake kila mmoja akiwa anaongea lake, lililovuma zaidi ni kitendo cha kuwa na kimada ndani ya gari. Bila kuchelewa, polisi waliingia kazini kuanza kuchunguza juu ya ajali hiyo. Vilio na simanzi vilitawala, ulikuwa usiku wa majonzi.
§§§§§
Madam S alipata taarifa hiyo majira ya saa saba usiku akiwa tayari amejilaza kitambo akiendelea kutembelewa na njozi mbalimbali zilizouburudisha ubongo wake.
Mwili ulimsisimka, akabaki kashika simu mikononi mwake kana kwamba hakuamini anachoambiwa na huyo aliyekuwa akipiga simu.
‘Itakuwaje?’ akajiwazia.
Madam S alitulia kidogo kisha akawasiliana na wanausalama wengine, kujua kinachoendelea, akapata maelezo yote ya jinsi ajali hiyo ilivyotoke. ‘Ajali,’ akajiwazia, akaanza kupata mashaka na jambo hilo, ‘lakini ajali haina kinga,’ akajipa moyo na kuendelea kulala usingizi. Madam S alikuwa akimfahamu vizuri sana bwana Msesema kutokana na wadhifa wake serikalini, alikuwa ni mtu anayependa kupigania haki ya wanyonge, kusema ukweli pale unapopindishwa, alitokea kupendwa sana na wenzake watatu ambao Watanzania waliwapa jina ‘Askari wa miamvuli,’ kutokana na tabia yao ya kuibua mambo yaliyo chini ya kapeti. Kipindi alichokufa ilikuwa ni kipindi muhimu sana kuwa na mtu huyo kwani ndiyo kwanza yeye na wenzake walikuwa wameibua uozo, ufisadi na wizi mkubwa wa mamilioni ya shilingi kama sio fedha katika akaunti maalumu ya kuhifadi fedha za mradi wa nishati.
Sakatia hilo lilikuwa kubwa kila mtu akawa analiangalia kwa jicho lake, lilisababisha malumbanoi makubwa kila mmoja kumuoneshea mkidole mwingine, wananchi nao wakaamua kuingia barabarani kuandamana juu ya hilo. ‘Tunataka fedha zetu’ kikawa kilio cha kila Mtanzania.
Madam S akakumbuka mara ya mwisho mtu huyo alipokutana naye waliongea mengi kwa kirefu lakini pia mambo mengi aliyoyaongea yalikuwa ni kama anahashiria kifo chake.
§§§§§
Kamanda Amata aliwasili Dodoma alfajiri ya siku hiyo ambayo kifo cha Msesema kilitokea, moja kwa moja akaenda na kupanga chumba Kenya Lodge, alifanikiwa kupata kimoja ijapokuwa watu wengi wa serikali walikuwa huko na inasemekeana kukiwa na shughuli yoyote ya kiserikali huwa si rahisi kupata chumba.
Kamanda Amata akaweka kila kitu vizuri katika chumba chake, vitega usalama vyote muhumu alivitega ndani ya chumba hicho kilicho ghorofa ya tatu juu. Akaagiza aletewe gazeti kisha yeye akajipumzisha kidogo kwani alikuwa na uchovu sana.
Akiwa katikati ya usingizi alisikia simu yake ikifurukuta, akainyakua, sio yenyewe, mfurukuto ule ulikuwa ukitoka katika simu yake ya siri, akaitoa na kuitazama, ‘TSA 0’ akashangaa kidogo maana simu hiyo ikiitwa moja kwa moja huwa anajua ni kazi ya hatari inamkabili. Akainyakuwa na kuiweka sikioni.
“Kuna ajali imetokea hapo, bwana Msesema amefariki dunia, hebu fuatilia unipe habari kamili,” ile simu ikakatika. Kamanda akakaa kitandani kwa muda akifikiria simu hiyo. ‘Ajali, madam anambie nifuatilie ajali, kwani mi traffic police? Any way, yeye akisema ujue kuna jambo,” akanyanyuka na kuingia maliwato, akajiswafi na kutoka. Akachagu suti nzuri kati ya alaizotembea nazo, ilikuwa suti nyeusi, aliyoitangulizia shati jeupe bila tai, miwani nyeusi iliyaficha macho yake, akatoka chumbani akiwa mtu mwingine kabisa. akazishuka ngazi na kupita katika kaunta ndogo.
“Nipe savanna moja baridi tafadhali, na toti moja ya GIN,” Kamanda akaomba.
“Umepata, sema linguine,” mhudumu wa kaunta akamwambia huku akimpatia alichohitaji. Kamanda Amata akachanganya madawa yake na kupiga tarumbeta kinywaji chote, aliposhusha glass ilikuwa tupu.
