Tafasiri Unavyoweza: Usijidanganye, Umoja Mbele Sawa, Haki na Uwazi Havikai Nyuma!
...kama unalijua hili, ukimya haujawahi kuwa njia sahihi ya kuelezea amani au umoja miongoni mwa wananchi wengi. Ipo dhana na inaonekana kukuzwa zaidi na watawala kuwa kuongea wazo tofauti lenye nia ya kujenga basi muongeaji anahatarisha umoja wa kitaifa (national unity). Siku zote watawala wanafanya yale yatakayowafanya wakae madarakani siku zote (hasa kwa nchi zetu), mifumo wanaitengeneza katika namna hata kama hawako madarakani basi waliopo madarakani watawalinda. Tafasiri unavyoweza.
Neno umoja limekuwa midomoni mwa watawala wote, kuanzia rais, waziri hadi wakuu wa wilaya, ukiwasikiliza wanavyoliongea utasema wanamaanisha. Midomo yao imejaa mate maana wanaongea wameshiba na wanaosikiliza wengi wamevaa mashati kupunguza njaa ya kukosa kazi, elimu bora, miundombinu rafiki ya kijamii na mambo mengine wanayoambiwa yapo hawayaoni. Haki za binadamu zinavunjwa kwa kisingizio cha kuleta maendeleo, haki inaminywa na katiba ya chama iko mbele ya katiba ya nchi, hatufiki kwa ukimya.
Neno umoja wa kitaifa linapotamkwa na kiongozi wa serikali kuwa makini, hata kama umekaa kimya, upe ubongo wako kazi ya kuchambua, usiyaachie masikio kusikiliza tu na kukariri. Mara zote kiongozi yeyote wa serikali aisema kuhusu kudumisha umoja wa kitaifa tambua kwamba anamaanisha mambo yafuatayo, usihoji matendo ya serikali, usihoji matumizi ya kodi yako, usihoji hali duni ya maisha kwa wengi. Ukihoji unaonekana mpinzani na utapata taabu sana. Tafasiri unavyoweza