Makapuku Forum

Makapuku Forum

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 53
ILIPOISHIA:
Tukaanza kuulizana maana ya kile kilichofanyika mpaka tukafanikiwa kumuokoa Shamila ambapo Junaitha alianza kutufundisha mambo ambayo hakuna aliyekuwa akiyajua kati yetu, ambayo kama hujui ungeweza kusema ni uchawi wa hali ya juu.
“Hata ukitaka kuingia benki na kuchukua kiwango chochote cha fedha unachotaka, inawezekana, mbona rahisi tu, nitawafundisha,” alisema.
SASA ENDELEA...

“Mh!” niliguna kama ishara ya kutoamini kile alichokisema, akanigeukia na kuniambia hakuna kitu kisichowezekana chini ya jua. Alianza kutufafanulia jinsi nguvu zisizoonekana kwa macho zilivyo na uwezo wa kufanya chochote na kikatimia.
“Hujawahi kuona mtu anakunja kijiko kwa kukitazama tu au mtu anahamisha glasi ya maji kwa kuitazama tu?” alisema. Nilishawahi kusikia habari hizo lakini sikutaka kabisa kuziamini mpaka nishuhudie mwenyewe.
“Kabla ya yote nataka kujua nini kilichotokea mpaka tukafanikiwa kumuokoa Shamila?” niliuliza, nikamgeukia Shamila ambaye muda wote alikuwa kimya kabisa, akionesha bado kuwa na hofu kubwa ndani ya moyo wake.
“Eti kwani wewe ulihisi nini wakati tumekuja kukuokoa?”
“Yaani hata sielewi kilichotokea, nakumbuka nilikuwa nimewekwa chini ya ulinzi, tena mambo yakiwa yamenikalia kooni kwelikweli kwa sababu jambo la kwanza nilitakiwa kulipa bili za matibabu za wewe na Shenaiza ambazo kimsingi ni kubwa sana kisha baada ya hapo ndiyo taratibu za kisheria zingefuatia.
“Nilishaanza kuwasikia wakisema kwamba kwa jinsi tukio lenyewe lilivyokuwa limenikalia vibaya, ningeenda kufungwa, tena si kifungo cha chini ya miaka saba,” alisema Shamila, akaendelea:
“Nikiwa nimekaa pale ndani ghafla nikaanza kuhisi kama upepo hivi unavuma, mara wale askari waliokuwa wakinilinda wakapitiwa na usingizi mzito na kufumba na kufumbua, nilishangaa nikisombwa na kimbunga kikali na sikuelewa tena kilichoendelea mpaka nilipozinduka na kujikuta humu ndani. Kwani ilikuwaje?” Shamila naye alinigeuzia mimi swali.
“Labda tumuulize mama mdogo,” na mimi nililikwepa swali, wote tukamgeukia Junaitha ambaye alishusha pumzi ndefu kisha akatuambia hawezi kueleza kilichotokea kwa maneno machache tukamuelewa, tunahitaji kukaa darasani na kupata muda wa kutosha kujifunza.
“Ila kwa kifupi kilichotokea ni uthibitisho wa jinsi kila mmoja wetu hapa alivyo na nguvu kubwa ndani yake ambayo iwe anajua au hajui, ina uwezo wa kufanya mambo makubwa sana. Na tukiunganisha nguvu hiyo ndiyo tunaweza kufanya mambo makubwa yakautingisha ulimwengu wote.
“Ukishajua kucheza na nguvu hizi unao uwezo hata wa kwenda kuzimu na kurudi, yaani roho ikatengana na mwili kabisa na kila mmoja akaamini kwamba umekufa kisha baada ya muda ukazinduka tena na kuwa hai,” alisema Junaitha huku akinitazama, nikajua alikuwa akinilenga mimi jambo fulani ingawa sikuwa na uhakika.
“Hayo tutaendelea nayo baadaye lakini niwape onyo, kama kuna yeyote anayeshiriki mapenzi nje ya ndoa aache kwa sababu hiyo ni sumu kubwa sana katika udhibiti wa nguvu za ndani na najua hakuna aliyeoa au kuolewa kati yenu. Tuna kazi ya kumzindua Shenaiza kwa hiyo lazima kila mmoja ajitahidi mwili wake kuwa msafi vinginevyo hakuna kitakachofanyika,” alisema Junaitha.
