Kuna mtu ndani ya moto. (mkasa wa Sodder)

SteveMollel

JF-Expert Member
Jul 12, 2015
8,430
23,752
Mwaka ulikuwa ni 1945, usiku wa kabla ya Christmass huko Fayetteville, West Virginia, ambapo Bwana Goerge Sodder na mkewe Jennie pamoja na watoto wao tisa kwa ujumla walikuwa wamelala wakati moto ulipoanza kushika nyumba yao katika majira ya saa saba ya usiku.

Bwana George na mkewe walifanikiwa kuchoropoka toka kwenye nyumba hiyo inayoungua huku wakiwa wameongozana na watoto wao wanne; Sylvia, Marion, John na George, hivyo watoto waliobakia ndani ya nyumba iliyokuwa inaungua wakawa ni watano; Maurice, Martha, Louis, Jenne na Betty.

Na watoto hao watano walikuwa wanashea vyumba viwili vya kulala, vyumba vyote hivyo vikiwa kwenye ghorofa ya juu.

Basi baada ya bwana George kutambua kuwa watoto wake hao wamebakia ndani ya nyumba, akataka kurudi ndani upesi akawajulie hali na hata kuwaokoa. Lakini alipozama huko, akakuta ngazi za nyumba zikiwa zimeshika moto sana, asingeweza kuzitumia kukwea juu.

Alipoendea ngazi nyingine mahali ambapo huwa anaiweka, hakuikuta! Na alipotaka kutumia magari yake mawili anayoyaegesha sehemu yake maalumu ili apate kuyatumia kukwea basi huko juu, nayo hayakuwaka yote!

Mmoja wa wale watoto waliokoka toka kwenye moto, kwa jina Marion, akakimbia kwenda kwa jirani yao ili akapate kutoa taarifa kwa kitengo cha moto juu ya ajali hiyo iliyotokea, lakini alipofika huko simu ikaita sana pasipo kupokelewa. Na hata jirani mwingine alipopiga kutoa taarifa, napo simu haikupokelewa.

Basi ikamlazimu jirani mmoja aendeshe upesi kwenda kwenye kitengo cha moto, huko akakutana na chief mwenyewe wa kitengo hicho kwa jina bwana F. J. Morris.

Japokuwa kitengo hicho cha moto kilikuwa kipo umbali wa maili mbili na nusu tu toka kwenye eneo ambapo moto ulizuka, gari la zimamoto na uokoaji likafika mnamo saa mbili ya asubuhi tangu usiku wote huo. Hivyo kwa muda waliowasili, nyumba ikawa imeshafikia majivuni.

Majivu yakachukuliwa na kwenda kufanyiwa uchunguzi ili kubaini kama yana mabaki ya binadamu, lakini walipofanya hivyo hakukuwa na viashiria vyovyote vile ingawa watoto wale watano walidhaniwa kufia motoni!

Bwana F. J. Morris, mkuu wa kitengo cha moto, akasema kuwa huenda moto ulikuwa mkali sana kiasi kwamba ulitafuna kila kitu kwenye miili ya watoto wale, ikiwamo mifupa yao.

Lakini taarifa hizi zikaja kuaminika si sahihi. Hata nyama yote ya binadamu ikitafunwa na moto, bado mifupa itabakia. Na zaidi hakukuwa na harufu yoyote ya nyama ya binadamu kuungua.

Basi baada ya muda kidogo, vyeti vya vifo vya watoto hao vikatolewa ikiwa inaaminika kuwa moto ule ulisababishwa na hitilafu za kiumeme. Mahali pale ambapo nyumba iliungua, bwana George Sodder akapatengenezea kuwa kumbukumbu ya wanawe waliojifia humo.

Lakini muda mfupi baadae, Bwana George Sodder na mkewe wakaanza kuhisi huenda watoto wao hawakufa kama wanavyodhani bali walitekwa, na moto ulikuwapo tu kama danganya toto kupoteza ushahidi.

Lakini kwanini mtu ateke watoto wa George? Pengine tumtazame haswa bwana George ni nani.

Inaaminika bwana huyu alikuwa ni mtu mweye asili ya Italy, tena toka katika kijiji ambacho kilikuwa na mahusiano mabovu na dikteta wa kiitaliano, bwana Benito Mussolini. Hivyo huko Marekani bwana George alihamia tu, na bwana huyu hakuwahi kusema kwanini aliondoka Italy hivyo ikaanza kujenga hoja kwamba labda mwanaume huyu aliwahi kujihusisha na biashara za vificho huko Italy atokeapo, hivyo inaaminika kati ya sababu hizi inaweka ikawa imepelekea watoto wake kutekwa.

Ebu tutazame hapa …

Masaa machache usiku kabla ya moto kuzuka, bwana George alitembelewa na mjumbe wa bima ya maisha. Na mjumbe huyu alipoona kuwa Bwana George hakuwa anavutiwa na mashauri yake ya kibima, akaghafirika na kupayuka,

“Nyumba yako hii ya kishenzi itapotelea kwenye moshi. Watoto wako wataharibika na utalipia maneno yako yote ya hovyo kumhusu Mussolini!”

