Sehemu ya sita...
"Hakika Tina! Hakikaaa ameweza German. Hakika ameweza kulipa uhai jina lake baada ya kifo chake. Hakikaaa ameweza aaah! Hakika jina lake litaishi milele...Eeee Mungu mueke pema sitamani kulia mimiii" Nililia na kukaa chini kabisa baada ya nguvu za kuchutama kuingia ganzi miguuni. Daaah! Sitakusahau German Machine. Ulichotwambia darasa la sita kuhusu jina ndivyo imekuwa kwa jina lako. GERMAN MACHINE Ama kweli maneno huumba......
Twende sasa...
.......Tukiwa bado tunahuzunika na kumlilia German Machine ambaye muda huo mwili wake ulikuwa ndani ya jeneza lililokuwa uwanjani tayari kwa kuagwa na mamia ya watanzania. Ndipo yule askofu kutoka Ujerumani alipomaliza ibada maalum na ulikuwa wakati walipopanda wasanii maarufu nchini walioungana kwa kuimba wimbo maalum wa maombelezo ulioitwa 'German Machine'.
Uwanja mzima ulizizima kwa sauti tamu za wasanii walioimba kwa ufanisi wimbo wa kumsifu German. Maneno yao yalinijengea hisia sana na kujikuta nasimama sambamba na Tina. Tulijikuta nasi tunayafatisha maneno ya wasanii huku tukinyoosha mikono hewani.
|/''Tutakukumbuuuukaaa hakikaaa! we ni German Machine...//
Tutakukumbuukaaa hakikaaa! we ni German Machine..//
Dunia inakuliliiiaaaaaaa....// German Machineeeee''/|
Wakati nami nikiimba kwa hisia nikiwa nimefumba macho hisia zangu zilisafiri tena kurudi miaka ile ya nyuma. Siku niliyorudi kuonana na German Machine baada ya kunipa kibao kilichonionesha maajabu ya jua asubuhi.
* * * *
||MIAKA 12 NYUMA||
Nilichapa ngwala huku shauku ikiwa imenijaa nilipozidi kukaribia kwa kina German Machine. Nilifika na kumkuta akiwa nje amesimama mguu mmoja juu ya kichuguu kilichokuwa jirani na nyumba yao.
"German! vipi uko poa?" Nilimuuliza na kumfata pale kwenye kichuguu.
"Karibu Twaha! niko salama tu." Alinijibu huku akiushusha ule mguu na kusimama sawa. Nilimtazama mwili ulimjaa jasho. Nilishangaa na kumuuliza.
"Vipi mbona umesimama hivyo juani?"
"Twaha, nishati ya jua la asubuhi ni ya kipekee katika mwili wa binaadamu endapo utakuwa unaitumia kila siku. Nakushauri nawe uwe unafanya hivi asubuhi jua lichomozapo usimame kwa mguu mmoja usishushe na utulize hisia zako. Lisikie jua linavyokupa joto hadi mwili wako unapolowa kama hivi ndipo utoke."
"Kwanini sasa unasimama kwa mguu mmoja?"
"Twaha, Ukisimama kwa mguu mmoja utazilazimisha fahamu zako kumakinika nawe kuliko kutumia miguu miwili utazitia uvivu. Karibu tukae kivulini pale kwenye mti." Alinambia natukaelekea pamoja kwenye mwembe. Bila kupoteza muda tulipokaa nilianza kumsimulia nilichokiona kupitia kile kibao alichonipa.
"Vizuri Twaha. Sasa ulichokiona ndicho alichokiona Johannes Kepler mwanzoni mwa karne ya 16 na kumfanya atafiti zaidi na kuujua ukweli kuhusu jua na sayari nyengine. Shuleni tunafundishwa kuwa dunia yetu inazunguka katika muhimili wake. Lakini vipi utaiona dunia inazunguka ihali kila siku tupo palepale? Jawabu ni hivi, ulichokiona kupitia hiki kibao ni jinsi muhimili wa dunia na sayari nyengine zinavyolizunguka jua." Alinambia German huku nikimsikiliza kwa umakini. Alinitazama na kuendelea.
"Twaha, nadhani uliiona michoro ya Johannes Kepler. Ile michoro ndani yake kuna pembe tatu 6 zinazounda pembe 18. Endapo ukaichora vyema hata chini na kuzungusha duara katikati hakika utaziona njia ambazo kimahesabu ndizo zinazopitiwa na mihimili ya kila sayari inavyozunguka jua. Ila haya ni mahesabu makubwa sana yanayohitaji utulivu kuyafanya."
"German! naomba unambie kweli. Habari za Johannes Kepler wapi unazitoa?" Nilimuuliza kwa shauku.
"Habari zake hata nikikwambia Twaha huwezi kuniamini kwasasa imani yako bado ndogo. Ila siku moja utaniamini vyema ingawa kwa sasa unaweza kuniitika lakini ukaondoka na shaka ndani yake."
"Hapana si hivyo German, nami nataka nijifunze kama wewe. Naomba unambie tafadhali." Nilibembeleza.
Alinitazama kwa muda akafikiri jambo kisha akanambia.
"Nitakwambia Twaha kuhusu Johannes Kepler nimeyajuaje mambo yake, lakini si kwa muda huu. Mungu akipenda siku moja nitakwambia kila kitu pasipo kuniuliza." Jibu lake lilinitia unyonge moyoni ingawa nilinyamaza tu. Ukomo wa fikra yangu ulishindwa kung'amua wapi anazitoa habari za mtu huyo aliyeishi karne nyingi nyuma. Lakini pia nilijiuliza kwanini anamfatilia huyo mtu? Ilibidi nimuulize na hilo.
"Twaha, maisha ya duniani ni safari. Safari tunayosafiri ndani ya ndoto na hisia zetu. Kila moyo wa kiumbe hai unatamani kitu fulani katika maisha. Lakini mfumo batili wa maisha ya wanadamu walioutengeneza wao wenyewe unasababisha wengine wakate tamaa na kuishi nje ya ndoto zao. Lakini ukiufata mfumo asilia alioutengeneza Mungu mwenyewe utaishi ndani ya misingi ya kutimiza ndoto. Kwa ufupi namaanisha kila mwanadamu anasafiri na ndoto ya maisha yake ya dunia kabla ya kifo. Lakini ndoto huwa hai siku zote na ndoto moja inaweza kusafiri ndani ya maisha ya binaadamu wengi kwa nyakati tofauti mpaka upatikane ukomo wake. Sasa ndoto aliyokuwa nayo Johannes Kepler ndiyo ndoto ambayo ninayo mimi. Lengo langu ni kukifanya kile ambacho hakuna aliyewahi kufanya kwenye uso wa dunia kama alivyofanya Johannes ambaye dunia na ujerumani walimuona ni machine ya kufikiri pale alipozibainisha siri za jua na mizunguko ya sayari. Lakini Johannes bado kuna hatua alitamani kusogea zaidi katika ndoto yake lakini muda wa kuishi ulifika ukomo. Mpaka leo duniani hakuna aliyethubutu kubaini wala kuendeleza pale alipoishia Johannes wakiamini amemaliza na vyengine alivyoshindwa haviwezekaniki. Lakini si kweli, nataka niwathibitishie dunia kama mimi nasafiri ndani ya ndoto ya mjerumani wa kale. Ndio maana nimejita German Machine." Aliongea German nami nikabaki kimya maskiliza. Siku hiyo ndiyo alinambia mambo mengi kuhusu ndoto yake ingawa hakunambia kipi hiko anachotaka akidhihirishe kwa dunia ambacho Johannes alikishindwa? Hili lilibaki swali ambalo sikulijua miaka yote hadi siku za mwisho wa uhai wake German Machine.
Baada ya maongezi marefu nilikumbuka shangazi alinisihi nisichelewe. Ndipo nilipoamua kumuaga German ambaye wakati huo alikuwa anamenya mashelisheli kwaajili ya chakula.
