Awamu ya 6 ya Rais Samia Suluhu: Ni upi mustakabali wa 'wanasiasa pendwa' wa Hayati Magufuli?

Mashimba Son

JF-Expert Member
Dec 22, 2014
1,109
1,365
Kila serikali mpya inapoingia madarakani inakuwa na mtaji wake. Huo ni msemo maarufu wa wataalamu wa sayansi ya siasa na utawala bora kote duniani. Kwamba utawala mpya unapoingia madarakani unapenda kufanya kazi na aina ya viongozi unaowataka iwe kwa kuibua wapya au kuchagua miongoni mwa waliokuwa kwenye serikali iliyomaliza muda wake.

Hilo lilifanywa na aliyekuwa rais wa awamu ya tano nchini Tanzania Dkt. John Magufuli mara baada ya kukabidhiwa madaraka mwaka 2015, na vivyo hivyo kwa rais wa sasa Samia Suluhu Hassan ambaye alirithi kiti hicho Machi 19 siku mbili baada ya kifo cha mtangulizi wake.

Jumamosi ya Juni 26, itatimia siku 100 tangu Rais Samia achukue hatamu za uongozi na moja ya masuala yaliyoibua mjadala ambao bado ni endelevu mpaka sasa ni mustakabali wa kisiasa wa baadhi ya viongozi ambao walionekana ama kujipambanua kama vipenzi ama watoto wa kisiasa wa hayati Magufuli.

Baadhi yao ni wanasiasa waliokulia ndani ya chama tawala cha CCM wengi wao wakiwa ni vijana machachari na waliokuwa na wenye sauti kali katika uongozi wa Magufuli, baashi yao ni Paul Makonda, Ali Hapi, Antony Mtaka, Jokate Mwegelo,Lengai Ole Sabaya, Alexander Mnyetti, Albert Chalamila,Humphrey Polepole, Dkt.Bashiru Ali, Robert Odunga, Juma Homera ,Jerry Murro, Dkt.Dorothy Gwajima, Ummy Mwalimu,J erry Muro, Mwigulu Nchemba kwa kuwataja wachache.

Kundi la pili linajumuisha wanasiasa wahamiaji waliotoka vyama vya upinzani vya Chadema, CUF, ACT Wazalendo na kuhamia CCM ambao ni Anna Mghwira, Pauline Gekul, Marwa Ryoba,Profesa Kitila Mkumbo,Mwita Waitara, David Silinde,Dkt. Godwin Mollel, Patrobas Katambi, Julius Kalanga, Maulid Mtulia, Julius Mtatiro, David Kafulila na wengineo.

Je, nini kimetokea ndani ya siku 100?

Mosi, kuendelezwa imani kwa viongozi. Rais Samia amefanya mabadiliko mbalimbali yakiwemo makatibu wakuu, wakuu wa mikoa, kuteua mabalozi na viongozi wengine wa taasisi ili kuunda mwelekeo wa serikali yake. Mabadiliko hayo yanaonesha wazi kuwa nafasi ya wanasiasa pendwa wa Magufuli wanaweza kutafsiriwa kwa namna mbili; wapo walionufaika na uongozi wa rais huyo vile hawajaondolewa katika baraza la mawaziri.

Mathalani mawaziri wanaotokana na kuhamia CCM wamebakizwa, Profesa Kitila Mkumbo, Mwita Waitara,David Silinde, Dkt.Godwin Mollel na Patrobas Katambi. Wanasiasa wengine kutoka upinzania waliobaki madarakani ni Julius Mtatiro (mkuu wa wilaya Tunduru), David Kafulila(Mkuu wa Mkoa wa Simiyu), Juma Homera (Mkuu wa Mkoa wa Mbeya).

Pia baadhi ya wale waliotokana na CCM na kuaminika kupendwa na Magufuli wamebaki katika nafasi za uwaziri japo baadhi wakibadilishwa vituo vya kazi na Rais Samia, nao ni Dkt.Gwajima, Ummy Mwalimu, Mwigulu Nchemba, na wengineo.

Pili, wanasiasa wa upinzani kuingia serikalini. Awali alitangaza kuwa hataanglia chama kwa baadhi ya teuzi zake katika kuendeleza utamaduni wa kuteua mwanasiasa wa upinzani kama Magufuli alimteuwa Anna Mghwira kuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro ambaye alikuwa mwenyekiti na mgombea wa urais wa chama cha ACT Wazalendo mwaka 2015, naye Rais Samia ndiyo mteua Queen Cuthbert Sendiga kuwa mkuu wa mkoa wa Iringa. Sendiga aliwakuwa mgombea urais mwaka 2020 kutoka chama cha Alliance for Democratic Change (ADC).