Lakini pia tukirudi nyuma, siku ya nyuma kabla ya moto kuwaka, watoto wawili wa kiume wa bwana George Sodder wakiwa wanatokea shule walimwona mwanaume mmoja barabarani akiwa anawatazama kwa urefu. Na siku ambayo moto uliwaka, kwenye majira ya usiku wa saa sita na nusu, simu iliita lakini haikupokelewa.

Jennie, mke wa bwana George Sodder, alitanabahi kuwa taa ilikuwa inawaka huko sebuleni. Na akiwa anafunga macho yake alale, akasikia sauti kubwa ya kubamiza paa ikifuatiwa na sauti ya kitu kinachozunguka! Lisaa limoja baadae akaja kuamka moshi ukiwa unaingia ndani.

Taarifa inayosisimua ni kwamba, bado taa ilikuwa inawaka. Sasa kama sababu ya moto ule ilikuwa ni hitilafu ya kiumeme kwenye soketi kama ilivyosemwa mwanzoni basi taa hiyo isingalikuwa inaendelea kuwaka kwa muda huo.

Baada ya moto kuwaka na George kugeuza eneo hilo kuwa la kumbukumbu ya wanae aliodhania wamefia humo, walipotembelea eneo hilo muda mwingine mtoto wa George Sodder aitwaye Sylvia Sodder aliokota kitu ndani ya eneo hilo, kitu ambacho Jennie aliamini inawezekana ikawa ndicho kilitumika kupigia paa aliposikia sauti ile usiku ule.

Lakini baada ya bwana George Sodder kufanya upelelezi zaidi juu ya kitu hicho akagundua kilikuwa ni kifaa kinachoitwa ‘NAPALM PINEAPPLE BOMB’. Aina fulani ya kifaa cha bomu kilichokuwa kinatumika kwenye vita kipindi hiko cha zamani.

Bila shaka sasa tunaweza tukaamini kuwa nyumba hii ilichomwa na si kwamba ni ajali, sio?

Basi kwa ajili ya kuhakikisha kama kweli moto unaweza kumpoteza mtu kabisa, Jennie, mkewe na George Sodder, akafanya majaribio ya kuchoma wanyama lakini kote huko mifupa ikabakia tofauti kabisa na wanae.

Hata alipotumia moto wenye degree alfu mbili za joto tena kwa masaa mawili, bado mifupa ilibakia vilevile. Sasa ilikuaje kwa nyumba yake ambayo iliungua kwa dakika arobaini na tano tu?

Vuta pumzi kwanza. Tayari? Kunywa na maji kidogo. Haya tuendelee …

Basi kama haitoshi tunaambiwa kwamba kulikuwa na ripoti kadhaa za kuonekana kwa watoto ambapo shushuda mmoja alisema, yaani wakati moto kule unaendelea kuwaka, aliona watoto ndani ya gari wakikatiza barabarani. Na pia kesho yake, yaani December 25, shuhuda mwingine, ambaye anakaa maili kumi na tano tokea ajali ya moto ilipotokea, naye akaibuka na kusema aliwaona watoto majira ya asubuhi kuamkia ajali hiyo. Kwa kunukuu alisema,

“Niliwapatia chakula cha asubuhi. Na kulikuwa na gari lenye usajili wa ‘plate number’ tokea Florida.”

Na kama hautoshi kuna mwanamke mmoja kwenye moja ya hoteli inayopatkana huko Charleston alidai kuwaona watoto wanne kati ya wale watano lakini ikiwa imeshapita juma moja tangu moto utokee.

Juma moja …

Kwa kumnukuu mwanamke huyo alisema, “Watoto walikuwa wakisindikizwa na wanaume wawili na wanawake wawili, wote wakiwa na asili ya Italy. Nilijaribu kuongea na watoto wale kiurafiki lakini wale wanaume wakawa maadui kwangu na wakanikataza kufanya hivyo. Nilihofia hivyo sikusema kitu tena. Kesho yake asubuhi ya mapema, wakaondoka zao.”

Mnamo mwaka 1947, miaka miwili tangu moto ujiri, George na Jennie wakajaribu kuwahusisha FBI (Federal Bureau of Investigation) kwa ajili ya msaada. Lakini katika namna ya kushangaza kidogo, polisi na hata kitengo cha zimamoto na uokoaji wakakataa kutoa msaada!

Mmmmmh, Hivi unaanza kuhisi nini kwa hiki kitengo cha zimamoto na uokoaji?

Basi kwakuwa ilishindikana huko, bwana George na Jennie wakamwajiri mpelelezi binafsi kwa jina la C.C. Tinsley. Bwana huyo alipokuja kufanya upelelezi akabaini kuwa mmoja wa wajumbe wa coroner’s jury ambao walitoa maamuzi kuwa tukio lile la moto lilikuwa ni ajali tu alikuwa ni yule wakala wa bima ambaye alikorofishana na bwana George Sodder hapo awali.

