Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Kusini, imesema kuwa watu wanaotumia dawa ya ‘Vega’ bila kuwa na tatizo la shinikizo la damu, wako hatarini zaidi kupoteza nguvu za kiume na hivyo kushindwa kabisa kushiriki tendo la ndoa.
Akizungumza na Mwananchi Digital katika banda la maonyesho ya kilimo Nanenane, Mkaguzi wa Dawa TMDA Kanda ya Kusini, Elias Magambo, amesema kuwa matumizi ya dawa hiyo yanaongezeka kwa kasi, hali ambayo inaweza kuchangia vijana hao kutokuwa na nguvu kabisa.
“Hii dawa maarufu kama vega, imekuwa ikitumiwa na wanaume hasa vijana wadogo, kwaajili ya kuongeza nguvu za kiume, wakidai kuwa wanaenda kuwakomesha wanawake. Na wamekuwa wakiambizana na hivyo kufanya matumizi yake kuongezeka, hali ni hatari kwa vijana wadogo,” amesema Magambo.
Mkaguzi huyo wa dawa, ameongeza kusema: “Kwakweli hii dawa haifai kutumiwa kwakuwa inaweza kusababishia matatizo ya baadae kwa watumiaji kushindwa kushiriki tendo la ndoa na wenzi wao bila kuipata dawa hiyo…huathiri nguvu za kiume.”
Kwa mujibu wa Magambo, dawa hiyo ni maalum kwa watu wenye matatizo ya presha, hivyo wanatumia ili kuongeza msukumo wa damu mwilini, na iwapo itatumiwa na mtu asiyekuwa na ugonjwa huo, dawa hiyo humuongezea msukumo wa damu kwa kiasi kikubwa, na ndipo mtumiaji huhisi kuongezeka kwa nguvu za kiume.
Kwa upande wake Amina Hussein, mkazi wa Lindi, amesema kuwa wanaume wengi wamekuwa na tabia hiyo ya kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume, na kwamba jambo hilo limekuwa kama ni desturi.
“Wengi hufanya hivyo kama kutukomoa na wakiona sifa sisi kuwasifia bila kujali afya zao, nadhani hili linaweza kusababisha tukapoteza wanaume wanaojiamini ndani ya nyumba na matokeo yake ni janga” amesema Amina.
View attachment 2709286