Tatu, kuzaliwa vita vya makundi ya kisiasa ndani ya chama tawala. Duru za kisiasa kutoka ndani ya chama na serikali zinabainisha kuwa wakati Rais Samia anaendelea kuunda serikali yake kwa umakini bado anakabiliwa na kibarua kizito cha kivuli cha Magufuli. Inaeelezwa makundi mawili ya wanasiasa ndiyo hasa yanayochangia siasa za Samia Suluhu kwenda kimahesabu zaidi kuliko kawaida. Kundi la kwanza ni lile la wafuasi siasa za Magufuli limekuwa likifuatilia nyendo zake kwa umakini, huku kundi la pili la wahanga wa siasa na washindani wa Magufuli linamwona Samia kama mwokozi wao na kwamba ni tofauti na mtangulizi wake.

Licha ya Samia kubainisha kuwa yeye na Magufuli ni kitu kimoja ambapo ametafsiriwa kujaribu kulivuta kundi la wafuasi wa Magufuli. Kiongozi mmoja mwandamizi amewambia mwandishi makala haya unatafutwa mwafaka ndani ya CCM kuliko wa kitaifa. "Makundi haya ndani ya CCM yanaweza kumwangusha au kumwinua. Samia alikuwa sehemu ya utawala wa Magufuli akiwa msaidizi namba moja hivyo kila kilichoendelea alikuwa anajua, anawajua wanasiasa wazee kwa vijana, na sasa ameonesha kubadili mwelekeo wa kisiasa ambao lazima kundi moja litaachwa nyuma,"

Nne,wanasiasa wapendwa wa Magufuli wakumbana na makali ya Rais Samia. Kwanza tarehe 6 mwezi Aprili mwaka 2021 akizungumza wakati wa kuwaapisha makatibu wakuu Rais Samia aliwaonya wakuu wa mikoa,wilaya na wakurugenzi kuwa iwapo katika ziara zake atakuta kero za wananchi kwenye mabango ambazo zinaweza kutatuliwa na wakurugenzi basi wakuu wa wilaya nao watatimuliwa madarakani. Kati ya hoja zingine, suala la mabango limetajwa kuwa kiini cha kuondolewa madarakani Albert Chalamila aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mwanza ambaye mwezi Mei mwaka huu alihamishwa kutoka mkoa wa Mbeya. Chalamila ni miongoni mwa wanasiasa pendwa wa awamu ya tano amekumbana na rungu la Rais Samia.

Rais Samia amefanya mabadiliko hayo kwa uangalifu mkubwa akizingatia siasa za ndani ya chama na serikalini. Kuhamishwa kwa Ali Hapi kutoka Iringa kwenda mkoani Tabora kulitajwa kuwa hesabu za mwanzo wa kile kinachoitwa 'wanasiasa pendwa awa awamu tano' kufurumshwa madarakani. Kabla hajatulia mkoani Tabora tangu ahamishiwe mwezi Mei, Ali Hapi amehamishiwa mkoani Mara. Duru za kisiasa zinataja kuwa uhamisho wa Ali Hapi 'umetumwa ujumbe' kwa wanasiasa pendwa wa nafasi ya kurekebisha mienendo yao kwa sababu Rais anawafahau kwa ukaribu zaidi mienendo yao katika kipindi cha miaka mitano ya Magufuli.

Aidha, kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi kisha kupandishwa kizimbani kwa aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Lengai Ole Sabaya kwa makosa ya uhujumuuchumi na matumizi mabaya ya madaraka ni ishara nyingine ya Rais Samia amedhamiria kujitenga na kile ambacho Mbunge wa zamani wa jimbo la Igunga mkoani Tabora na mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania Rostam Aziz ni 'siasa za majitaka'.

Katika muktadha huo ni dhahiri kundi hilo limepokea ujumbe kuwa zama za siasa zimebadilika, na hatua ya nzito aliyochukua ni kuteua Sylvester Antony Mwakitalu kuwa Mkurugenzi mpya wa Mashtaka pamoja na uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamabana na Rushwa nchini Tanzania (TAKUKURU) Kamishna wa Polisi, Salum Rashid Hamduni.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Albert Chalamila, ambaye kauli zake na matendo yake yalizua utata toka wakati wa Magufuli pia ametimuliwa kazi hivi karibuni. Wengi waliamini alistahiki kukemewa ama kuondolewa madarakani toka wamu iliyopita, lakini aliendelea kusalia madarakani kutokana na 'kupendwa na mamlaka ya juu'.