“Hilo linguine ntakwambia baadae,” akamwambia yule mhudumu na kumpa noti ya elfu kumi, “keep change mtoto mzuri,” akamwambia huku akiicha kaunta na kuondoka.
Kwa mwendo wa mguu, Amata alkatiza barabara chache na kuwasili katika lango kuu la hospitali ya mkoa wa Dodoma, alipita getini na moja kwa moja akafika eneo la chumba cha kuhifadhia maiti, baada ya kuongozwa na mhudumu wa chumba hicho, kamanda Amata aliuona mwili wa Bwana Msesema ukiwa katika mfuko maalumu.
“Naweza kuonana na uongozi wa hospitali?” aliomba Amata.
“Bila shaka, inawezekana,” yule mhudumu alimjibu na kumuongoza mpka kwa mganga mfawidhi wa hospitali hiyo.
“Karibu sana, karibu kiti,” Mganga mfawidhi Dr Chilonwa alimkaribisha kitini Kamanda Amata, naye akaketi. Baada ya kuijitambulisha kama kawaida yake.
“Nilitaka kuona kama kuna taarifa yoyote ya uchunguzi wa mwili wa bwana Msesema,” kamanda aliomba kwa Mganga mfawidhi.
“Mwili wa bwana Msesema umechunguzwa na mganga mkuu wa mkoa kwa niaba ya serikali, hivyo taarifa zote wanazo wao hapa bado hawajaleta kopi,” yule Mganga akamueleza Amata. Kwa sekunde chache kamanda Amata alichukua uamuzi wa kuonana na mganga mkuu wa mkoa ili kujua nini kimepatikana kwenye mwili huo, aliagana na Dr Chilonwa akatoka nje ya hospitali hiyo.
Usafiri wa tax ulikuwa ni usafiri mahsusi kwa Amata muda huo, kabla ya kuonana na mganga wa mkoa aliamua kwanza kuingia katika ofisi za serikali zilizojengwa katika eneo la Makole.
“Nisubiri hapa, nakuja sasa hivi,” alimwambia dereva tax na kumuachia noti ya shilingi elfu kumi, akapita getini na moja kwa moja akaingia katika ofisi mojawapo.
“Karibu kijana,” kamanda Amata alikaribisha na mwanamama aliyevaa nadhifu, suti nyeusi mbele yake juu ya meza kulikuwa na bendera mbili zikipepeza kuonesha ukuu uliotukuka wa mwanamama huyo.
“Asante mama, nimekaribia,” Kamanda aliitikia huku akiketi katika kiti kimojawapo kati ya viwili vilivyokua jirani kabisa ya meza hiyo.
“Enhe, niambie kamanda, maana ujio wako lazima una jambo, mi nakufahamu sana,” yule mama alianza mazungumzo.
“Ndiyo, mama nimekuja kukusalimia tu ni sikunyinmgi sana hatujaonana, lakini pia nakupa pole kwa kuondokewa na mmoja wa vijana wako machachri,” kamanda alitoa pole.
“Asante sana, japo hatuwezi kiupoa kwa sababu tukio lenyewe bado la moto, maana kama ulivyosikia ni ajali alipata jana usiku,” yule mama kiongozi akaeleza.
“Poleni, ni kitu ambacho mtu hakitegemei lakini basi hajali haina kinga,” Kamanda alitoa pole.
“Basi ndo hivo Kamanda, enhe niambie juu ya ujioi wako hapa,” Yule mama alimweleza Kamnda.
“Usihofu, nimepata taarifa ya huu msiba hivyo nimetumwa kuja kuwakilisha ofisi, lakini hata hivyo kusaidia uchunguzi, sasa sijui naweza kupata taarifa iliyopo ya uchunguzi juu ya kifo hichi?” kamanda akaeleza wazi tu juu ya shida yake.
“Hapa kuna taarifa mbili ambazo zote zimeingia asubuhi hii, kuna hii ya polisi nah ii ya daktari,” yule mama akampa Kamanda taarifa zote mbili. Kamanda Amata akazichukua na kuzitazama moja baada ya nyingine.
Taarifa ya polisi ilieleza tu kuwa gari ya mheshimiwa Msesema ilipoteza uelekeo baada ya tairi lake moja kupata pancha, na gari kupanda msingi wa barabara kabla ya kugonga ukuta wa round about na kupinduka matairi juu. Taarifa iliendelea kusema kuwa gari hiyo ilisota kuanzia eneo la pancha mpaka ilipoangukia kwa umbali wa mita kumi na tatu hii ikiwa na maana dereva alikuwa akiendesha kwa mwendo kasi wa kilomita katia ya 100 na 130 kwa saa.