Akilini mwangu nilielewa kwa nini ameyasema maneno hayo, ndani ya kichwa chake alishahisi kwamba miongoni mwa wale wasichana lazima kuna ambaye natoka naye kimapenzi na kwa sababu tayari nilishamuonjesha asali, alikuwa tayari kuchonga mzinga ila hakutaka mtu mwingine yeyote aendelee kuchangia naye.
Aliposema hivyo niliwaona wote watatu, Shamila, Raya na Firyaal wakinitazama kwa macho ya chinichini kama wanaosema ‘potelea mbali’. Alituchukua wote na kutupeleka kwenye chumba alichokuwa amelala Shenaiza akiwa hana fahamu.
“Roho yake imekwenda mbali kabisa na mwili, tunatakiwa kuivuta mpaka irudi mahali pake na hilo likifanyika tu, atazinduka. Tutakuwa na kazi kubwa kwa sababu licha ya kuwa roho yake imekwenda mbali, pia nguvu za ubongo wake zimevurugwa na madawa makali aliyokuwa anachomwa kule hospitalini, haitakuwa kazi nyepesi,” alisema Junaitha kwa msisitizo.
Wote tukawa kimya kabisa tukisubiri maelekezo yake, akatuambia kwamba itabidi wenye nguvu kati yetu ndiyo watoke kuifuata roho yake mahali ilipo na wale wengine wajazie nguvu zao kwetu.
“Narudia tena, haitakuwa kazi nyepesi na pengine tutachoka kuliko hata ilivyokuwa mwanzo,” alisema, sote tukashusha pumzi ndefu na kuendelea kumsikiliza. Akatuambia kabla ya yote, kila mmoja anatakiwa kwenda kuoga kwa maji mengi na kuhakikisha amevaa nguo safi, akatuambia kama hatukuwa na nguo safi tusijali atatupa mavazi maalum ambayo huwa anayatumia kwenye shughuli kama hizo.
“Shughuli kama hizi? Zipi?”
“Za kusaidia watu wenye matatizo kama wewe,” alijibu Junaitha huku akinitazama kwa macho ambayo yalimaanisha yupo kikazi zaidi. Kwa kututazama, usingeweza kuamini kwamba ndiyo sisi ambao muda mfupi uliopita tulikuwa tukisakata kabumbu kwenye uwanja wa fundi seremala. Tofauti na wanawake wengine, Junaitha alionesha kuwa na uwezo mkubwa wa kuzimudu vyema hisia zake.
Hakukuwa na muda wa kupoteza, harakaharaka tulienda kuoga, kwa kuwa karibu kila chumba kilikuwa na bafu la ndani, muda mfupi tu baadaye tayari wote tulikuwa tumeshaoga, ingawa ilibidi mimi nijitenge peke yangu ili kuzuia mtafaruku unaoweza kutokea.
Muda mfupi baadaye wote tulikuwa tumevalia mavazi maalum kama yale yanayotumika kwenye hoteli kubwakubwa kwa ajili ya kulalia, yote yakiwa na rangi nyeupe.
“Hamuoni mmependeza?” alisema Junaitha, wote tukacheka, tukarudi kwenye chumba alichokuwa amelala Shenaiza. Ilibidi tusaidiane kumshusha kutoka pale kitandani mpaka chini kwenye jamvi, kisha na sisi tukakaa mkao maalum wa kukunja miguu na kutengeneza duara kumzunguka Shenaiza ambaye hakuwa akielewa chochote.
“Tunafanya kama tulivyofanya wakati wa kumuokoa Shamila,” alisema Junaitha, kwa sababu wote tulikuwa tunakumbuka tulichokifanya, tulishikana mikono na kufumba macho, kila mmoja akaanza kuvuta hewa kwa utaratibu maalum na kuiachia, haikuchukua muda eneo lote likatawaliwa na utulivu wa hali ya juu.
Ile hali ilianza tena kunirudia kama mwanzo, nikaanza kuhisi kama napaa huku nikishuhudia jinsi mwili wangu usioonekana ulivyokuwa ukiachana na huu unaoonekana. Tofauti na mwanzo ambapo nilikuwa nahisi hofu kubwa ndani ya moyo wangu, safari hii nilikuwa najisikia ku-relax sana.
