Gavana wa Mombasa, Abdulswamad Nassir, amepata pigo baada ya Bunge la Kaunti kukataa kumwidhinisha Ofisa Mkuu mteule wa Idara ya Kawi na Mabadiliko ya Tabianchi.
Kwa mujibu wa mtandao wa Taifa leo, Gavana alikuwa amemteua John Kiprop katika nafasi hiyo, lakini madiwani wengi wamemkataa wakishangaa aliteuliwaje wakati hajui Kiswahili, mambo yahusuyo wadhifa huo na Kaunti ya Mombasa.
Kwenye mjadala mkali katika bunge la kaunti hiyo, baadhi ya madiwani, wameshangazwa na hatua ya mtu mwenye utajiri wa Sh41 milioni (pesa ya Kenya) kusaka ajira aina hiyo.
Mwakilishi wa Wadi Chaani, Kaunti ya Mombasa, Franklin Makanga, amenukuliwa akisema mteule huyo hajui Kiswahili ambayo ni lugha inayotumiwa zaidi Mombasa, na pia hajui mitaa ya mji huo.
“Hajui Changamwe, Chaani wala Bangladesh iko sehemu gani. Ataleta mabadiliko gani hapa Mombasa? Hafai na ninaomba bunge hili lisimpitishe,” amesema.
Kwa upande wa Mwakilishi Wadi ya Kadzandani, Fatma Kushe, amewataka madiwani wenzake kufanya uamuzi huru kuhusu watu wanaoteuliwa huku akisema: “Kama mtu hafai, hafai. Tusiogope mtu yeyote,” amesema.
Hata hivyo kwa upande wake Leila Nyache, ambaye ni Mwakilishi Wadi ya Kipevu, aliunga mkono uteuzi wa Kiprop huku akisema ni sifa za elimu yake zilizosababisha ateuliwe kwenye nafasi hiyo.
Nyache hakuwa peke yake, kwani Mwakilishi wa Junda, Sylvester Kai, amesema: “Kutoka Baringo isiwe sababu ya kumnyima nafasi hii. Hakuna sheria ambayo inamzuia mtu yeyote kufanya kazi mahali kokote. Si lazima awe mkazi ama mzaliwa wa Mombasa, tuache ubaguzi.”
Hata hivyo baada ya mjadala huo mkali, bunge la kaunti hiyo, lilikataa kumuidhinisha Kiprop kuitumikia nafasi aliyokuwa ameteuliwa na Gavana Nassir.