Na Leon Bahati, Dodoma
MBUNGE wa Mchinga, Mudhihir Mudhihir (CCM) amesema hatishiki na uamuzi wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kuwa atamshtaki vikao vya CCM vya wilaya na mkoa baada ya kumtuhumu kuwa anakwamisha maendeleo kwenye jimbo lake.
Mudhihir, akiongea kwa mafumbo na kunukuu wanafalsafa mbalimbali, alimfananisha waziri huyo na nyoka anayeishi kwenye mti wa mdimu na kuuma watu wanaotaka kuchuma ndimu wakati hali matunda hayo.
Alikuwa akimaanisha kuwa Membe anatumia wadhifa wake kutaka kiwanda cha saruji kisijengwe kwenye jimbo la Mchinga wakati uamuzi huo hatanufaika nao.
Pamoja na Mudhihir kutomtaja Membe, waziri huyo alijitokeza na kusema kuwa ameshapigiwa simu na watu wengi waliomuhusisha na mafumbo hayo na hivyo akaahidi kulifikisha suala hilo kwenye vikao vya CCM vya wilaya na mkoa.
Juzi akizungumza na Mwananchi, Mudhihir alielezea kushangazwa na kauli ya Membe kujihisi kuwa ndiye aliyemzungumzia katika mafumbo yake, lakini akasema haogopi kushtakiwa kwa sababu anajiamini kuwa ana uzoefu katika mambo ya kisiasa na bunge kwa miaka 14.
"Kwa miaka 14 nimekuwa bungeni, sijawahi kumtaja mtu kwa kumsingizia," alisema Mudhidir huku akisisitiza kuwa hawezi kujibu hoja za kusadikika, akiimanisha tuhuma zilizotolewa na Membe juzi.
Alisema kuwa atamchukulia hatua kwa kufikisha suala hilo kwenye vikao vya CCM ili wamuadhibu.
Katika madai yake aliyotoa Jumatatu wiki hii wakati akichangia hotuba ya makadirio ya matumizi ya ofisi ya Waziri Mkuu, Mudhihir alidai kuwa mtu huyo anataka kiwanda kijengwe kilomita 35 kutoka eneo ambalo malighafi zinapatikana, ambako ni Mchinga.
Alisema karibu viwanda vyote vya saruji nchini vimejengwa kwenye maeneo ambayo yana malighafi, akitoa mfano wa kiwanda cha Twiga Cement kilicho Dar es salaam, na vingine vilivyo mkoani Tanga na Mbeya.
Alidiriki kusema endapo nia hiyo ya kujenga kiwanda mbali na eneo lenye malighafi itatekelezwa, wananchi wa Mchinga hawatakubali malighafi hiyo ichukuliwe hata kama mtu huyo atakuwa rais na kusema "watampiga mawe".