Kuna muda nilitamani hata maisha yangu ya kila siku niwe kwenye ulimwengu huo mwingine. Hata hivyo, hali niliyokuwa naisikia ilikuwa ya muda, ghafla nikaanza kuhisi mtikisiko mkubwa, ukasikika mlio mkali wa radi na mandhari yakabadilika hapohapo.
Kelele za vyuma vingi vilivyokuwa vikigongana, pamoja na muungurumo wa kutisha sambamba na moshi mwingi mweusi unaopalia kooni vikanizingira kila upande.
“Mbona kama nimewahi kufika kwenye haya mazingira?” niliwaza lakini cha ajabu nikasikia sauti ya kile nilichokuwa nakiwaza ikijirudia kama mwangwi mkali, nikajua kazi imeanza.
Nilipogeuka huku na kule, nilijikuta nimekaa kwenye kiti cha chuma kilichokuwa na kutu nyingi, nikageuka tena na kutazama huku na kule, nikagundua kwamba nipo kwenye lile treni ambalo siku ile nilipojeruhiwa na kupoteza fahamu kisha kuhamia kwenye ulimwengu mwingine, nililipanda.
Kwa mbali niliwaona watu kadhaa wakiwa wamevaa nguo zilizokuwa zikifanana na zile nilizovaa, lakini kila mmoja akiwa ameinamisha kichwa kuonesha kwamba yupo usingizini. Kasi ya treni ilizidi kuongezeka na kadiri tulivyokuwa tunasonga mbele, milio ya ajabu ilianza kusikika kwa mbali, ukichanganya na muungurumo wa treni lile la ajabu, na giza totyoro lililokuwepo, hali ilikuwa ya kutisha mno.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 
Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 54
ILIPOISHIA:
Kwa mbali niliwaona watu kadhaa wakiwa wamevaa nguo zilizokuwa zikifanana na zile nilizovaa, lakini kila mmoja akiwa ameinamisha kichwa kuonesha kwamba yupo usingizini. Kasi ya treni ilizidi kuongezeka na kadiri tulivyokuwa tunasonga mbele, milio ya ajabu ilianza kusikika kwa mbali, ukichanganya na muungurumo wa treni lile la ajabu, na giza totoro lililokuwepo, hali ilikuwa ya kutisha mno.
SASA ENDELEA...

“Poooh! Pooh!” honi kali ya treni ilisikika ikifuatiwa na msuguano mkali wa vyuma, nikaona watu wote waliokuwa mle ndani ya treni la ajabu wakirushwa upande wa mbele. Nilijishikilia kwa nguvu, treni likajisugua juu ya reli na kusababisha cheche nyingi ziruke, eneo lote likawa kama karakana ya kutengenezea vifaa vya chuma.
Treni liliposimama, nilishtukia nimeshashuka, hata sikumbuki nilipitia mlango gani, macho yangu yakatua kwenye kitu kilichosababisha treni hiyo ifunge breki za ghafla kiasi kile. Msichana mmoja, aliyekuwa na macho yanayong’ara kama paka awapo gizani, nywele ndefu zilizokosa matunzo na kucha kama mnyama wa porini alikuwa amekaa katikati ya reli huku akinguruma kama mnyama wa kutisha.
Sijui nilipata wapi ujasiri wa kumsogelea, kadiri nilivyokuwa nasogea mbele ndivyo msichana yule alivyozidi kutoa mlio wa kunguruma na kusababisha nipatwe na hofu kubwa mwilini. Lakini cha ajabu, eti muda huohuo nilikuwa nasikia sauti ya Junaitha ikiniambia napaswa kuishinda hofu yangu, nikazidi kumsogelea.
Kwa msaada wa taa moja kubwa iliyokuwa mbele ya lile treni, kufumba na kufumbua, nilishangaa yule niliyekuwa namuona kama msichana akibadilika na kuwa jibwa lenye meno na kucha ndefu, likaanza kubweka kwa nguvu huku likitokwa na mate mengi mdomoni.
Kiukweli nafsi yangu ilielemewa na hofu lakini eti cha ajabu sauti ya Junaitha ikawa inaendelea kusikika ndani ya moyo wangu ikiniambia sipaswi kuogopa chochote, nikapiga hatua moja mbele na sasa tukawa tumekaribiana sana na jibwa hilo ambalo lilikuwa likiendelea kubweka kwa hasira lakini lilipoona sishtuki, liligeuka na kuanza kutimua mbio huku likiendelea kubweka.
