Tafasiri Unavyoweza: Haijaanza Leo, Nyamaza Ukisubiri Kesho
Nitaandika bila kunukuu (rephrasing) maneno ya mwanahabari na wakili maarufu nchini Jenerali Ulimwengu ambaye alikaririwa akiandika kuwa tatizo kubwa la watawala ni kujiona wana akili zaidi ya watu wengine. Kwa kujiona na akili huku wao wanajiona si raia wa kawaida, ni watu spesho na wengine wote tufuate wanachotuambia. Nimemaliza kunukuu na kwa sababu hii nafunga hii nukuu kwa maneno haya, wanasiasa wanatufanya sisi ni kondoo. Wanafikira kwa niaba yetu wakijiona kuwa hatuna uwezo wa kufikiri. Tafasiri Unavyoweza.
Ninaandika haya kwa sababu ya taarifa ya waziri wa sheria akisema kuwa malipo yote ya madini na vitu kama hivyo yatakuwa hayatajwi hadharani ili kuwakimbia wadai wetu. Dawa ya deni ni kulipa, hakuna njia ya mkato. wamemaliza kujenga mageti makubwa kwenye nyumba zao, wamejiongezea walinzi na mbwa kuwalinda na sasa wanakuja na usiri. Ninakuandikia tu kwa nia njema, ukiona kiongozi anajiongezea walinzi, mageti kila kukicha na sasa anataka usijue pesa kiasi gani zimeingizwa na rasilimali za nchi basi huyu anakuibia, huhitaji kumaliza form four kulijua hili.
Usishangae, halijaanza leo, ni mwendelezo wa kubinya haki ya kupata taarifa, wamezima bunge, ila wanataka kujionesha wao kila wanapofanya vitukio vya kuwaonesha wao zaidi. Umimi unawatawala kuzidi maelezo na wengi wanajiaminisha kuwa watawala wako sahihi, wanasubiri warushiwe mapesa. Tafasiri unavyoweza