Wale wa simulizi. ..shunie ongoza wenzako kumtambua x mr....
Alibaki amemkodolea macho mama Shebby ambapo kikubwa alichokuwa anshangaa Hussein ambacho alikigundua ni alama ya baka la mstari mweusi juu ya paji lake la uso eneo lilipoanzia nywele kuota.
Alama hii safari hii aliiona vizuri baada ya ushungi aliojifunika mke wa mzee Mwinchande (mama Shebby) kufunuka bahati mbaya na alikuwa hajavaa kiremba kama ilivyokuwa kawaida, na hata chanzo cha kuvaaga kiremba Zai ilikuwa ni kwasababu ya kuficha baka la mstari pale juu ya paji la uso ndio maana ufungaji wake Kiremba ulikuwa wa kipekee sana, sasa imekuaje na mama Shebby nae awe na mitindo ya kufunga kiremba kama Zai harafu kumbe na yeye ana baka la mstari mweusi?
("Mh! hapana sasa nina wasiwasi")
alijisemea moyoni Hussein na kumuaga kwanza mzee Mwinchande akizuga kwenda chooni lakini ukweli hakuwa na haja yoyote zaidi alienda kukaa kufikiria kile alichokuwa amekiona pale nyumbani kwa mkwewe Kamishna Shebby.
("Inakuaje kuaje mama Shebby afanane vitu vingi na mke wangu Zai? au ni kweli yeye huyu! Eee Mungu naomba unisaidie nipande ufumbuzi wa uhakika wa hili suala")
aliwaza na kuomba kimoyo moyo Hussein pindi alipokuwa chooni akilifikiria sana lile jambo na alijaribu kukumbuka mambo mengi aliyokuwa anayapenda mkewe Zai kipindi hiko ili iwe rahisi kuzidi kuyapima na kuyafuatilia kwa mama Shebby kama kuna uwezekeno wa kufananisha mambo mengine zaidi.
("Mh! lazima nifanye hivi nione, ina maana kama kweli huyu ni yuleyule Zai mke wangu basi naamini babaake Shebby ndie adui angu Mr X mwenyewe. Mh!! lakini sasa mbona babaake Shebby haoneshi hata chembe kama ana moyo m baya? hafanani hata kidogo na vitendo vya mwana izaya Mr X.")
aliendelea kufikiria Hussein na hatimae alitoka kule chooni na kurudi sebuleni alipokuwa Mzee Mwinchande na kuendelea na maongezi yao.
"Basi inshaallah mzee mwenzangu, wewe tulia kisome kwa umakini sana hiko kitabu tuwe tunajumuika wote hapa kuswali suna za usiku na faradhi ya alfajiri"
"Nashukuru kaka, usihofu."
* * * *
Siku zilienda huku fukuto likizidi kufukuta kifuani na kichwani mwa Hussein juu ya kumtilia mashaka siku baada ya siku mama Shebby ambapo safari hii kila ile tabia sugu aliyokuwa anaikumbuka kuwa Zai alikuwa nayo alibaini kuwa hata mamaake Shebby alikuwa nayo na hii ikazidi kumpa uhakika wa asilimia nyingi kuwa akitafutacho ndicho akionacho.
Lakini uzito wa kuamini hilo unakuja pale kila jinsi alivyomtazama mzee Mwinchande alkuwa hafanani kabisa kuwa ni mtu mwenye moyo wa kikatiri na roho mbaya kama alivyo mr X kwani kama kweli mamaake Shebby ni Zai basi bila shaka babaake Shebby ni Mr X na hata akiwa siye bado Zai atajua wapi alipo kwa kuwa katika maneno ya mwisho ya mke wake Zai kabla hajapoteza fahamu baada ya kupigwa na kitu kizito siku ile walipovamiwa na Ninja wa mr X pindi walipokuwa wanaelekea kwa baba mkubwa ambae alikuwa mganga mzee Mnyungunyungu.
