Rubani wa ndege mwandamizi wa shirika la United Airlines, Capt. Michael Tallon, amefungua kesi ya madai dhidi ya mwajiri wake akidai alilazimishwa kukubali tuhuma za uraibu wa pombe ambazo si za kweli, kinyume na hali yake halisi ya kiafya.
Kwa mujibu wa malalamiko yaliyowasilishwa mahakamani mjini Chicago, Tallon, mwenye uzoefu wa takriban miaka 30, alilazimishwa kuhudhuria tiba ya uraibu wa pombe, kuhudhuria mikutano ya kila siku ya Alcoholics Anonymous (AA), na kupitia vipimo vya pumzi mara mbili kwa siku, licha ya vipimo vya kitabibu kuonyesha hana matatizo ya uraibu.
Tukio hilo lilianzia Juni 10, 2023, alipokuwa mapumziko kwenye visiwa vya Azores, ambapo Tallon alianguka kwenye jiwe na kuumia kichwa. Licha ya dalili dhahiri za mshtuko wa ubongo, alituhumiwa kuwa mlevi na alionywa kuwa asipokubali kuwa ana uraibu wa pombe, hataruhusiwa tena kurusha ndege za United.
Katika hali ya kuchanganyikiwa, Tallon alikubali kujiunga na mpango wa matibabu ya uraibu maarufu kama HIMS, akielezwa kuwa atafukuzwa kazi endapo atakana tatizo hilo. Baada ya matibabu ya miezi kadhaa, madaktari kadhaa walithibitisha kuwa hana dalili yoyote ya uraibu, lakini United ilisisitiza aendelee na matibabu hayo.
Februari 2025, Tallon alifutwa kazi rasmi kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kukiuka masharti ya mpango wa HIMS. Anadai kufukuzwa kwake kwa njia hiyo kulipelekea kampuni ya United kuepuka kumlipa mafao ya ulemavu wa muda mrefu.
Tallon sasa anadai fidia ya mishahara iliyopotea, mateso ya kihisia aliyoyapitia, uharibifu wa sifa yake na gharama za kisheria, pamoja na agizo la kuilazimisha United kurekebisha utaratibu wa programu ya HIMS.
“Niliambiwa nikikataa kusema kuwa mimi ni mlevi, basi sitapanda tena ndege ya United,” alisema Tallon. “Nimesimama kidete kwa sababu siwezi kukubali jambo lisilo la kweli ili tu nipate mshahara.”
United Airlines imesema haitatoa tamko kwa kuwa kesi bado iko mahakamani.