Kwanini Marekani ina hofu na diplomasia ya China katika eneo la mashariki ya kati?

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,036
VCG111466557093.jpg


Kwa mara nyingine hali tete imetokea tena katika eneo la mashariki ya kati. Mbali na mgogoro wa Yemen, na mvutano kati ya Marekani na Iran, mgogoro kati ya Israel na kundi la Hamas umekuwa kuigonga vichwa vya habari, upande mmoja ukilaani vikali mashambulizi yaliyofanywa na kundi la Hamas na kusababisha vifo vya watu wasio na hatia nchini Israel, na upande mwingine ukilaani nguvu inayotumiwa na jeshi la Israel kujaribu kuliangamiza kundi la Hamas.

Mvutano na hata mapigano kati ya jeshi la Israel na kundi la Hamas, sio jambo jipya kwa wanazuoni wa mambo ya mashariki ya kati. Pande hizo mbili zimepambana si mara moja wala mara mbili, na matokeo siku zote ni yale yale. Lakini katika kipindi chote cha huko nyuma, Marekani imeonekana kuwa nyuma ya diplomasia ya kushughulikia changamoto hiyo, na siku zote matokeo yamekuwa ni yale yale.

Katika miaka ya hivi karibuni China imekuwa ikijitokeza zaidi kwenye diplomasia ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Mashariki ya kati. Na katika kipindi kifupi sana China imeweza kufanya jambo ambalo lilionekana kuwa ni ndoto. Imeweza kuzipatanisha Iran na Saudi Arabia na kufanya nchi hizo ziwe tena na uhusiano wa kibalozi. Wachambuzi wanaona kuwa mchango wa China umekuwa muhimu sana kwa nchi hizo mbili kurudisha uhusiano huyo, na kuitaja China kuwa ni mhimiza utulivu, mdau wa maendeleo, na mhimiza umoja katika eneo la mashariki ya kati.

Hivi karibuni kwenye mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai uliofanyika nchini Kyrgyzstan, Waziri mkuu wa China Bw. Li Qiang alikutana na maofisa waandamizi wa nchi za mashariki ya kati na kujadili suala la mgogoro kati ya kundi la Hamas na Israel.

Hali hii kimsingi inaifanya Marekani iwe na wasiwasi, kwani inaonekana kuwa China inaleta diplomasia mpya ambayo inalenga amani, utulivu, umoja na maendeleo. Hii ni tofauti kabisa na diplomasia ya Marekani katika eneo hilo ambayo msingi wake imekuwa ni kuleta mgawanyo, kuziwezesha kijeshi baadhi ya nchi na makundi ya kijeshi, au hata kuchochea mapigano kati ya baadhi ya nchi ili iendelee kuwa na udhibiti katika eneo hilo.

Uzoefu unaonesha kuwa diplomasia ya amani, utulivu, umoja na maendeleo ni jambo geni kabisa kwa eneo la mashariki ya kati. Kwa muda wa miongo kadhaa ambayo diplomasia ya eneo hilo imekuwa ikidhibitiwa na Marekani na nchi za magharibi, hali ya wasiwasi, vita, kutoaminiana ndio imekuwa ikitawala. Kujitokeza kwa China kwenye eneo hilo kunaonekana kuleta diplomasia mbadala ambayo itakuwa na manufaa kwa pande zote.

Kwenye mgogoro wa muda mrefu kati ya Palestina na Israel, na kwenye mgogoro wa hivi karibuni kati ya Israel na kundi la Hamas mwelekeo wa Marekani unaonekana kuwa ni ule ule…vita, vita, vita. Inashangaza kuwa wakati jumuiya ya kimataifa imekuwa ikipaza sauti kwa sauti mmoja kukomeshwa kwa mapigano kati ya Israel na kundi la Hamas, Marekani inatumia hali hiyo kuonesha umwamba kwa kutuma meli zake za kubeba ndege na hata kuchochea mgogoro huo kwa kusambaza silaha zaidi. Mapigano ya sasa yaliyosababisha vifo vya watu wasio na hatia wa upande wa Israel na Gaza si jambo la kufurahisha, lakini ni wazi kabisa kuwa baadhi ya wanasiasa wanalichukulia kuwa ni mtaji wao wa kisiasa.

Ni wazi kuwa dunia inatambua kuwa huu ni wakati wa kuwepo kwa diplomasia ya amani, utulivu, umoja na maendeleo. Kama diplomasia ya vita, mgawanyo na vurugu itaendelea kuwepo kwenye eneo la mashariki ya kati, ni wazi kabisa kuwa mzunguko wa mauaji ya raia wasio na hatia utaendelea kutokea.
 
Back
Top Bottom