Kamanda Amata akaweka pembeni taarifa ya polisi na kuchukua ile ya kidaktari iliyoonesha vipimo mbalimbali viliyotazamwa kitaalamu. Ilisema mwili wa marehemu una majeraha machache na mikono yote miwili ilivunjika, hakuwa na jeraha baya au hakuumia mahali pabaya sana zaidi ya vioo vikali vilivyoijeruhi vibaya sura yake na bati lililomkata vibaya katika kisogo chake.
“Uhhhhh!” kamanda akashusha pumzi baada ya kusoma taarifa zile.
“Nafikiri umepata jibu,” yule mama akamwambia Kamanda. Kamanda Amata akatulia kimya hakujibu lolote, baadaye akamtazama yule mama.
“Mheshimiwa, mimi nahitaji kurudiwa kwa hizi chunguzi zote mbili, nikiwa na maana kwamba ni vizuri serikali iwe na uhakika na hili, daktari kachunguza mwili wa marehemu, sawa, lakini mwili huo kaukuta tayari ukiwa hospitali, je alichukua muda kuwaona polisi waliopima ajali? Najua hilo sio lazima sana lakini, tuyaache nitakutafuta baadae,” Kamanda alikatisha maneno yake.
“Aaaah Kamanda endelea kusema, unajua wewe ukiwa na mashaka na kitu, basi ujue hata Ikulu ina mashaka, na mimi sipendi kuharibu kazi, kwa hiyo sema utakacho,” yule mama alimruhusu Kamanda kusema.
“Ni hivi, hatuna budi kuangalia kwa makini sana hii ajali, je ni vipi kama Msesema atakuwa ameuawa?” Maneno ya Kamanda yakamfanya yule mama aduwae kwa muda.
“Hivi inawezekana?” akauliza.
“Kwa nini isiwezekane mheshimiwa? Sisi ndo tunajua mambo haya yanayopita chini ya jamvi, naomba marehemu asizikwe kwanza mpaka ofisi yangu itakapokamilisha uchunguzi,” kamanda alioa oda kama kawaida ya kazi yake.
“Sawa kamanda, kwa kuwa ni wewe na ofisi yako imeona hilo basi nitatoa tu taarifa ya kusubiria kidogo kwa shughuli za kuaga mwili ili nikupe nafasi,” Mheshimiwa akamwambia Kamanda Amata.
“Sasa hutakiwi kumwambia mtu kama tunafanya uchunguzi huu wa siri,” kamanda akamwambia mheshimiwa.
“Usijali nalijua hilo,” akajibu. Baada ya hapo wa kaagana na kila mtu akaendelea na shughuli zake za kawaida.
Kamanda Amata alipokuwa anatoka katika ofisi ya mheshimiwa, alipishana na Land Cruiser Prado iliyokuwa ikiingia ndani ya viwanja hivyo, harakaharaka alipochungulia ndani alimuona bwana Matata akiwa ametuna kwenye kiti cha kushoto mbele. Matata alipata kitu kama mshtuko alipomuona kijana yule akitoka katika eneo lile. Mbele kidogo akateremka garini na kurudi kwa mguu kuingia ofisi ya Mheshimiwa.
Kamanda Amata aliingia kwenye tax aliyokuja nayo, lakini jicho lake lilinasa kitendo cha Bwana Matata kushukia njiani na kuingia kwenye ofisi ile aliyotoka Amata.
“Nipeleke, kituo cha polisi cha kati,” kamanda akamwambi yule dereva tax. Akaitoa ile gari kwenye maegesho ya jengo la bunge na kuingia barabarani kuja Jamatini, alipopita mzunguko wa kwanza pale stendi kuu akanyoosha mpaka mzunguko wa pili na kukunja kushoto akachukua barabara ya Iringa, alipovuka reki tu akakunja kulia kuelekea alikoamuriwa.
Mbele ya kituo cha polisi wa usalama barabarani pale Dodoma, kulipambwa na magari mengi yaliyobomoka na kubondeka kwa ajali mbalimbali. Kamanda Amata alipita katikati yake na kuifikia kaunta ya kituo hicho.
“Nikusaidie nini ndugu?” polisi mmoja wa kike aliyekuwa hapo alimuuliza Kamanda Amata huku akiendelea kuandika andika kwenye likitabu lake.
“Nahitaji kumuona RTO,” kamanda akamwambia yule WP.
“Kibinafsi au kiofisi?” akauliza yule WP.