Nikasikia sauti ikiniambia nianze kulifukuza jibwa lile, bila hata kuuliza nikaanza kukimbia kuelekea kule lilikokimbilia, huku nyuma nikasikia lile treni likianza kunguruma tena kwa kasi, moshi mwingi ukatanda eneo lote kisha likaanza kuondoka.
Nilifunga breki za ghafla na kugeuka nyuma, nilishindwa kuelewa kama lile treni linaondoka mimi nitaondokaje kwenye mazingira yale ambayo kwanza sikuwa najua ni wapi halafu yalikuwa yakitisha sana?
“Mkimbize Jamal, utakosa vyote,” ilisikika sauti ya Junaitha, nikaachana na treni hilo na kuanza kutimua mbio, lile jibwa lilikuwa likikimbia na kufika mbali kidogo, linasimama na kugeuka kunitazama, likawa linaendelea kubweka kwa nguvu na likiniona nakuja, linaanza tena kukimbia.
Japokuwa kulikuwa na giza nene, niliweza kuyatambua mazingira hayo kuwa ilikuwa ni katikati ya msitu mkubwa wenye miti iliyofungana kwani hata nilipojaribu kutazama juu, sikuona mwezi wala nyota, kila sehemu kulikuwa na giza. Kilichosaidia niweze kuelewa jibwa lile lilikokimbilia, ilikuwa ni mwanga wa macho ya lile jibwa, ambayo sasa yalikuwa yaking’aa sana.
Niliendelea kukimbia, mara nikajikuta nimetokezea sehemu iliyokuwa na majimaji, nikawa kila nikipiga hatua nakanyaga kwenye matope, sikupunguza mwendo, niliendelea kutimua mbio, nikawa najikwaa kwenye visiki, wakati mwingine nakanyaga miiba lakini sikuchoka, mara tukatokezea kwenye sehemu ambayo hakukuwa na giza kama kule tulikotoka.
Giza lake lilikuwa ni kama katikati ya usiku wa manane na mapambazuko, kwamba kunakuwa na giza lakini siyo totoro na kwa mbali kuna mwanga unaonekana. Hali hiyo ilifanya niweze kuona vizuri mazingira yote, nikawa pia na uwezo wa kuliona vizuri jibwa lile ambalo liliendelea kutimua mbio huku likibweka kwa hasira.
“Huyo siyo mbwa, ni binadamu, mganga wa baba yake Shenaiza, anajua siri nyingi sana kumhusu na ndiye atakayetusaidia kuiona nafsi ya Shenaiza ilikofungiwa, jitahidi uishike ile kamba yake ya shingoni, usijali hata kama litakurarua,” sauti ya Junaitha ilisikika tena ingawa sikuwa na uwezo wa kumuona. Kauli hiyo ilinitisha sana, nikaanza kuamini kwamba kumbe zile stori nilizokuwa nazisikia tangu kitambo, kwamba kuna binadamu wanaoweza kubadilika na kuwa mbwa, zilikuwa za kweli.
Nilipiga moyo konde, nikaongeza mwendo na hatimaye nikawa nimelikaribia kabisa lile jibwa ambalo sasa lilipoona naelekea kulizidi mbio, liligeuka kwa hasira na kutaka kunirukia, likiwa limetoa makucha yake. Nilifanya kama nilivyoagizwa na ile sauti, mkono mmoja nikautumia kuibana miguu yake ya mbele iliyokuwa na nguvu kubwa, likadondoka chini kama mzigo.
Kwa bahati mbaya sikuweza kuidhibiti miguu ya nyuma, likaitumia kunirarua mapajani mwangu ambapo kama isingekuwa uzito wa ile nguo niliyokuwa nimevaa, huenda lingenijeruhi zaidi ya vile.
Japokuwa nilisikia maumivu makali, sikujali, nikalishika shingoni ambapo lilikuwa limefungwa kwa kamba iliyokuwa na mafundofundo kadhaa.
