Watu takribani 3,000 wameukimbia Mji wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Goma kuelekea Rwanda leo Jumapili baada ya kutokea kwa mlipuko wa volcano katika Mlima Nyiragongo.
Balozi wa Rwanda nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo Vincent Karega amesema ———“mipaka iko wazi na Majirani zetu wanakaribishwa kwa amani"
Serikali nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeagiza Watu waondolewe kutoka Mji wa mashariki wa Goma, baada ya kutokea mlipuko huo wa volcano katika Mlima Nyiragongo uliopo karibu na Mji huo wa mpakani.
Afisa mmoja katika hifadhi ya kitaifa ya Virunga iliyopo kwenye eneo ambako volcano imelipuka amesema hadi hii leo asubuhi tope la moto linalotiririka kutoka kwenye Mlima Nyiragongo limefika kwenye uwanja wa ndege wa mji huo wa Goma na kwamba hali inazidi kuwa mbaya.
Afisa huyo amesema anahofia kwamba tope hilo la moto (Lava) linaweza kufika hadi kwenye fukwe za ziwa Kivu na kusema mlipuko huo unalingana na ule uliotokea mwaka 2002 na amewataka Raia waondoke mahala hapo haraka.