Nitawaambia kitakachotokea lakini msiniite mtabiri!
Siku moja kwa jiwe fulani karibu na soko au kigenge cha vijana, vijana wawili ambao wamekufa marafiki na washikaji wa siku nyingi watakuwa wanapiga gumzo. Kama unavyojua tena mada za vijiwe zinaanzi mademu, siasa, mpira, n.k na kuishia tena kwenye mademu. Wakati wakijadiliana mara mmoja anasema "JK amewapendelea waislamu kwenye teuzi zake mbalimbali" huyo ni kijana wa kikristu. Yule wa kiislamu atabisha. Yeye (muislamu) atasema "mbona wakati Nyerere anateua wakristu huko nyuma hakuna aliyesema"? Mkristu atabisha, mabishano hayo yataendelea huku kila mmoja akijaribu kutoa mfano wa kuhalalisha maamuzi ya viongozi wetu. Hawa wawili wakiendelea kubishana kiustaarabu ndo jamaa mmoja asiyejua mwanzo wala mwisho wa kinachozungumziwa atakuja na kusema "Waislamu wote ni wapumbavu" au "Wakristu wote ni makafiri" Hapo ndipo yule atakayehisi dini yake imetukanwa atakapovurumusha ngumi...
Ngumi itajibiwa kwa ngumi... mara watu wanaanza kuchagua upande... waislamu wanajaribu kumuokoa muislamu mwenzao.. wakristu wanajaribu kumuokoa mkristu mwenzao... wakiendelea kusukumana, mara mtu anapigwa na ubao.... ndipo gumzo linapogeuka varangati!!!
Wakitawanyika, mtu asiyejua kilichokuwa kinabishaniwa.. anaenda na kusema "wale vijana wa kikristu wa mtaa fulani, wamemtukana Mtume wetu mtukufu"... ndipo shehe na maalim fulani wakati wa swala ya Ijumaa wakahamasisha waumini wao ili kupinga matusi dhidi ya Uislamu... wanaamua kuandamana kuelekea lilipo kanisa fulani... kutokana na hamasa.. vijana waanza kurusha mawe na mwishowe kanisa hilo linachomwa moto...
Vijana wa kikristu nao wanakasirika kwa sababu wanaambiwa vijana wa kiislamu wameenda na kukojoa ndani ya kanisa lao ...
hatimaye hadi mwisho wa mambo yatakapotulia... Watanzania wapata 100 watakuwa wamepoteza maisha yao.... mamia kadhaa kujeruhiwa... makanisa 20 kuchomwa moto na misikiti 39 kuvunjwa ......
tutakapokaa chini na kujiuliza nini kimetokea... jibu halitakuwa gumu....!!!
baada ya kusema hayo.... natema mate kando "Mungu aepushie mbali"..!