“Kuna tofauti gani kati ya hayo mawili?” kamanda akauliza.
“Hapa mtu unamuona kiofisi tu lakini kibinafsi umuone nje hukohuko,” yule WP akajibu kwa nyodo huku akiendelea kuandika na kuwasikiliza wateja wengine waliokuwa hapo.
“Ok, nimekuja kibinafsi, naomba uniitie RTO hapa nje nimuone,” Kamanda akamwambia yule WP.
“Hivi we kaka, mbona una dharau na ofisi za watu?” akauliza yule WP akiwa amefura na kuacha kuandika.
Kamanda Amata akaamua kuzunguka kaunta na kupita bila kukaribishwa akaingia mwenyewe katika ofisi ya RTO, akamkuta akiwa bize na kuchakurachakura makaratasi lukuki pale mezani mwake.
“Karibu sana kijana,” yule RTO akamkaribisha Kamanda Amata.
“Asante afande,” kamanda akashukuru na kujitambulisha.
“Sasa afande shida yangu ni moja, najua una habari za ajali iliyotokea jana, ajali ya Mheshimiwa Msesema,” kamanda akaanza.
“Ndyo nakusikiliza,” RTO alimjibu
“Nimeiona taarifa ya uchunguzi, sasa ninaomba nionane na askari aliyepima ajali kuna mambo nataka kumhoji na pia nilione gari lenyewe,” kamanda akatoa ombi lake. Kutokana na uzito wa kazi yake haikuwa tabu. RTO akachukua simu ya upepo na kuibofya mahala Fulani.
“PC Omari Kihondo, ripoti kwenye ofisi ya RTO haraka iwezekanavyo, ova” akairudiarudia hiyo sentensi mara kadhaa, sauti nyingi zikawa zinapishana kwenye spika ya redio hiyo.
“PC Omary Kihondo, nimekusoma mheshimiwa, ova” sauti moja ikajibu kupitia redio ile.
Dakika kumi baadae, PC Omary Kihondo alikuwa amesimama kwa ukakamavu mbele ya bosi wake.
“Nimekuita hapa, kuna huyu kiongozi kutoka serikalini, anataka akuhoji maswala machache na kuichunguza upya gari ya mheshimiwa Msesema,” RTO akamaliza. Kamanda Amata akatoka na PC Omary Kihondo wakaelekea nje.
“Ndiyo bwana Omari,” kamanda Amata akaanzisha mazungumzo wakati wakizishuka ngazi za kituo hicho kulielekea gari iliyopata ajali, “Hebu nambie, jana ulipofika eneo la ajali ulikuta hali gani kwa majeruhi?” akauliza.
“Nilifika pale kwa kuchelewa kidogo, lakini nilikuta tayari Mheshimiwa amekwishakufa alikuwa amelazwa pembeni na wasamalia wema, nilichokifanya ni kutafuta usafiri wa mwili huo kufikishwa hospitalini, hii gari inaonekana ilipanda tuta la kutenga barabara baada ya kupasuka kwa gurudumu lake, ina maana liliyumba na dereva akakosa uongozo,” PC Omary akaeleza kwa ufasaha sana jinsi alivyoipima ile ajali, kiukweli alieleza kama alivyoandika hakuongeza wala hakupunguza.
“Ningekuuliza kama marehemu alifunga mkanda, lakini umeshasema ulichelewa kufika,” kamanda akazungumza.
“Inaonekana alifunga mkanda kwa maana tazama mkanda huu umekatwa kwa kitu kama kisu au wembe, labda wakati wanamnasua,” PC Omary akajibu. Kamanda Amata akaizunguka ile gari na kutazama huku na kule, alipofika eneo la kiti cha abiria, altazama kwa makini kulikuwa na damu japokuwa sio nyingi sana lakini zilikuwepo.
“PC, kwa jinsi ulivyoikuta gari inawezekana damu za marehemu kufika kwenye kiti cha pili?” kamanda akauliza.
“Hapana na haiwezekani, kwa sababu huyu marehemu lazima ameumia wakati gari ikitua chini, hivyo kama ni damu basi nyingi ndio hizi juu kwenye paa la gari,” Omary alijibu. Kamanda Amata aliangalia vizuri, akakumbuka ripoti ya daktari kuwa marehemu kaumizwa sana sehemu ya nyuma ya kichwa chake, lakini pale aliona tu bodi lililobonyea ambalo kama ni kumuumiza mtu halitaweza kumsababishia jeraha. Baada ya kazi hiyo iliyowachukua takribani saa moja, Kamanda Amata alimshukuru PC Omar akaagana na RTO na kuondoka zake.