Huyu ndie Franco, alikuwa na watoto 18, watoto 17 walikuwa wa kike...alizaa na wanawake 14..!
"'Umesikia jinsi anavyokuongelea vibaya kwa watu
Kwanini usitafute kazi yako Mario", hayo ni maneno ya Franco Luambo kwenye wimbo wake wa Mario.
Mario kilikuwa ni kisa cha kweli mwanaume msomi aliyekuwa ana ishi na kulelewa na wanawake huko Ureno.
Unapomtaja Franco hauwezi kuacha kuutaja wimbo wa Mario, unaachaje kuutaja wimbo uliouzwa zaidi ya kopi laki 2. Franco hakuwa Mario, alifanya kazi kwa bidii na kuachia ngoma juu ya ngoma, kuna mwaka mwamba huyu alitoa album 12 karibu kila mwezi alikuwa anatoa album moja.
Mpaka sasa watu wanabishana kuhusu idadi kamili ya album alizotoa Franco, wengi wanasema alitoa albums 85, na wengine wanasema alitoa album 150.
Nyimbo nyingi za Franco zilihusu maisha ya kila siku hasa mapambano ya ukoloni. Jina lake lilikuwa maarufu na kutamkwa na karibu kila mtu katika bara zima la Afrika.
Franco alizaliwa mwaka 1938 huko Kongo enzi za ukoloni wa Wabelgiji. Franco hakuwa msomi sana, aliacha shule akiwa na miaka 10 baada ya baba yake kufariki. Alijifundisha kupiga gitaa na kuanza kulisha familia katika umri huo mdogo.
Alikuwa rafiki mkubwa wa Rais wa Zaire Mobutu, hata hivyo urafiki wao haukudumu sana ukageuka uadui wa paka na panya.
Licha ya uadui wao, baada ya Franco kufariki Mobutu alitangaza siku 4 za maombolezo.
Franco alifariki mwaka 1989, alikuwa na umri wa miaka 51, vyanzo vingi vinasema Franco alifariki kutokana na ugonjwa wa UKIMWI.
Katika uhai wake Franco alibahatika kupata watoto 18, miongoni mwao watoto wakike walikuwa 17 na mmoja wa kiume. Alizaa na wanawake 14...!