RC aingilia kati sakata la Rostam, Mwakyembe
Na Mwandishi Wetu,Singida
MVUTANO wa kugombea eneo la kuwekeza mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia upepo kati ya kampuni mbili zinazomilikiwa na wanasiasa nchini, sasa umeingia katika sura mpya baada ya mkuu wa mkoa wa Singida, Parseko Kone kuingilia kati na kueleza kuwa kila moja itapata eneo lake.
Kampuni za Power Pool East Africa, ambayo mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe amekiri kuwa na hisa na Wind East Africa, inayohusishwa na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, zinadaiwa kugombea ardhi katika kijiji cha Kisekida wilayani Singida Vijijini kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa kutumia upepo.
Kampuni hizo zinatarajiwa kuzalisha jumla ya megawati 500 kama miradi hiyo itaanza.
Habari za wanasiasa hao kuhusika katika mzozo huo wa ardhi ziliibuliwa na Mbunge wa Karatu, Dk Willibrod Slaa wakati sakata la ununuzi wa mitambo ya kampuni ya Dowans Tanzania Limited likiwa moto wakati Dk Mwakyembe alipodaiwa kukiuka kanuni za bunge kwa kutotangaza kuwa na hisa katika masuala ya umeme wakati akiomba nafasi ya makamu mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini.
Tuhuma hizo zilimfanya Dk Mwakyembe kujibu vikali akikiri kuwa na hisa kwenye kampuni hiyo, lakini akasema habari hizo zilichapishwa na magazeti ya Rostam kwa lengo la kumchafua. Mvutano huo tayari uliiweka pabaya serikali ya mkoa wa Singida ambayo ilituhumiwa na wananchi kuwa inatoa upendeleo kwa kampuni mojawapo.
Akizungumza na waandishi wa habari wiki hii, Kone alisema serikali ya mkoa haijatoa upendeleo kwa kampuni yoyote inayotaka kuwekeza umeme katika kijiji hicho, kutokana na taratibu za uwekezaji kuwa wazi na kila kampuni kutakiwa kuzifuata.
Alisema kilichotokea ni kuwa makampuni hayo mawili yaliingia katika mgogoro wa kugombea eneo hilo bila kujua kuwa maeneo wanayopatiwa ni tofauti, hivyo kuanza kuwatumia wananchi kwa kuwatia hofu juu ya kampuni nyingine.
Kone alisema kampuni ya Wind East Africa ipo katika mchakato wa kufanya tathmini ya mali katika eneo ambalo itawekeza ili iweze kutoa fidia kwa wananchi watakaotakiwa kuhama.
Aliwataka wananchi kuwa na subira kwani mgogoro huo umekwisha na serikali yao ipo makini kuhakikisha kuwa wananchi hawaporwi haki zao, bali ni kuona kuwa wanalipwa fidia kulingana na thamani halisi za mali zao.
Pia aliwataka wawekezaji kufuata taratibu za kisheria katika uwekezaji ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza baina yao na wananchi katika maeneo husika.
Alisema pia wanatakiwa kuwashirikisha wananchi kwenye eneo husika katika kila hatua ili wapate ushirikiano wa kutosha, na wamalize tofauti zao kabla ya kuja kuwekeza mkoani Singida.
Katika sakata la Dowans, Dk Mwakyembe na wengine wanapinga vikali serikali kununua mitambo hiyo kwa kuwa inapingana na Sheria ya Manunuzi ya Umma ambayo inaielekeza serikali kutonunua vitu vilivyotumika.
Dk Mwakyembe, ambaye aliongoza kamati teule ya Bunge iliyobaini ukiukwaji wa taratibu wakati wa kutoa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura kwa kampuni ya Richmond Development (LLC) ambayo mkataba wake ulirithiwa na Dowans, na wengine wanaonekana kuhisi kuwepo kwa ufisadi katika suala zima la ununuzi wa mitambo hiyo.
Rostam, ambaye alitajwa kwenye ripoti ya kamati ya Dk Mwakyembe, amekuwa hajitokezi kuzungumzia suala la Dowans na aliibuka hivi karibuni kujibu tuhuma za Mwakyembe kuwa alitumia magazeti yake kumchafua.
Rostam alimtuhumu Mwakyembe kuwa na ubaguzi na kumtaka ajibu tuhuma zake badala ya kuzungumzia wengine.
Akizungumzia sakata hilo, mbunge wa Karatu, Dk Willibrod Slaa alisema tofauti za wabunge hao wawili wa CCM zinatokana na kugombea eneo la kufua umeme kwa kutumia upepo.
Hata hivyo, wakazi wa kijiji hicho wameiomba serikali kuamua ni nani mwekezaji halisi kati ya kampuni hizo kwa vile mpaka sasa moja ya kampuni hizo imewalipa fidia wananchi na nyingine bado.
Akizungumza juzi na waandishi wa habari, msemaji wa wakazi wa kijiji hicho, Josephat Isango aliyekuwa ameambatana na mwenyekiti wa kijiji, Iddi Dadia na ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Jumanne Mtipa, alisema wamefikia uamuzi huo ili waweze kutoa wasiwasi unaowakabili.
Alisema katika kijiji hicho, kuna kampuni moja inayojulikana kwa jina la Power Pool East Africa, ambayo imeonyesha nia yake ya kuwekeza kuzalisha umeme unaotokana na nguvu za upepo na kwamba, tayari imejadiliana na wananchi na kuwalipa fidia wanaotakiwa kupisha mradi huo.
Isango alisema kampuni hiyo imeomba na kupewa eneo lenye ukubwa wa ekari 550 na imelipa fidia baada ya tathmini kufanywa na mthamini wa serikali katika eneo hilo na wananchi waliolipwa fidia wameanza kuhamia maeneo mengine kupisha utekelezaji wa mradi huo.
Isango alisema pamoja na kampuni hiyo, kuna taarifa ambazo zinatolewa na viongozi wa serikali kuwa kuna kampuni nyingine inayojulikana kwa jina la Wind East Africa ambayo imepewa eneo la kijiji hicho kwa ajili ya kuzalisha umeme bila kuwashirikisha wananchi.
Alisema hali hiyo imezusha mgogoro kati ya wananchi na viongozi wa serikali ya kijiji hicho kwa kuwa viongozi hao wametoa eneo hilo bila kuwashirikisha wananchi.
"Kimsingi tunaipokea kwa mikono miwili miradi yote, lakini tunahofu kwanini hawa Wind East Africa wasifike kijijini kwetu na kushirikiana na uongozi pamoja na wananchi katika kutenga eneo kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo," alihoji.
Alisema mpaka sasa Wind East Africa hawajawahi kufika kijijini hapo kwa ajili ya majadiliano na wananchi, lakini wamekuwa wakisikia kutoka kwa viongozi wa serikali akiwemo mkuu wa mkoa wakitambulisha kampuni hiyo.