Sehemu ya nne
...... . Ama kwa hakika urafiki tu wa German Machine ulinipa faida kubwa kuliko hata urafiki niliouweka kwa shule. Nilichokivuna kwa German Machine kilikuwa kikubwa kuliko nilichokivuna shule. Hakika ukikaa nae unaweza kufaulu mengi kwenye maisha kuliko aliyesoma. Lakini leo hii ndio hayupo! kwanini German umeenda mapemaa!
||*******||
Kumbukizi zilikatika kilio kikanishika. Sikuweza kujizuia kabisa nikajikuta nanyong'onyea miguu na kushuka chini taratibu. Watu wa huduma ya kwanza waliniwahi.
Ingawa miguu ilinisaliti nguvu ya kuubeba mwili lakini akili ilibaki na utimamu wake. Niliekwa sehemu ya wazi na watu wa huduma ya kwanza ambapo pia kulikuwa na watu wengine wakiwahudumia. Kweli German alipendwa na wengi. Kuahirishwa sherehe za sikukuu ya uhuru ilikuwa si suala dogo kwa Taifa. Hakika alikuwa lulu ya kipekee ambayo hutokea kwa nadra sana kwenye uso wa dunia.
Spika zilizofungwa uwanjani zilisafirisha sauti za kila muongeaji rasmi kwenye shughuli za msiba wa German Machine.
"Wapendwa katika bwana. Neno la Mungu linatukumbusha kuwa kifo si mwisho wa binaadamu bali ni hatua tu ya kuvuka kutoka kwenye ulimwengu wa kimwili na kurudi ulimwengu wa kiroho kwa baba yetu aliye mbinguni. Sisi sote ni wa kwake na kwake tutarejea. Hatupaswi kuhuzunika na kutia kufuru katika kazi ya Mungu ambayo milele haina makosa. Sisi tulimpenda lakini Mungu amempenda zaidi. Kitu cha msingi ni kumuomba bwana ampe raha za milele na itapofika zamu yetu atupokee kwenye falme ya baba. Tunajua kimwili hayuko nasi lakini kiroho mpendwa wetu bado tunaye. Sasa napenda kumkaribisha askofu ANTON SCHWARZ kutoka Ujerumani kwa sala maalum kabla hatujampisha msemaji wa familia kutusomea historia ya mpendwa wetu aliyelala kwenye usingizi wa milele. Asante."
Sauti hii ilinipa nguvu ya kusimama kwa mara nyengine baada ya kupatiwa huduma ya kwanza. Msemaji ambaye alikuwa mchungaji maarufu nchini nilimuona akimkaribisha askofu aliyesafiri kutoka Ujerumani kwaajili ya kuja kumzika German Machine. Kijana mdogo aliyezimika kabla hata kufika robo ya karne toka azaliwe laikini ameweza kulitikisa taifa na dunia kwa ujumla. Uwepo wa askofu yule sambamba na wageni wengine kutoka ulaya kwaajili yake, hakika ulizidi kunidhihirishia kuwa German Machine alichokifanya kitabaki kuwa kwenye kumbukumbu ya vizazi. Alisimama askofu Anton akiwa na mkalimani wake alianza kuongoza sala maalum ambapo uwanja mzima ulizizima utulivu. Kumbukizi zangu zilinirudisha tena mpaka siku ile nilipokuwa kwenye chumba cha German Machine nikishangaa michoro yake huku akinipa elimu ya mambo mawili, Hofu na Imani.
* * * *
||MIAKA 12 NYUMA||
"German hakika mambo unayonambia ni ya kushangaza sana. Wapi unajifunza hivi vitu? Mbona elimu hii hatukufundishwa, we unaitoa wapi?" Nilimuuliza huku nikimtazama kwa mshangao.
"Twaha, kujifunza ni kuamua. Elimu haiko darasani wala shule hazipo kwa ajili ya kuwapa watu elimu ingawa watu wengi wanaamini shule ndipo mahala inapotolewa elimu." Alichonambia safari hii kilinifanya nicheke na kumpinga.
"Hapana German. Hapo umeelewa vibaya na hiko usemacho ni uongo. Shule ndipo panapotolewa elimu na hakuna mtu mwenye elimu ambaye hakusoma." Nilimpinga kutoka moyoni. Lakini alinitazama na kusikitika kisha akaanza kuyachimba maneno yake yaliyonionesha kina cha maana yake ambayo ilinishinda ubishi.
"Twaha usiyatazame maneno kama yalivyo. Kumbuka nilipokwambia juu ya mambo mawili, Imani na Hofu. Bado hujajua kuyatumia ndio maana umewahi kupinga. Sasa nakupa hizi siri ambazo zimefichwa vitabuni hawakuandika tofauti ya SHULE na ELIMU. Na havikufichwa kwa bahati mbaya bali vimefichwa kwa makusudi na watu maalum wa kale waliovumbua shule. Wamefanya hivyo ili watu maalum wazidi kuwa wachache na ndio maana kina Johannes Kepler wamegundua sayari na mambo mengi ya anga katika karne ambazo hakukuwa hata na ndege za kwenda angani wala shule iliyofundisha mambo hayo. Unaweza kujiuliza Johannes Kepler alijuaje mambo ya umbali na jinsi sayari zinavyozunguka ikiwa elimu hiyo haikuwepo shuleni karne hizo? Je wapi aliitoa elimu hiyo? Na vipi kuhusu waliobuni hesabu ambazo tunafundishwa leo ikiwa hapo kabla hazikuwepo? Wapi waliitoa elimu ya ubunifu huo? Je, ushajiuliza mtu wa kwanza kusoma na kuandika alifundishwa na nani? Jiulize kwanza waliipata wapi elimu watu hao wa kale hata wakaja kubuni uwepo wa shule? Sasa nataka nikuthibitishie kuwa elimu haitolewi shule ingawa shule ndiyo sehemu inayoweza kuonesha wapi elimu ilipo ili ukaitafute. Lakini kama utaenda shule kuitafuta elimu hakika utaikosa kwa kuwa haiko huko." Aliongea kwa hisia German Machine na maneno yake hakika yalizidi kunishangaza.