Lakini bado swali lengine lilikuja kichwani mwa Hussein bubu kama basi yule atakuwa Zai harafu yule mzee Mwinchande asiwe Mr X hivi usalama wao ungekaakaa vipi miaka yote hadi wanafikia pale wakati yeye tu aliponzwa kwa kuishi na Zai tena alikuwa mkewe kabisaa lakini bado Mr X alimfanyia matukio makubwa na wote waliokuwa na habari walau za tetesi kuhusu mr X waliuawa.
Sasa inakuaje kwa mtu anayejua kila kitu kuhusu mr X akaachwa hai hadi muda ule wakati mr X mwenyewe bado yu mzima?
Maswali yalikuwa mengi sana kwa Hussein babu bubu na kila alipoamka na kuwa anasalishwa na mzee Mwinchande yeye mawazo yake yalihama kabisa akiwa haamini kile akifikiriacho na mara akawa anaamini lakini bado akawa anaomba Mungu azidi kumpa uyakinifu zaidi katika lile swala na kila siku alitamani kumuuliza mama Shebby jina lake harisi ni nani lakini alishindwa wala hakujua aanzie wapi.
Baada ya siku saba fungate la kinyumbani nyumbani la Dokta Asha na Kamishna Shebby liliisha na kufanikiwa kuondoka na mkewe kuishi kwele yale makazi aliyoandaliwa na serikali kule karibu na gereza ambapo kulikuwa na nyumba za kisasa zilizojengwa na serikali kwa niaba ya makamishna wote nchini.
Na ulipotimu ule usiku ambao Shebby aliondoka Hussein bubu alipatwa na ndoto ya maajabu sana........
'''''''''
(^^"Tumuue tu mke wangu.^^")
(("^^ Hapana mume wangu kwa adhabu ya awali imetosha mbonaa!?^^"))
(^^"Hapana mke wangu atatusumbua huyu tusipofanya haraka."^^)
(("^^Mh ! sidhani kwani wewe unatakaje^^")
(^^"Vizuri, chukua dawa hii ujitahidi ifike kwenye chakula atachokula au maji atayokunywa hapo ataanza kumung/unyuka taratibu na hatochukua miezi mitatu atakufa"^^)
(("^^Haya ila moyo unaniuma daah!^^^"))
(^^"Usiumie Zai mke wangu"^^)
''''''''''
"Hee!"
alikurupuka Hussein mara baada ya kumuota mama Shebby na mzee Mwinchande wakijadili suala la kumuua.
Alikaa kitandani huku akihema na kuifikiria ndoto ile na pale pale lilimjia wazo atoke anyate kuelekea juu chumbani kwa mzee Mwinchande na Zai lakini hakujua aende kufanya nini ila alijikuta moyo unamsukuma atoke aende huko.
Aliangalia saa ilikuwa ni saa saba za usiku ndipo alipoanza kufungua mlango na kunyata taratibu kuelekea kule juu kulipokuwa na chumba cha mzee Mwinchande na mkewe.
Katika hali ya ajabu na mshangao mkubwa Hussein pindi alipokaribia tu kumbe muda huo mzee Mwinchande na mkewe walikuwa hawajalala wala hawakuwa chumbani zaidi walukuwa kwenye korido moja ya kisasa pale juu iliyotengenezwa kwa niaba ya kupumzika na kula kipupwe cha upepo wa bahari.
Kilichomstua zaidi Hussein si kutolala kwao bali ni maneno waliyokuwa wanaongea.
"Unaona Zai mke wangu, hii picha ya video ni siku ilee, hapa nahisi ndio alikugundua na kujifanya anaenda chooni kujisaidia kumbe kufikiria tu kwa kile alichoanza kukihisi. Nilikwambia mapema mke wangu, sasa acha kwanza nimpofue ili iwe rahisi kumpoteza jumla"
aliisikia vizuri kauli hii ya mzee Mwinchande iliyomfanya agande kwa mshtuko wa hasira na maumivu ya ajabu baada ya kujua ukweli sasa kumbe yule ni kweli Zainab mkewe na mzee Mwinchande ni Mr X....
