Makapuku Forum

Makapuku Forum

002f61aa98b783f696d29657c82dc57b.jpg
 
Sehemu ya 31.....



Shughuli za uagaji zilimalizika baada ya masaa matatu. Misafara ya viongozi ilianza kuondoka eneo la viwanja huku gumzo kubwa kwa wananchi na waandishi wa habari likiwa ni kuhusu Kamishna Shebby kusahau kilichowakuta hali ya kuwa yeye pekee alisalimika na ndie aliyepaswa kutoa maelezo yakinifu mbele ya umma.

******
Miezi mitatu ilikatika pasipo jibu rasmi kupatikana juu ya kile kilichotokea Mkuyuni. Japo kidogo habari za tukio la Mkuyuni zilianza kupungua midomoni mwa watu lakini bado zilizidi kufukuta vichwani mwa viongozi wakuu wa usalama nchini akiwemo Mh Rais. Tume iliyoundwa kwa agizo la rais ilikutana na ugumu wa kumfanya aseme kilicho nyuma ya pazia mfungwa ambaye ilibainika alikuwa chanzo cha Kamishna Shebby kuifanya kazi kinyume na taratibu za jeshi ili kuutafuta ukweli wa kesi ya mfungwa huyo. Lakini Hussein bubu alizidi kuwa bubu maradufu hakuwa tayari tena kusimulia kile alichomsimulia Shebby hata alipobanwa kwa kila namna. Mh Rais alichukizwa na kuamua kuivunja tume ya waziri baada ya kuona imeshindwa kufanya kazi yake ipasavyo. Kipindi hiko Kamishna Shebby alikuwa likizo chini ya uangalizi maalum akiugua mguu wake huku jitihada za kitabibu zikiendelea kwa kumsaidia akili zake zirejee katika utimamu haraka.
Kikao maalum cha faragha kiliendelea Ikulu baina ya Rais na mkuu wa majeshi. Ilionekana wazi tayari jeshi la polisi limezidiwa uwezo na akili kwa kile kilichotokea Mkuyuni.
"Kwa upande wa jeshi letu mheshimiwa haina haja ya kupeleka kikosi kama polisi. Hii kazi nina imani na uhakika itafanywa vyema na kijana mmoja aliyetoka Cuba mwezi ulioisha hakika namuamini na nina imani naye sana." Mkuu wa majeshi alimshauri Rais katika maongezi.
"Una imani ya hakika mtu mmoja ataweza kuujua ukweli uliojificha?"
"Haswaa! huyu ni zaidi ya mpelelezi pia ni mtu mwenye kipaji nina hakika ana uwezo wa kuifanya kazi pasipo hata kutumia muda mrefu. Ila suala hili inabidi lifanyike kwa siri muheshimiwa."
"Anhaa! basi vyema maana ni aibu kwa taifa kupoteza askari huku tukishindwa kujua hata muuaji ni nani? kama tukio la kigaidi ama laah! Najua dunia inatutazama kama tutashindwa kuubaini ukweli basi tunaweza kukosa pato kubwa hata kwa upande wa utalii watata shaka na usalama wa nchi yetu."
"Usiwe na wasi muheshimiwa kila kitu kinaenda kuwa sawa muda si mwingi ukweli utakuwa bayana ndani ya siku sitini tu zinatosha kwa kijana huyu." Mkuu wa majeshi alizidi kumtoa shaka Rais huku akimfafanulia kati ya siku hizo kuwa siku thelathini zitatumika kumtia ndani ya gereza kijana huyo na siku thelathini nyengine uraiani ambapo ataweza kugundua kila kitu ambacho alikuwa akikifatilia kamishna aliyepoteza kumbukumbu na hata kugundua hao waliowashambulia na kutambua kina nani na wapi walipo.
"Mh! una hakika anaweza kuifanya kazi hii kwa muda mfupi hivyo?"
"Haswaa muheshimiwa nawajua sana vijana wangu mashupavu na huyu anatoka katika moja ya kitengo nyeti sana si askari wa kawaida huyu ni Komando muheshimiwa."
Alimuhakikishia zaidi Rais na baada ya makubaliano papo hapo alipigiwa simu Kamanda mkuu wa jeshi la polisi na kuitwa ikulu na kupewa habari zile na kwa pamoja ukasukwa mpango pevu madhubuti utaokamilishwa kwa viendo na kijana huyo aliyeaminiwa na mkuu wa majeshi ya ulinzi JWTZ.
********
"Dokta Asha hivi kwanini kichwa changu kimekuwa kizito kila nikijaribu kufikiria kilichotokea hadi wenzangu wamekufa nami nimekuwa hivi nashindwa kukumbuka?!" Aliuliza Shebby pindi alipokuwa anafanyishwa mazoezi ya kutembea na yule daktari bingwa maalum wa kike aliyeitwa Asha. Wakati huo walikuwa kwenye bustani iliyokuwa nyuma ya jumba la mzee Mwinchande.
"Hapana usikate tamaa naamini utapozidi kupona taratibu na kumbukumbu zako zote zitarudi tu usihofu Shebby." Kwa sauti tamu ya upole aliongea yule dokta na kumfariji Kamishna Shebby ambaye aliumizwa na hali yake. Kupotea kwa kumbukumbu muhimu za kule Mkuyuni zilizidi kutesa kichwa chake akitamani kujua kwanini walienda huko.
"Ila Asha si unaona kila mtu haniamini ninavyosema sijui kitu..! Lakini ukweli sijui kitu mimi wala sikumbuki kabisa naona kama ni ndoto tu haya! hivi kweli nitaweza kukumbuka kabisa?"
Alisisitiza Shebby wasiwasi ulizidi kusambaa kichwani mwake. Wakati huo kwa ndani ghorofani alionekana mzee Mwinchande sambamba na mkewe wakimuangalia mtoto wao kwa dirishani jinsi anavyofanyishwa mazoezi na yule daktari. Walitabasamu na kumshukuru Mungu kwa hatua aliyofikia mtoto wao wa pekee iliyowapa matumaini kuwa atapona kabisa na kutembea vyema kama zamani.
"Hakika wanapendeza natamani hata huyu daktari angekuwa mkwe wetu kabisa au unaonaje mke wangu?" alisema mzee Mwinchande kumwambia mkewe.
"Mhh! kama ataridhia bila shaka hata mimi natamani hivyo baba Shebby fanya mpango naamini utaweza kumshawishi." Alisema mama Shebby kwa kuunga mkono huku akimtazama usoni mumewe. Mzee Mwinchande alitabasamu na wote waliendelea kuwatazama kina Shebby pale chini bustanini.