"Twaha sasa leo chukua na hiki kibao cha pili. Ila hakikisha unakifunga na mfuko mweusi wa naironi uuwambe kama ngoma. Kisha unatakiwa uviweke kwa kuvipishanisha usawa ule wa dirisha. Hakikisha viwe vimetengeneza pembe 6 mpishano. Nenda kajionee vizuri muhimili wa dunia yetu unapolizunguka jua." Alinikabidhi kibao nami nami nikakipokea. Nilijikuta nami naingia kwenye utafiti wa German ingawa sikuwa najua muelekeo wake. Asubuhi yake tena nilifanya kama alivyonambia. Daah! hakika nilishangaa mno jinsi nilivyokuwa naliona jua kwa picha nzuri sana. Pembeni yake niliweza kuona miale iliyochora njia njia. Kwa mara nyengine tena baada ya kumsaidia kazi Shangazi nilikusanya vile vibao na kwenda kwa kina German. Lakini nikiwa nakaribia nyumbani kwao nilishangaa kuona watu wengi. Nilikazana zaidi wasiwasi ukanivaa baada ya kusikia vilio kwa mbali.
"Shikamooni wazee wangu. Samahani eti nini kimetokea?" Nilisalimu na kuwauliza wazee wawili waliokuwa wanatokea usawa ule kwenye nyumba ya kina German ambapo kulionekana watu wengi wamesimama wengine wameshika tama wakionesha nyuso za huzuni.
"Marhaba kijana. Ni msiba umetokea mwanetu. Kijana mwenzako sasa ameukamilisha uyatima kwa neema za Mungu." Alijibu mzee mmoja na kunichanganya zaidi kichwa. Nilikazana pasipo kusema kitu na nilipofika jirani zaidi niliweza kumuona German akiwa amekaa chini amezungukwa na wazee watatu wakimfariji.
Moyo ulinipasuka kwa taharuki pindi niliposogea na kukutanisha macho na German. Kana kwamba alijua nilichotaka kuuliza pale aliposema.
"Baba yangu Twaha. Baba ameniacha peke yangu." Aliongea kwa huzuni kilio kikachukua nafasi. Sikutia neno zaidi ya kujumuika nae na kumfariji. Nilishangaa sana kukuta msiba hali ya kuwa jana niliondoka nikimuacha babaye yu mzima kabisa!. Nilitamani kuuliza lakini niliona si busara kwa muda ule. Ukweli ukabaki kuwa baba yake German Machine amefariki dunia.
"Jikaze mjukuu wangu ndio ukubwa huo. Kazi ya Mungu haina makosa." Sauti ya mzee mmoja ilisikika kumwambia German baada ya kutulia kilioni. Hata mimi nilijikuta machozi yakinitoka picha ilivyonijia juzi yake nilizungumza na baba German. Leo tena hayupo? ama kweli kifo kinakuja bila hodi wala taarifa.
Siku hiyo ndiyo nilibaini kuwa German Machine hakuwa na ndugu kabisa pale kijijini. Wengi waliohusika kwenye msiba wa baba yake walikuwa majirani. Nilishangaa kwa kuwa si kawaida. Majirani walipofanikisha zoezi la mazishi ya baba German walitawanyika mmoja baada ya mwengine huku wakimuaga kwa huzuni na kumfariji kwa maneno. Mwishowe tulibaki wawili tu pale nyumbani kwa kina German wakati ambao kiza kilianza kuingia.
"Twaha, nenda nyumbani. Usihuzunike sana kuhusu mimi. Nitaishi tu kwa kuwa uhai wangu na wa baba vilikuwa vitu viwili tofauti. Hakuna kilichobadilika zaidi ya uwepo wake baba yangu. Nenda usimtie mashaka shangazi yako." Aliongea kwa huzuni sana. Moyo uliniuma nikitamani kuwa nae. Umri wake ulikuwa mdogo kama mimi. Nilijiuliza kwanini hakujitokeza jirani hata mmoja wa kuwa naye? Lakini mwishowe nakumbuka German alitabasamu na kuingia ndani akinisihi niondoke nimuache. Hakika siku ile nilibaki nimeganda nikiwa mwingi wa maumivu kana kwamba mimi ndiye nilifiwa. Daaaah! Masikini German...leo na yeye ameelekea kule alipotangulia baba yake miaka 12 nyuma.
.......