Alianza kunyata taratibu Hussein bubu huku mapigo yake ya moyo yakienda kasi kupita kawaida akiwa haamini kabisa kama kweli leo hii amemtambua adui yake kwa mtindo ambao hakuwahi kuufikiria hata siku moja wala kuuota.
Alifanikiwa kufika mwisho wa ngazi taratibu na kuendelea kunyata kwa umakini mkubwa na kilichomsaidia zaidi alikuwa pekupeku ambapo mara alipofanikiwa kuukuta mlango wake na kuingia ndani tu aliufunga taratibu na ndipo alipofanikiwa hata kushusha pumzi ambayo alikuwa kaibana muda wote alivyokuwa ananyata kurudi mara tu aliposikia sauti ya mzee Mwinchande na mama Shebby ambae sasa aligundua kuwa ni Zainab yule yule mke wake wakijadili juu ya kumuua.
"Uuuuuphhhhhhhhh"
Alihema kwa nguvu Hussein huku akiwa kaegemea ukuta wa pale chumbani pindi alipoufunga mlango na kujikuta akisota kwa mgongo taratibu mpaka akakaa kitako pale chini huku mikono kiwa ameiweka kichwani.
("Heeee! Mungu kumbe muda wote niko katika chaka la Simba mla watu aliyevaa ngozi ya kondoo? hapana aaa uuupphhhh")
aliongea moyoni Hussein huku machozi yakimtoka akiwa anasugua sugua mikono kwa nguvu pale chini lakini mara aligundua kitu kilichomfanya ainuke haraka na kuzima taa kisha kujilaza kitandani moja kwa moja na kujifunika mwili wote.
("Huyu ni mshenzi mwenye mbinu nyingi sana, kama aliweza kunitegea kamera chooni nadhani hata humu chumbani kamera haikosi, sasa hapa inabidi niwe makini kabla hajawahi kunistukia kama nimemstukia ili niweze kumuua kiurahisi. Lakini nitamuua ua vipi mshenzi huyu? Aaaah.. Kivyovyote lazima nimuue. Naamini Mungu aliyeniotesha haya na kunnikutanisha nae ndie atayeniongoza na kunionyesha njia rahisi ya kummaliza huyu mshenzi loh! Kumbe mr X ni babaake kijana aliyenisaidia kutoka jera? au isije kuwa ndie Mwinshehe wangu?")
aliwaza Hussein na kufika mbali zaidi mara alipotia shaka isije kuwa na Kamishna Shebby akawa ndie Mwinshehe, jina la mtoto wake alieuawa akiwa na miezi minne tu.
("Zainabu...Zainabu...Zainabuu Mke wangu kumbe hukufa? aaaagh! Wanawake ni Wauaji kweli aaaaagh, au kwa sababu uliniona masikini Zai, si ungenambia tu nikuache uende salama nami nibaki salama...!!! Aaaaagh! Eeeeh Mungu kwaniniii Kwaniniiiiiiiii??!!!")
aliendelea kusema na moyo wake Hussein huku machozi yakimtoka mfurulizo na moyo kumuenda mbio kupita kawaida.
Mwili wote wa Hussein bubu ulibadilisha homon ghafra na kuanza kutetemeka kwa hasira mithili ya mgonjwa wa homa aliyemwagiwa maji ya baridi.
("Aaaagh! Zaiiii...Zaiii... Zaii!!!!? siaminiiiii aaaaaaaaaaaagh. Wanawake ni Wauaji..... Wanawake ni Wauaji..... wanawakeeeee!?")
(..........................) (.......................) (......)
(..."Zai ulijua kumbe ile barua ni ya nani lakini ulikanusha Zai? aaagh! Ulinipa moyo nipuuze kumbe kila kitu ulijua... aaagh! umemgeuka mumeo kwa ajili ya tamaaa kwa mtu baradhuli na katili kama huyu? Eti Mr X. aaaaagh! Samson alimuamini Delila kuwa mwanamke anayempenda bila kujua kumbe Delila anatumiwa kumchunguza na maadui zake. Yaliyokuja mkuta Samson mwanaume yeyote kweli yanaweza kumkutaaa. Zai!!!? Lazima nawe ufe")
Uchungu na mawazo aliyokuwa nayo Hussein uliendelea hadi pale alipostuliwa baada ya mlango kugongwa.