******

Siku zilikatika. Mapema siku hiyo dani ya gereza kubwa alilokuwa anafanyia kazi Kamishna Shaaban lilionekana basi la magereza lililokuwa limesindikizwa na difenda mbili likiwasili na kusimama kwenye eneo la maegesho huku ulinzi ulikaa sawa pindi walipoanza kushushwa wafungwa wapya walioletwa pale gerezani tayari kwa kutumikia kifungo chao. Baadhi ya wafungwa waliokuwa upande wa pili wakitenganishwa na ukuta wa seng'enge mbili waliacha kwanza shughuli za kufyeka fyeka na kuwaangalia wafungwa wapya waliokuwa wanashuka kwenye lile basi.
Ilikuwa ni idadi ndogo tu ya wafungwa wapya 12. Waliposhuka waliamuriwa kupanga mstari huku kamanda wa magereza akipita na kuanza kuwakagua akiwauliza majina kwa kuwaita kwa namba.
"namba nane.."
"ADORH JUMA"
"Tisa.."
"IDDI JUMBE."
"Kumi.."
"JUMA KOBERO"
"Kumi na moja"
"IBRA RADI"
"Kumi na mbili"
"HHAHAHAHAA.."
"Kumi na Mbilii..?"
"HAHAHAHAHAAAA''
Kilisikika tu kicheko kilichowashangaza askari wote na wafungwa waliokuwa wanamshuhudia kijana mmoja wa makamo mwili mkubwa, mfungwa mpya aliyekuwa anakamilisha ile idadi ya wafungwa wapya kumi na mbili. Lakini ajabu alipotakiwa ataje jina kama wenzake baada ya kuitwa namba yeye alicheka tu. Tena alicheka kwa sauti kubwa pasipo bila kujulikana kipi kimchekeshacho. Afande alichukia na kuita kwa mara ya tatu kwa sauti ya ukali.
"Kumi na mbiliiiii.."
"HAHAHAHAHAA WANAWAKE NI WAUAJIIII"
Safari hii nae alicheka kwa nguvu zaidi na kuongea maneno yaliyosikiwa na kumstua Hussein babu bubu aliyekuwa upande wa pili wa seng'enge akiendelea kufyeka pasi kuwaangalia wale wafungwa wapya waliokuwa wanahesabiwa. Lakini maneno aliyoropoka yule mfungwa mpya namba kumi na mbili yalimfanya aache kila kitu na kusimama kumuangalia huyo mfungwa ni nani aliyenukuu maneno kama aliyokuwa anasema yeye. Akiwa anamtazama kwa udadisi na umakini mkubwa ndipo macho yake yalipokutana na yule kijana ambaye sasa kipigo cha mikanda kilimshukia kutoka kwa askari magereza kama bakshishi ya dharau aliyoonesha kukaidi kutaja jina lake.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom