Huko nchini Scotland katika miaka ya 1500's - 1600's kulikuwa na mtu hatari sana aliyejulikana kama Alexander "Sawney" Bean. Maisha aliyokuwa anaishi huyu jamaa ni ya kutisha haijawahi tokea, alikuwa anamiliki watu, yaani kama jinsi watu wanavyomiliki mifugo kama kuku, n'gombe au mbuzi basi ndivyo jamaa naye alivyokuwa anamiliki watu.
Nikizungumzia watu katili niliowahi kuskia simulizi zao hapa duniani, basi huyu jamaa nimemvulia kofia. Bean alikufa kwa kunyongwa kutokana na makosa ya kuwafanya binadamu wenzake nyama huku akiwa ameacha jumla ya watoto 29.
Kwa zaidi ya miaka 25 aliyaishi maisha hayo ya kinyama mapangoni mjini East Lothian. Alikuwa ameshawafanya nyama watu zaidi ya 5,000 na wengine bado walikutwa amewafungia.
Baada ya Bean kuhama nyumbani alienda kuishi mapangoni na mkewe Agnes Douglas huko Bennane Head nchini humo ambako katika maisha yao walifanikiwa kupata watoto sita, baadaye familia ikakua na kufika wanafamilia 45, hakuna aliyekua anajua mapangoni humo kama kuna watu wanaishi.
Yeye pamoja na wanawe walianza kuteka watu, wanawafungia mapangoni humo alafu wanawachinja na kuwala nyama kama jinsi tunavyokula mifugo yetu nyumbani. Mabaki walikua wanayatupa ufukweni hali iliyopelekea watu kuamini kuwa kulikuwa na wanyama wakali wanaokula watu, hawakujua kabisa kama kuna familia inaishi katika mapango hayo yaliyopo karibu.
Bean na familia yake hiyo kubwa waliendelea kufanya uhalifu huo hadi siku moja walipomvamia bwana mmoja aliyekua mjuzi kupigana, baada ya kuwadhibiti maadui akawapeleka kwa viongozi, ikabidi waongozane hadi mapangoni wakiwa na kikundi cha askari 400 wa mfalme James VI.
Kufika mapangoni walistaajabu kuuona ukoo mkubwa wa Bean ukiishi humo, mabaki ya miili yalikuwa mengi mnoo huku sehemu nyingine zikining'inizwa ukutani, miili iliyopatikana mapangoni humo kwa siku hiyo ilifika 1000, wengine walikuwa wamefungwa wakiwa wazima. Bean alikamatwa na kunyongwa siku hiyo hiyo.