Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa ahirisho la mwisho katika kesi ya kuchapisha maudhui mtandaoni bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), inayomkabili msanii wa vichekesho, Idris Sultani na wenzake wawili.
Hatua hiyo imetokana na upande wa mashtaka kushindwa kupeleka mashahidi mahakamani kwa miezi mitano mfululizo, tangu Desemba 8, 2020 kesi hiyo ilipotakiwa ianze kusikiliza ushahidi.
Uamuzi huo umetolewa leo, Alhamisi Mei 27, 2021 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Yusto Ruboroga, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuendelea.
Hakimu Ruboroga amesema tarehe ijayo kama upande wa mashtaka hawatapeleka shahidi mahakamani hapo ataifuta kesi hiyo.