"Sasa kama ni hivyo shule ni nini na kwanini tunaenda?" Nilimuuliza.
"Kaa kitandani nikuoneshe kitu." Alinambia nami nikajisogeza mpaka kwenye kitanda kidogo cha kamba kilichogubikwa na mkeka chakavu. Nilitulia nikimuangalia ambapo aliinama uvunguni mwa kitanda kuna kitu alikivuta.
"Twaha, naomba uniahidi hutoanika haya mambo kwanza." Alisema huku akitoa vibao viwili vilivyotengenezwa kwa pembe tatu kila kimoja.
"Nakuahidi sitomwambia mtu." Nilimuhakikishia ndipo aliponikabidhi kibao kimoja naye alibaki ameshika kile cha pili, kisha akaendelea kunidadavulia kuhusu shule na elimu.
"Nakupa siri iliyoweka tofauti ya Elimu na Shule ambayo wengi hawaijui. SHULE ni sehemu maalum kwa ajili ya kuwafunza watu matokeo ya uvumbuzi, tafiti, maono na mawazo ya watu waliofanikiwa kabla yao ambayo yamekusanywa sehemu moja ili kuzipa changamoto akili zao. Pia ELIMU ni matokeo ya pevuko la akili kuweza kutafiti na kupambanua mambo kwa kina na kuzalisha mawazo ya uvumbuzi hata kuleta mafanikio kwenye maisha ya mtu na vizazi. Sasa watu wenye elimu walizijenga shule ili waweze kuwaonesha wengine elimu zao na vipi walizichuma ili kuyatanua mawazo ya wengine wapate kutumia akili zao na wao wakachume elimu na kuzikusanya shule wapate kufanya muendelezo. Ndio sababu kama utaitumia shule kwa umakini utaiona wapi elimu ilipo na utaifata. Na kama ukiipata na ukaitumia vyema unaweza kuongeza kitu ndani ya shule ili wengine waweze kujifunza pia kupitia wewe." Alipomaliza nilishusha pumzi na kumwambia.
"German Machine wewe si mtu wa kawaida ujue vitu unavyonambia ni vigeni kabisa? Kwa hiyo naweza nisiende shule na nikaipata elimu?"
"Hiyo ni bahati inayoendana na mazingira. Ingawa shule haikupi elimu lakini kumbuka shule ndipo kwenye njia ya kukuonesha wapi elimu ilipo ili uifate ama uiache. Shule ni sehemu ya kuifunza akili yako na kuipa changamoto ipate utambuzi wa kuitafuta elimu ambayo iko nje ya pale. Na utapoipata elimu shule pia itakuhitaji ili iyatumie mawazo yako kuzichangamsha akili za wengine ili nazo zijitambue. Sasa kama hujaenda kabisa shule ili uipate elimu unatakiwa uishi kwenye misingi ile niliyokwambia awali ama upewe kipawa maalum na Mungu na si vyenginevyo."
"Na je, unaweza kusoma shule mpaka umemaliza na usiwe na elimu?"
"Kabisa Twaha. Unaweza kusoma hata ukafaulu masomo mengi lakini bado ukaikosa elimu kichwani mwako na matokeo yake ukawa limbukeni wa mawazo ya watu walioelimika ambayo yametumika kukufundisha tu. Muda ushaenda Twaha kwa leo tuishie hapa ila hiko kibao nilichokupa nenda kakisimamishe kwenye dirisha la nyumba yenu wakati wa asubuhi jua lichomozapo au jioni lizamapo kisha simama kwenye pembe ya chumba ukiwa umelipa kisogo dirisha chukua kioo kimulikie upande wa dirisha na uwe unatazama jua kwa jicho moja kupitia usawa wa kibao tu, Kuna kitu utaona." Alinambia German Machine baada ya kunipa chakula cha ubongo.
"Ni kitu gani nitaona?" Nilimuuliza lakini alinisisitiza nikafanye hivyo nitajionea mwenyewe kisha atanipa tafsiri ya hiko nitachokiona pindi tutapokutana siku nyengine. Daaah! ama kweli maajabu ya German Machine yataendelea kusafiri kwenye ndoto zangu daima. Alinisindikiza siku hiyo baada ya kutoka na kumuaga baba yake aliyekuwa pale pale nje amekaa mkekani ameegama kwenye nyumba yao. Kila hatua niliyopiga niliihisi sauti ya German Machine na maneno yake ambayo hayakuendana kabisa na muonekano wake achilia umri. Nilipofika nyumbani usiku mzima nilimfikiria na kukumbuka maneno yake. Kesho yake niliamka subuhi na mapema niliwahi kufanya kama vile alivyonambia huku nikiwa mwingi wa shauku kujua ni kitu gani amenambia nitaona. Daaah! Jua lilipoanza kuchomoza ukweli nilichokiona kupitia kile kibao alichonipa nilistaajabu mno. German ama kwa hakika ni Machine.......