
JINA jema ni SILAHA
“1Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi; Na neema kuliko fedha na dhahabu” (Mithali 22:1).
“5Basi Daudi akatoka kwenda kila mahali alikotumwa na Sauli, akatenda kwa akili; Sauli akamweka juu ya watu wa vita; jambo hili likawa jema machoni pa watu wote, na machoni pa watumishi wa Sauli pia [……]
12 Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu BWANA alikuwa pamoja naye, ila amemwacha Sauli [……]
14 Naye Daudi akatenda kwa busara katika njia zake zote naye BWANA alikuwa pamoja naye. 15Sauli alipoona ya kwamba alitenda kwa busara sana, yeye alimwogopa. 16Lakini Israeli wote na Yuda wakampenda Daudi; kwa kuwa alitoka na kuingia mbele yao [……..]
29 Naye Sauli akazidi kumwogopa Daudi; Sauli akawa adui yake Daudi sikuzote” (1 Samweli 18: 5, 12, 14-15 & 29).
Ni vigumu kuelewa jinsi ambavyo JINA linaweza kuwa na THAMANI kubwa kuliko mali nyingi; Na, NEEMA kuliko dhahabu na fedha, hadi uone kwa vitendo JINA jema na NEEMA vikifanya kazi katika maisha ya mtu.
Hebu fikiri Daudi ni kijana mdogo tu, umri sawa na mtoto mdogo wa mfalme Sauli, tena ni maskini [….”Daudi akasema, Je! Ninyi mwaona kuwa ni shani mimi kuwa mkwewe mfalme, nami ni maskini, tena sina cheo?” - 1 Samweli 18: 23b]
Kwa sifa za nje, Daudi bado alikuwa hajakomaa kiasi cha kuruhusiwa kwenda vitani, ila baada ya kumuua Goliath, alijipatia sifa hiyo muhimu.
Leo mfalme Sauli, mtu wa vita tangu siku nyingi, baba mtu mzima, tajiri wa kila kitu, mwenye vikosi vya jeshi na silaha, huku yeye mwenyewe akiwa jemadari na mpiganaji mzoefu, anamwogopa Daudi, mchunga mbuzi tu, asiye na mali (maskini), asiye na cheo wala silaha, isipokuwa kombeo, fimbo ya kuchungia mbuzi na mfuko wa mchungaji!
Je! Alichokuwa anaogopa mfalme Sauli ni kitu gani? Jibu liko hapa, ni “JINA JEMA” la Daudi katika Israeli yote na Yuda yote! Tena, aliona NEEMA juu ya Daudi; yaani, alijua kwamba Mungu yuko naye. Hivi vitu viwili vikamtisha mfalme mkuu, hata akakosa amani mbele ya kijana mdogo tu! Mfalme Sauli akamwogoa Daudi vibaya.
“8 Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? 9 Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile” (1 Samweli 18:8, 9).
Hebu nisikilize, najua unahangaika KUSOMA, kufungua BIASHARA, au kijitahidi kwa namna fulani kupata PESA au CHEO, ukidhani kwamba HESHIMA yako itaongezeka na utapata unachokitaka maishani kwa sababu UMEFANIKIWA katika vitu vya mwilini! Sawa, utapata vyote, ila akina Daudi wataendelea kukutisha kila siku na kukunyima usingizi.
Ana heri mtu yule ambaye Bwana ni NGUVU zake. Soma, fanya kazi kwa bidii, pata mali na cheo, ila kama BWANA sio Mungu wako, bado utakimbia pasipo kufuatwa na mtu. Na, kama Bwana ni Mungu wako kweli-kweli, wala hutajua, kumbe, Wanakuogopa!
“Tazama, kumcha Bwana ndiyo hekima, Na kujitenga na uovu ndio ufahamu” (Ayubu 28:28).
JIONI NJEMA MBARIKIWE