“Unaniuaaaa, nisamehe unaniuaaa,” nilishangaa mno kuona jibwa lile likibadilika na kuwa mtu ambaye alianza kupiga kelele akiniomba msamaha. Bado nilijihisi kama nipo ndotoni, nikawa nimekodoa macho nikiwa ni kama siamini.
Nikiwa bado nimepigwa na butwaa, nilishangaa Junaitha naye akidondoka kutoka kusikojulikana kama mzigo, harakaharaka akainuka na kujikung’uta, akasogea pale nilipokuwa nimelikaba lile jibwa ambalo sasa lilibadilika na kuwa mwanamke, tena mzee tofauti na msichana ambaye nilimuona pale treni liliposimama ghafla.
“Nilikwambia nitakupata tu ukabisha, sasa yako wapi?” nilimsikia Junaitha akisema wakati akinisaidia kumfunga mwanamke yule ambaye bado alikuwa akiendelea kupiga kelele huku akifurukuta. Nilishangaa kugundua kwamba kumbe Junaitha alikuwa akifahamiana na yule mtu wa maajabu.
Nikawa najiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu, Junaitha alipomaliza kumfunga mikono kwa kutumia kamba za miti, alihamia miguuni. Akamfunga na kumgeuza, akamburuza na kumkalisha akiwa ameegamia kisiki cha mti.
“Unaona ulivyomuumiza? Haya nataka umtibu sasa hivi, vinginevyo nitakufunza adabu,” alisema Junaitha kwa hasira huku akimshika nywele na kumtingisha, kwa msaada wa mwanga hafifu nikawa namshangaa yule mwanamke jinsi alivyoumbwa usoni.
Alikuwa na masikio makubwa, pua nene ya duara na meno yaliyochongoka pembeni. Ama kwa hakika alikuwa akitisha. Baada ya Junaitha kumwambia vile, huku akitetemeka alitoa ishara kwamba nifunue lile eneo alilokuwa amenijeruhi, akatoa ulimi wake na kunipa ishara kwamba nisogeze majeraha yangu anilambe, jambo ambalo nilisita.
“Sogea tu hawezi kukufanya chochote, si unaona nimeshamvua kamba yake ya shingoni,” alisema Junaitha huku akinionesha kamba iliyokuwa na mafundo kadhaa aliyokuwa ameishika mkononi. Nikasogeza mapaja yangu ambapo alitoa ulimi wake mrefu na kuanza kunilamba damu zilizokuwa zinachuruzika.
Ulimi wake ulikuwa mgumu na unaokwangua kama wa mnyama mkali, nikashangaa maumivu niliyokuwa nikiyasikia yakiyeyuka ghafla, Junaitha akanihakikishia kwamba nitapona baada ya muda mfupi, nikawa bado nimepigwa na butwaa.
“Ukitaka kuendelea kuishi, kazi ni moja tu, tunataka utuoneshe Shenaiza alipo na pia utuambie mbinu zote za kishirikina ulizomfanyia baba yake alipokuja kwako kuomba kinga ya kufanikisha mambo yake ya kishetani,” alisema Junaitha, mwanamke huyo akaanza upya kulia huku akitingisha kichwa chake, hali iliyozidi kunifanya nikose majibu.
Aliendelea kulia na mara akaanza tena kutoa muungurumo kama mnyama mkali wa porini, akawa anafurukuta kwa nguvu.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 
Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 55
ILIPOISHIA:
“Ukitaka kuendelea kuishi, kazi ni moja tu, tunataka utuoneshe Shenaiza alipo na pia utuambie mbinu zote za kishirikina ulizomfanyia baba yake alipokuja kwako kuomba kinga ya kufanikisha mambo yake ya kishetani,” alisema Junaitha, mwanamke huyo akaanza upya kulia huku akitingisha kichwa chake, hali iliyozidi kunifanya nikose majibu. Aliendelea kulia na mara akaanza tena kutoa muungurumo kama mnyama mkali wa porini, akawa anafurukuta kwa nguvu.
SASA ENDELEA...

“Usitake kututisha hapa na ukiendelea na upuuzi wako nitakuua kwa mikono yangu mwenyewe, unajua ni kwa kiasi gani nina hasira na wewe?” alisema Junaitha kwa sauti nzito ya kunguruma, ambayo sikuwahi kumsikia hata siku moja, yule mwanamke mzee akanywea na kurudi kwenye hali yake ya kawaida lakini bado alikuwa akilia huku akitingisha kichwa, akionesha hayupo tayari kuzungumza kitu chochote.