Pindi alipohamishiwa Mwanza na Rais Samia, wengi walitafsiri hatua hiyo kama kumpandisha cheo, jamboa ambalo lilikosolewa vikali mitandaoni kutokana na kauli zake. Baada ya kualika watu kumpokea Rais Samia mkoani humo hata kwa mabango 'ya matusi' panga la mamlaka ya juu likamkata.

Je, nini mustakabali wao baada ya mshtuko wa kisiasa?

Ni nani asiyefahamu makeke ya aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda katika siasa na uongozi wa JPM? Jibu hayupo. Mwandishi wa makala haya mnamo tarehe 8 Septemba mwaka 2018 katika uchambuzi wake alihoji, "Sakata la Makontena; Je serikali ya Tanzania inampendelea Paul Makonda?" ambaye wakati wote wa utawala wa Magufuli hakuadhibiwa.

Licha ya Makonda kutajwa kwa makosa mbalimbali, huku viongozi wenzake wakitimuliwa mamlakani wakiwemo Nape Nnauye (aliyekuwa waziri wa habari) na Mwigulu Nchemba (aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani) bado aliendelea kuwa 'mtoto mpendwa'. Lakini sasa jina la Paul Makonda lipo machweo, halisikiki katika siasa tangu aliposhindwa jaribio la kura za maoni za kuomba kuteuliwa kuwania ubunge jimbo la Kigamboni mwaka 2020 kwa tiketi ya CCM.

Kuondolewa Balozi Dkt.Bashiru Ali katika nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi ambayo inamwezesha kuwa katibu wa Baraza la Usalama la Taifa unatajwa kuwa wa kijasiri ndani ya siku 100 za maisha bila Magufuli. Bashiru aliteuliwa kuwa mbunge, anakuwa mwanasiasa alama ya mjadala juu ya hatima ya wanasiasa yatima wa JPM, huku safu ya uongozi ndani ya chama ni kama imesafishwa na huko serikalini inaendelea kusafishwa.

Hali hiyo imechochea ukiwa mkubwa kwa waliokuwa wanasiasa pendwa wakati wa Magufuli kwa sababu Bashiru alikuwa kama ngao yao katika siasa tangu alipokuwa Katibu mkuu wa CCM na sasa wanaonekana kufutwa taratibu katika ramani ya siasa nchini Tanzania.

Richard Ngaya, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine nchini Tanzania amemwambia mwandishi wa makala haya wanasiasa waliokuwa karibu sana na hayati JPM baadhi yao bado wana nafasi kwenye siasa za kuanzia mwaka 2025. Hata hivyo ameonya kuwa hilo litategemea sababu kuu mbili walizonazo sasa kwa kuwa muda unaruhusu.

"Mosi, wanaweza kujisogeza kwenye kundi lililo na chama na serikali kwa sasa ili kuwa na uhakika wa kupata teuzi wa ndani ya chama kupitia kura za maoni. Pili, wanaweza kujijenga wao binafsi kupitia majukwaa mbalimbali zenye manufaa kwa wananchi kitaifa na Bunge ili kulazimisha chama kuwapa nafasi kwenye kura za maoni mwaka 2025.

"Na watakaoweza kujijenga kwa njia hii ya pili wanaweza kuwa na uhai mrefu kisiasa kuliko wale wa kujisogeza kwenye kundi linalotawala sasa. Hii ya pili inawafaa zaidi wabunge wa kuteuliwa wasio na majimbo kama Humphrey Polepole,Bashiru Ali na wengineo iwapo wana malengo zaidi kupitia siasa baada ya wakati huu ambapo wameingia kwenye siasa kupitia teuzi na si ushindani majimboni.

Aidha, amefafanua kuwa baadhi ya wanasiasa wengi wapo kwenye mshtuko wa kupoteza kiongozi ambaye alikuwa anatafsiri dira na uelekeo wa aina ya siasa mpya ambazo zinatajwa kuwa kandamizi. Kwamba kundi hili linaweza kukaa pembeni na kukaa kimya ili lisome mahitaji ya wananchi utakuwa nini kwa kipindi ambacho wao hawapo kwenye siasa za majukwaani na kutumia hayo mahitaji kama ajenda zao za kurejea kwenye uchaguzi mwaka 2030, huku wakiwa na dira ya kuepuka makosa ya kiufundi ya kwenye siasa za hayati JPM.

Credit to: Markus Mgaya/BBC

Binafsi nimeridhika na uchambuzi huu mwandishi kama amenisoma akili zangu.!​

bashiru.jpg
 
Back
Top Bottom