Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeishauri Chadema kuweka picha ya Rais katika ofisi za viongozi wa chama hicho kwa sababu hiyo ni taasisi ya umma.
Ushauri huo umetolewa leo Ijumaa Septemba 10, 2021 na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza wakati wakifanya ukaguzi wa chama hicho katika utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi.
Amesema ofisi za vyama vya siasa ni ofisi za umma hivyo ni vizuri wakaendeleza utamaduni wa kuwa na picha ya Rais kwenye taasisi za umma.
"Hii ni ofisi ya umma, ni vizuri kukawa na picha ya Rais ukutani, siyo unaweka picha ya katibu mkuu. Huu ni ushauri tumewapa, tutapita Januari kuona kama wamelifanyia kazi," amesema Nyahoza.
Akizungumzia suala hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema - Zanzibar, Salum Mwalimu amesema Msajili amekuta mambo yamekaa vizuri ndiyo maana akagundua hakuna picha ya Rais.