“Wala sikulazimishi, uchaguzi ni wako, ukitaka kuendelea kuishi ni lazima uzungumze na ukitaka kufa endelea kukataa.”
“Hata nikizungumza nitakufa tu, hawezi kuniacha, ataniua.”
“Nani, unamzungumzia nani?”
Badala ya kujibu, yule mwanamke alionesha kwa ishara, Junaitha na mimi tukageuka kutazama kule alikokuwa anaonesha.
“Mungu wangu,” nilijikuta nimetamka wa sauti kubwa, Junaitha akaniwahi na kuniziba mdomo.
“Huku huwa hatumtaji ovyo Mungu, si unajua kuna amri katika vitaabu vitakatifu ambayo inasema usilitaje bure jina la Bwana Mungu wako?” alisema Junaitha kwa sauti ya kunong’ona, nikatingisha kichwa kama ishara ya kukubaliana naye lakini bado moyoni nilikuwa nimepatwa na hofu kubwa mno.
Joka kubwa lililokuwa limesimamia mkia na kujiinua, likiwa na macho mekundu yanayowaka huku ulimi wake mrefu wenye ncha mbili ukichezacheza, lilikuwa likitutazama, mita chache kutoka pale tulipokuwa tumembananisha yule mwanamke mzee.
“Huyu ni nani?”
“Mkuu.”
“Anahusikaje katika hili?”
“Maagano yote wanayoyafanya watu wanaoishi Kusini mwa Jangwa la Sahara na kuzimu hupitia kwake na yeye ndiye anayeidhinisha.”
“Anataka nini?”
“Anataka mniachie niende zangu,” alisema yule mwanamke huku akitetemeka. Muda wote huo, macho yangu yalikuwa yameganda kwenye lile joka, kuna wakati nilihisi kama haja ndogo inanitoka kwa hofu. Likawa linageuza kichwa huku na kule, likiendelea kuchezesha ulimi huku likitutazama.
Mara likaanza kuteleza taratibu likitusogelea, Junaitha akanipa ishara kwamba nisogee tusaidiane kumshika yule mwanamke, nikafanya hivyo. Ndani ya dakika sifuri tayari tulikuwa tumemshika yule mwanamke, mimi upande wa kulia na Junaitha upande wa kushoto.
“Inabidi tuondoke, fuatisha ninachokifanya,” alisema Junaitha, akapiga mguu wa kushoto chini, na mimi nikafanya hivyo, akapiga tena, na mimi nikapiga mpaka mara tatu kisha akanionesha ishara kwamba tunatakiwa kuanza kuzunguka kutengeneza duara, tukifuata uelekeo wa kinyume na mshale wa saa au kwa Kizungu wanaita Anti-Clockwise, yaani kutoka kulia kwenda kushoto.
Tulipozunguka mara moja tu, ghafla upepo mkali ulianza kuvuma, Junaitha akanionesha ishara kwamba tuendelee kuzunguka kwa kasi zaidi, kufumba na kufumbua kikaibuka kimbunga kikali na kutuzoa, kwa mbali nikawa nasikia sauti ya lile joka likinguruma kwa hasira, sauti zikafifia masikioni mwangu na ikafika mahali nikawa sijitambui tena.
Nilipokuja kuzinduka, nilijikuta nikiwa nimelala kwenye zulia, ndani ya kile chumba tulichokuwa tumekaa mimi, Junaitha, Raya, Shamila na Firyaal. Kama ilivyokuwa mara ya kwanza tulipotoka kumuokoa Shamila, mwili wangu ulikuwa umechoka mno, karibu kila kiungo kikiniuma.
Nilipofumbua macho, nilimuona Junaitha akiwa anasumbuana na yule mwanamke mzee, ilivyoonesha ni kama alikuwa akitaka kujifungua kamba tulizomfunga, akamzabua kibao kwa nguvu na kumtaka atulie.
Nilijikakamua na kusimama, japo kwa taabu, miguu yangu ikiwa inatetemeka kwani sikuwa na nguvu kabisa.
