Pamoja na wasanii kumuunga mkono msanii mwenzao Diamond Platnumz katika kile kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kumpigia kura katika tuzo za BET alizochaguliwa kushiriki, baadhi ya wadau wanaona hastahili kuungwa mkono.
Wadau hao wamemkemea waziwazi kupitia mitandao ya kijamii wakidai kuwa hajalitumia vema jina lake la msanii mkubwa kukemea maovu, badala yake amekuwa akifanya mambo yake binafsi.
Baadhi ya wachangiaji suala hilo katika mtandao wa Twitter wamekwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa watawaunga mkono wasanii wa Nigeria anaoshindana nao kuwania tuzo hiyo katika kipengele cha ‘Best International Act’ wakiwamo Wizkid, Burna Boy, Emicida, Headie, Aya Nakamura, Youssoupha na Young T & Bugsey.
Hata hivyo mshindi wa tuzo hizo anachaguliwa na jopo la majaji 500 wa BET na hapatikani kwa kupigiwa kura.
Baadhi ya wasanii wamemuunga mkono wakitaka apigiwe kura, huku wengine wakimkumbusha ajiulize kwa nini watu wanahamasishana kutompigia kura (ingawa hakuna kura zitakazopigwa kutoka kwa wananchi katika tuzo hii).
Mwimbaji Ray C amemtaka Diamond kujiuliza kwa nini wakati huu wa tuzo za BET ndio mambo hayo yanatokea na sio kipindi cha nyuma ambapo ameshinda tuzo nyingi kubwa.
Ray C alidai kipindi cha katikati Diamond alikuwa msanii mwenye majivuno sana na kubeza wenzake, pia kitendo chake cha kucheka hadharani mara baada ya kuahirishwa tamasha la Fiesta Novemba 2018 ambalo linawahusisha wasanii wengine, ndipo alipotengeneza huo mpasuko unaonekana kwa sasa.