"Nani?"
aliuliza Hussein kwa sauti iliyojaa mikwaruzo.
"Swalaaa swalaaa.. Salaaa. swala ni bora kuliko usingizi"
aliisikia sauti ya Mzee Mwinchande akimuamsha waende wakasali na kugundua kuwa tayari ilitimu alfajiri.
("Kum**aako lazima Nikuue Mshenzi wewe.")
aliongea moyoni kwa hasira na kushuka pale kitandani hussein na kuwasha taa ili ajiandae kwaajili ya kuungana na adui yake katika kumuomba Mungu (kusali) pamoja.
* * * * *
"Mme wangu, mme wangu Nakupenda sana"
"Hata mimi nakupenda sana mke wangu Asha"
"Lakini sidhani kama nastahili upendo huo"
"Kwanini usistahili sasa! Unastahili kabisa na una haki nikupende zaidi ya hapa"
"Kweli?!"
"Kweli kabisa mke wangu. Kwanini unaniuliza hilo?"
"Kwa sababu nina wasiwasi."
"Wasiwasi!!? wasiwasi gani tena mke wangu.. Ondoa wasi kabisa Asha siwezi kuja kukutenda kwa mwanamke yeyote yule. Kwako mimi nimefika kabisa kama ni meli imetia nanga."
"Najua ni rahisi kusema hivyo kwa sasa, lakini sidhani kama kila siku utasema hivyo. Naamini kuna siku utanichukia kupita kiasi na nina wasiwasi utaniua."
"WHAT!!?"
Alistuka Kamishna Shebby baada ya kusikia kauli ile ya Asha pindi walipokuwa wanazungumza alfajiri ile wakiwa kitandani.
"Asha baby, mbona leo umeamka ukiwa na maneno makali sana?"
"Kwasababu ya maumivu baby"
"Maumivu? yapi tena"
"Ya mshono tuu"
Alizuga Asha pindi alipotaka kumwambia ukweli Kamishna Shebby juu ya yote ambayo hakuyajua kuhusu yeye lakini alijikuta anaamua kumkwepa baada ya moyo wake kuwa mzito ghafra na kushindwa jua aanzie wapi.
"Pole sana baby, sasa maumivu yako ya mshono ndio yasababishe nikuchukie? niache kumchukia mshenzi mr.........."
alisita Shebby baada ya kutaka kuropoka juu ya mr X na kukumbuka kauli na ushauri wa Cj4 kuwa asimzungumzie wala kumtaja Mr.X hata kwa mkewe ama wazazi wake bila kujua huyo anayemficha anajua mengi zaidi ya anavyomuona.
"Unasema umchukie Mr..!!? mr. ndio nani?"
aliuliza kimakusudi Asha na kuzidi kumpoteza kisaikology Shebby aliyeamua kutunga uongo wa palepale ambao Asha alijifanya kuukubali.
Maisha yao mule ndani kila mmoja alikuwa na siri ambayo mwengine haijui na mtu aliyekuwa anawaunganisha kwenye hiyo siri kila mmoja hajui kama mwenzake huyo mtu anamjua ama anawasiliana nae, na wote kwa pamoja walimuamini sana huyo mtu na kumsikiliza kutokana na mioyo yao kukiri kuwa huyo mtu amewazidi kila kitu kuanzia mbinu hadi uwezo wa kupambana kimwili.
Na hakuwa mwengine huyo mtu bali ni Komandoo aliyeaminiwa kati ya makomando kutoka Jwtz naye ni Komando Jumanne au Cj4. ambae sasa nae aliwaingiza kwenye mchezo Shebby na Asha baada ya kugundua siri ambazo aliona ili apate majibu inabidi acheze mwenyewe mchezo kama alioutengeneza Mr X ule wa vipofu lakini tofauti yeye aliwaweka vipofu rafiki zake, watu asio na visasi nao na kwa sababu maalum zenye faida kwao wote.