Wanasheria waliofungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya kupinga makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi baina ya Serikali za Tanzania na Dubai, yanayohusisha uwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam, wameondoa shauri lao la maombi madogo ya kusimamishwa utekelezaji wa makubaliano hayo.
Wanasheria hao Alphonce Lusako, Emmanuel Kalikenya Changula, Raphael Japhet Ngonde na Frank John Nyalusi, walifungua kesi hiyo chini ya hati ya dharura wakipinga masharti ya baadhi ya ibara za makubaliano hayo.
Pamoja na kesi hiyo, pia wamefungua shauri dogo, wakiiomba mahakama hiyo itoe amri ya maelekezo kwa wadaiwa (Serikali) kusimamisha utekelezaji wa makubaliano hayo, kusubiri kumalizika kwa kesi ya msingi.
Hata hivyo kiongozi wa jopo la mawakili wa upande wa madai, Boniface Mwabukusi, amesema leo Alhamis Julai 20,2023 kuwa wameamua kuyaondoa maombi hayo baada ya kujadiliana na wateja wao ili kuiwezesha kesi ya msingi kusikilizwa na kuamuriwa haraka na kufuatia ushauri wa majaji wanaoisikiliza kesi hiyo.
(Imeandikwa na James Magai na Hawa Mathias)