Huyu ndio Nyerere GT anayedai alikwanza na anaendelea kukwaza maendeleo ya KusiniKombora la Mbunge Mudhihir lamtikisa Waziri Membe
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe, ametikiswa na kombora la Mbunge Mudhihir Mudhihir .
*Ajitetea anamheshimu, atajibu kwenye vyombo vya mkoa
Na Ramadhan Semtawa
MBUNGE wa Mchinga, Mudhihir Mudhihir hakutaja jina la waziri aliyemfananisha na "nyoka wa mdimu", lakini akasema kondoo wa manyoya atazizima mwenyewe na kujitokeza hadharani.
Jana Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe alijitokeza na kusema kuwa amepigiwa simu na watu wengine waliomwambia kuwa makombora hayo ya Mudhihir yanaelekezwa kwake na hivyo atachukua hatua kwa kulifikisha suala hilo kwenye vikao vya chama na serikali vya wilaya na mkoa.
Mudhihir, mmoja wa wabunge wenye kupenda kutumia misemo na methali huku akinukuu wanafalsa na vitabu mbalimbali, juzi alimlaumu mtu huyo kuwa ndiye anayetaka kiwanda cha saruji kijengwe kilomita 35 kutoka eneo lenye malighafi ambalo ni Mchinga.
Alisema mtu huyo, ambaye alimuelezea kuwa atawania urais katika uchaguzi wa mwaka 2015 anafanya hivyo kwa roho mbaya kwa kuwa hatanufaika lolote na msimamo wake kuhusu kujengwa kwa kiwanda hicho na kumfananisha na nyoka anayeishi kwenye mti wa ndimu ambaye hali majani yake wala ndimu, lakini mtu anayekwenda kuchuma ndimu kwenye mti huo humng'ata.
"Unajua nyoka wa mdimu ana hila sana; anapenda kukaa kwenye mdimu, lakini hali ndimu, ila akija mtu anayetaka kuchuma ndimu humshambulia, sasa yeye kiwanda kinataka kujengwa Mchinga, lakini anakizuia," alisema Mudhihir juzi.
Mudhihir, ambaye alikuwa akitumia mafumbo kwa kunukuu wanafalsafa mbalimbali, alitetea uamuzi wake wa kueleza bayana suala hilo alipotumia mfano wa mwendawazimu ambaye anatembea huku akizungumza kwa sauti na mtu mwingine ambaye anatembea akiwaza akilini masuala tofauti.
"Wote ni sawa, tofauti yake ni kwamba mmoja anazungumza kwa sauti na mwingine anazungumza kimyakimya," alisema mbunge huyo ambaye ni mwanafasihi.
Mudhihir pia alimnukuu mwanafalsafa ambaye alisema mtu ambaye hatumii akili yake, mambo humgeuka na akili huanza kumtumia yeye.
Wakati akitoa hoja na mifano yake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge, Sera na Uratibu), Philip Marmo aliingilia kati na kutaka wachangiaji wawe wanataja majina ya mawaziri wanaowatuhumu badala ya kutoa tuhuma za jumla. Alidai kuwa tabia hiyo imeanza kukomaa tangu mbunge wa Nzega, Lucas Selelii alipolituhumu baraza zima la mawaziri na kuliombea laana.
Hata hivyo, Spika Samuel Sitta alimtetea akisema hawezi kumlazimisha kila mchangiaji amtaje waziri anayemtuhumu, na badala yake akashauri wachangiaji waeleze kuwa wataliwasilisha jina la waziri anayetuhumiwa kwa Waziri Mkuu Pinda.
Alipoulizwa na Mwananchi jana, Waziri Membe alisema, tayari pia alishapata simu nyingi kutoka Lindi na watu wengine ambao walimwambia kuwa ndiye alikuwa akitajwa na Mudhihir.
"Sikusikia hiyo hotuba, lakini nimepata simu nyingi kutoka Lindi zikinieleza kwamba, mimi ndiye nilikuwa nikitajwa," alikiri Membe.
Membe jana alisema baada ya kupata simu hizo kutoka Lindi, ameamua kujiandaa kulitolea suala hilo ufafanuzi katika vikao vya chama na serikali ngazi za wilaya na mkoa ili lieleweke vema na kuondoa hisia za uadui na chuki kwa watu ambao wanatoka katika mkoa mmoja na wanaoheshimiana.
"Nimeamua kulitolea ufafanuzi (halmashauri kuu ya CCM) NEC wilaya, kikao cha baraza la ushauri la mkoa. Haya ni mambo ya aibu hatuwezi kulipuana hadharani," alifafanua Membe.
Membe, ambaye ni mmoja wa wabunge wanaotokea mkoa wa Lindi, aliongeza kusema: "Nisingependa kufanya malumbano na ndugu yangu Mudhihir."
Alisema anamheshimu Mudhihir kwa muda mrefu na ni ndugu yake, hivyo ni vema jambo hilo akalizungumzia kwenye vikao hivyo ili kuondoa malumbano zaidi hadharani.
"Niko tayari kwenda Mchinga. Nitazungumza na wananchi wa kule ili waweze kuelewa vema suala hili," aliongeza.
Waziri huyo aliongeza kwamba yeye ni mtu wa maadili hivyo asingependa kukaa na kuzungumza mambo ya aibu hadharani bila kufuata maadili.
"Unajua katika kazi kuna mambo ya ethics (maadili), sasa sitaki kuanza kukaa na kuvunja maadili hayo, mimi ni mtu ambaye najiheshimu na nafanya kazi kwa misingi na miiko ya kazi," alifafanua.
Alipoulizwa iwapo anahisi matamshi ya Mudhihir yana msukumo wa maadui wake kisiasa ambao wanahisi anaweza kugombea urais 2015, Membe alisema kwa vyovyote itakuwa hivyo.
"Bila shaka ... bila shaka. Mudhihiri ninayemfahamu mimi asingeweza kutoa matamshi ya aina ile, lakini nasema sihitaji kulumbana naye namheshimu sana," alisisitiza Membe.
Membe aliongeza kwamba yeye si kampuni inayofanya mradi huo, hivyo hata akituhumiwa inakuwa ngumu kuelewa na hivyo kulimaliza suala hilo ataliripoti kwenye vikao husika.
"Kwa unyenyekevu mkubwa, nitalifafanua hili ili kuondoa haya malumbano ya aibu," alisema.
Alipoulizwa jana, Mudhihir, ambaye aliwahi kuwa naibu waziri kwenye Wizara ya Elimu na Utamaduni, alijibu: "Mtu niliyemtaja ni kondoo wa manyoya ambaye ni yeyote atakayezizima."
Alipokuwa akisisitiza hoja hiyo awali, Mudhihir aliapa kwamba waziri huyo ambaye anataka urais mwaka 2015, hata akiwa rais hakuna malighafi itakayochukuliwa kutoka Mchinga.
Tangu kuanza kwa bunge la bajeti, kumekuwa na makombora mbalimbali ya wabunge dhidi ya mawaziri na baraza zima la mawaziri.
Mbunge wa kwanza kuanza kulipua mawaziri alikuwa Selelii ambaye alililaani baraza hilo akisema limejaa watu wenye roho mbaya na wanaotaka kukwamisha baadhi ya wabunge majimboni kwao.
Wengine waliotoa shutuma nzito kwa mawaziri ni mbunge wa Maswa, John Shibuda, aliyehoji kipimo cha uzalendo cha baraza hilo, huku akilituhumu kuwa ndilo linalobariki mikataba ya kifisadi.