Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Mei 23, 2022 kutoa uamuzi wa kesi ya aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu nchini Tanzania (CWT), Deus Seif na Mwekahazina wa chama hicho, Abubakari Allawi kama wanakesi ya kujibu au la.
Seif na Allawi wakabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kutumia madaraka yao vibaya kwa kuchepusha fedha kiasi cha Sh 13.9milioni ambacho ni mali ya CWT.
Washtakiwa hao wanadaiwa kutumia fedha hizo kwa ajili ya safari ya ndege kwenda Cape Verde, kuangalia mpira wa miguu, kati ya Taifa Stars na timu ya Cape Verde, kinyume cha sheria.
Uamuzi huo umetolewa leo, Mei 13, 2022 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Richard Kabate, baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao mashahidi 9 na vielelezo 11, walivyotoa mahakamani hapo dhidi ya washtakiwa .
" Upande wa mashtaka wamefunga ushahidi wao hivyo nahitaji muda kidogo ili niweze kupitia na kuja kutoa uamuzi, hivyo Mei 23, kesi hii itakuja kwa ajili ya kutoa uamuzi" Amesema Hakimu Kabate.
Kabla ya kuahirishwa kwa kesi hiyo upande wa mashtaka ukiongozwa na Iman Nitume akishirikiana na Veronica Chimwada, walikuwa na shahidi mmoja, Faustine Mashauri, ambaye ni Mtaalamu wa Maandishi kutoka Jeshi la Polisi.
" Mheshimiwa hakimu baada ya shahidi wetu huyu( Faustine) kumaliza kutoa ushahidi wake leo, naomba kuieleza mahakama kuwa upande wa mashtaka tumefunga ushahidi wetu" amedai wakili Nitume.
Nitume baada ya kueleza hayo, hakimu Kabate aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 23, 2022 itakapoitwa kwa ajili ya mahakama kutoa uamuzi.
Katika kesi ya msingi, Seif na Allawi, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 39/2021.