Daktari binafsi wa Benard Membe, Profesa Harun Nyagori amesema kifo cha mwanasiasa huyo kimechagizwa na ugonjwa wa maambukizi ya mfumo wa mapafu hewa.
Taarifa hiyo ya daktari inakuja kipindi ambacho kumekuwepo na taarifa mbalimbali katika mitandao ya kijamii kuhusu chanzo cha kifo chake.
Membe amefariki dunia leo, Ijumaa ya Mei 12, 2023 katika Hospitali ya Hubert Kairuki jijini Dar es Salaam.
Akizungumza nyumbani kwa marehemu, Profesa Harun amesema ugonjwa huo unasababisha mgando wa damu na kuzuia mapafu kupeleka hewa ya oksijeni.
"Hali hii inaweza kumkuta mtu yeyote mara tu anapopata maambukizi haya kwa njia ya hewa hata kwa wagonjwa wanaopata pneumonia pia inaweza kuwakuta.
"Kinachozungumzwa huko mtaani kwamba mzee ameuawa amepewa sumu sijui nini, hiyo iondoke, ukweli ni kwamba amefariki kwa maradhi ya kawaida," amesema Profesa Nyagori ambaye pia ni Mtaalamu wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).