“Hebu njoo tukamfungie huyu mshenzi naona anataka kushindana na mimi,” Junaitha alisema, kijasho chembamba kikimtoka. Kwa kuwa mle ndani kulikuwa na mwanga tofauti na kule kwenye ulimwengu mwingine tulikotoka, niliweza kumtazama vizuri yule mwanamke. Ama kwa hakika alikuwa anatisha.
Ngozi yake ilikuwa imeweka utando mweusi juu yake, kuonesha kwamba ulipita muda mrefu sana bila kuoga au kugusa maji, kucha zake nazo zilikuwa ndefu, zilizojaa uchafu, huku kichwani nako akiwa na nywele ndefu, chafu, zilizonyonyoka na mdomoni alikuwa na meno machafu, yaliyochongoka kama ya mnyama wa porini.
“Mbona unashangaa? Shika tumpeleke ndani,” alisema Junaitha, akawa ni kama amenizindua kutoka kwenye lindi la mawazo ya kutisha. Nilimshika yule mwanamke japo kwa woga, nikamuona akinitazama na kunikazia macho.
“Sura yako siyo ngeni, tumewahi kukutana mahali,” alisema yule mwanamke huku akiendelea kunitazama kwa kunikazia macho. Alipozungumza, harufu mbaya ilimtoka mdomoni na kusababisha hali ya hewa ichafuke, sikumjibu kitu, akawa anaendelea kunitazama.
Sikuwahi kumuona kabla wala sikuwahi kukutana na kiumbe cha mfano wake, nilishangaa ananiambia sura yangu siyo ngeni, nikahisi anataka kunichezea mchezo wa kunirubuni.
“Donda lako la kifuani lilishapona?” aliniuliza swali lingine lililonishtua mno. Ni kweli nilikuwa na kidonda kifuani ambacho kilinitesa kwa kipindi kirefu lakini alijuaje? Nikajikuta nikiwa kwenye mtihani mgumu uliokosa majibu. Nilimtazama Junaitha lakini alifanya kama vile kunipotezea fulani hivi, akijifanya hajasikia kilichozungumzwa na yule mwanamke.
“Hukupaswa kuwepo hapa leo, ulimwengu huu siyo sehemu yako, unatakiwa kuwa sehemu nyingine sasa hivi,” alizidi kusema yule mwanamke wakati tukimkokota kuelekea kwenye chumba cha ndani kabisa ambacho Junaitha hakuwa akiruhusu mtu yeyote kuingia.
“Naongea na wewe, unajifanya hunisikii si ndiyo?” alifoka yule mwanamke baada ya kuona nimemchunia, akawa anatishia kama anataka kuning’ata na meno yake kama mnyama wa porini, Junaitha akamzibua kibao kingine cha uso, akatoa ukelele kuonesha kilikuwa kimemkolea.
“Kanisubiri chumbani kwangu,” alisema Junaitha, akawa amenizuia kijanja kuingia kwenye kile chumba chake cha siri ambacho hakuna aliyekuwa anajua ndani yake kuna nini kwa sababu hakuna aliyewahi kuingia. Hata Shamila mwenyewe, alinidokeza kwamba hakuwahi kuingia hata mara moja.
Alimuingiza yule mwanamke kisha akafunga kwa ndani, nikamsikia yule mwanamke mzee akitoa sauti ya kuugulia, sikujua nini kilichokuwa nikaendelea humo ndani. Nilijivuta na kuelekea chumbani kwa Junaitha kama alivyioniambia.
Kila kitu kilikuwa kikitokea kwa kasi kubwa mno kiasi cha kunifanya nijihisi kama nipo kwenye ndoto za kutisha. Nilirudi mpaka kwenye kile chumba nilichowaacha akina Shamila, bado walikuwa wamelala fofofo kama mizigo, nikarudisha mlango taratibu na kuelekea chumbani kwa Junaitha lakini kabla sijafika, nikiwa napita kwenye chumba alichokuwa amelala Shenaiza, nilimsikia akikohoa.
Harakaharaka nikafungua mlango nikiwa ni kama siamini nilichokisikia, nikamkuta Shenaiza akihangaika kujigeuza, jambo ambalo hakuwa amelifanya kwa kipndi kirefu tangu akiwa kule hospitalini.
“Shenaiza! Shenaiza,” nilisema huku nikipiga magoti pembeni ya kitanda chake. Bado hakuwa amefumbua macho yake.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom