Wizara ya Afya imetangaza kufanya kampeni ya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Polio (chanjo ya matone dhidi ya Polio) kwa lengo la kukabiliana na hatariya ugonjwa huo kuingia nchini kutokana na muingiliano mkubwa na Malawi ambao kumetangazwa uwepo wa Polio baada ya Mtoto wa miaka mitatu katika Mji mkuu wa Malawi Lilongwe kugundulika na ugonjwa huo.
"Taarifa hii (ya Mgonjwa wa Polio Malawi) inakuwa ni mara ya kwanza kwa Bara la Afrika kutokea maambukizi baada ya kupita miaka mitano, ambapo ilipelekea ugonjwa wa Polio kutangazwa umetokomezwa katika ukanda wa Afrika mnamo mwezi Agosti, 2020"
"Duniani, ni nchi mbili pekee za Afghanistan na Pakistani ambako ugonjwa wa polio bado haujatokomezwa, hapa Tanzania kwa mara ya
mwisho mgonjwa wa Polio kugundulika ilikuwa mwaka 1996 ambaye alitokea Mkoa wa Mtwara, ilipofika Disemba 2015 Tanzania ilithibitishwa kuwa ni nchi isiyo na ugonjwa wa Polio"
"Malawi imepakana na Tanzania kupitia Mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Njombe na Songwe, hii inapelekea kuwepo kwa hatari ya ugonjwa huu kuingia nchini kutokana na muingiliano mkubwa wa kibiashara na shughuli nyingine za kijamii, kampeni ya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Polio awamu ya kwanza imefanyika katika Mikoa minne ya Mbeya, Njombe, Songwe na Ruvuma na awamu ya pili itafanyika mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar kuanzia Aprili 28, 2022 hadi 01 Mei 2022"