Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM)-Bara, John Malecela ameshukuru miradi ya maendeleo iliyoanzishwa na Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoiendeleza.
Malecela ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu wa saba wa Tanzania ameyasema hayo leo Jumapili Juni 25, 2023 nyumbani kwake Kilimani, Dodoma alipokutana na waandishi wa habari kuzungumzia jitihada zinazofanywa na Rais Samia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Samia aliyekuwa makamu wa Rais kuanzia Novemba 5, 2015 baada ya uchaguzi mkuu huku Rais akiwa John Magufuli, aliapishwa kuwa Rais Machi 19, 2021 baada ya Magufuli kufariki dunia Machi 17.
Malecela amewataka Watanzania kumpa nafasi Rais Samia ambaye anafanya kazi usiku na mchana katika kuliletea maendeleo Taifa hili.
“Kwa mfano, katika Tanzania baada ya miezi 12, tukifika mpaka mwaka kesho reli ya SGR au reli ya mwendokasi itakapokuwa tayari, Watanzania tutakuwa katika dunia mpya, dunia ambayo unatoka Dar es Salaam mpaka Dodoma kwa saa tatu, saa moja na nusu Morogoro, saa moja na nusu Dodoma kwa treni ya mwendokosi.
“Na nadhani tutakuwa katika nchi chache za Bara la Afrika zenye aina hiyo ya usafiri. Sasa hii italeta maana gani, italeta maana kwamba wenzetu wa Rwanda, Burundi, Congo nao watafaidika, kwa sababu mizigo yao kutoka Dar es Salaam mpaka Kigoma itachukua muda mfupi zaidi,” amesema.