Korti Kuu ya Kenya imesimamisha hatua ya serikali ya nchi hiyo ya kuzifunga kambi mbili za wakimbizi ambazo zinahifadhi mamia kwa maelfu ya wakimbizi kutoka nchi jirani zinazozongwa na mizozo ya kivita.
Jaji Antony Mrima wa mahakama hiyo ametoa amri ya kuisitisha hatua hiyo ya serikali kwa muda wa siku thelathini, kufuatia ombi la mmoja wa wanasiasa wenye ndoto za kuwania urais wa Kenya, Peter Gichira.
Awali, waziri wa mambo ya ndani wa Kenya, Fred Matiang'i, alikuwa amelipa shirika la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wakimbizi, UNHCR, muda wa siku 14 wa kuzifunga kambi za wakimbizi za Dadaab na Kakuma, akisema hakuna uwezekano wowote wa kujadiliana kuhusu uamuzi huo.
Muda huo ulimalizika jana. Kambi ya Dadaab inao wakimbizi wapatao 200,000 wengi wao wakiwa kutoka Somalia, nayo ya Kakuma inahifadhi takiribani idadi kama hiyo, wengi wao wakiwa ni wakimbizi wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini.
View attachment 1747641