Lakini kabla hatujaendelea, Coroner’s jury ni nini? Ebu tujuzane tusije kuachana njiani.

Coroner’s jury ni bodi rasmi ambayo inakuwa inamwongoza afisa maamuzi kwenye mambo ama mashtaka ya ghafla na vifo vya kutiliwa mashaka. Kwahiyo sasa katika bodi hiyo ambayo inamwongoza afisa kufanya maamuzi, mmoja wao ni bwana yule wa bima. Nadhani tumeelewana hapo.

Lakini kwanini bwana huyu wa bima hakuwahi kuhojiwa tokea mwanzo na ingali kuna mashaka kumzunguka?

Baada ya kila kitu, gavana wa jimbo akatangaza rasmi kesi hii kufungwa na kufanya matumaini ya familia ya Sodder kufikia kikomo. Lakini zaidi ikiwaachia uchungu mkubwa wa kupoteza watoto wao wengi na huku vyombo vya usalama vikionekana vizito kuchukua hatua.

Nanukuu maneno yao, “Yapi yalikuwa malengo ya maafisa waliohusika na hili? Ni nini walikuwa wanakipata kwa kututaabisha miaka yote hii ya kukosa haki. Kwanini walituongopea na kutulazimisha tuamini uongo huo?”

Watu wamekuwa na maoni tofauti juu ya swala hilo la familia ya George Sodder. Baadhi wanaamini ‘mafia’ walihusika kwenye swala hilo. Wengine wakiamini watoto hao watakuwa wamepelekwa huko Italy.

KIDOGO MATUMAINI YAJA BAADA YA MIAKA …

Ikiwa imepita miaka ishirini na tatu tangu moto utokee, kidogo likaja tumaini ambapo picha ilitumwa kwa Jennie Sodder, mama mtu, picha ambayo ilikuwa ni ya mwanaume mwenye makadirio ya miaka ishirini na. Picha hiyo ilitumwa moja kwa moja kwa anwani ya mama huyo lakini ikiwa haina anwani ya kurejeshea.

Ila picha hiyo ilikuwa ina muhuri wa eneo liitwalo ‘Kentucky’.

Basi George na Jennie wakaamini kabisa kuwa picha ile ilikuwa ni ya mtoto wao anayeitwa Louis Sodder. Mwanaume yule kwenye picha alikuwa na macho ya brown kama ya mtoto wao Louis, nywele zilizojiviringita na pia pua iliyonyooka wima na nyusi moja iliyosimama.

Nyuma ya picha kulikuwa na maneno yalosomeka, “Louis Sodder. Nampenda kaka Frankie …”

Kutokana na hayo, George na Jennie wakamwajiri mpelelezi binafsi aende huko Kentucky akamtafute Louis, lakini ajabu mpelelezi huyo hakusikika tena. Haijulikani nini kilimtokea!

Muda mfupi baadae, mnamo mwaka 1969, bwana George Sodder akafariki dunia akiwa na umri wa miaka 74. Na mwaka 1989, Jennie akafariki akiwa na miaka 85.

Sylvia Sodder ndiye mtoto pekee aliyebakia kwa upande wa familia hii, na yeye bado anaamini kuwa nduguze hawakufa kwenye ule moto. Jennie Henthorn, mtoto wa Sylvia Sodder, na yeye anaendesha kampeni ya kutafuta taarifa za watu hao na kwa yeyote ambaye anazo anaweza tuma kwenye mtandao wa ‘websleuths.com’.

Jennie Henthorn anasema kuwa mama yake, bibie Sylvia Sodder, alimuahidi bibi yake, yaani Jennie Sodder, kuwa hatoacha habari hiyo ipotee.

Kwa muda wote huo hamna majibu ya kueleweka, je watoto hao walifia motoni au walitekwa?






images-3.jpg


Sent using Jamii Forums mobile app
 
Ili mtu afanye tukio lazima kue na faida flani atakayoipata. What was the motive behind the murder/kidnapping?

Sent using Jamii Forums mobile app
Nobody knows as nobody was confirmed guilty. Yote yalobakia ni madhanio tu, kubwa huenda kuna mahusiano kati ya kile kilichomwondoa Sodder Italy na kupotea kwa watoto wake...

Sent using Jamii Forums mobile app
 
nilitegemea jamaa alivyoingia ndani kuwaokoa wanae, alimwona mtu mwingine kwenye moto(sio kuungua) kutokana na nilivoelewa kichwa cha mada.
 
nilitegemea jamaa alivyoingia ndani kuwaokoa wanae, alimwona mtu mwingine kwenye moto(sio kuungua) kutokana na nilivoelewa kichwa cha mada.
Kichwa cha habari kimekaa kifasihi tu. Ya kwamba ndani ya moto huo kuna mtu, yaani kisababishi au muwashaji, ila hakuonekana wala kugundulikana mpaka leo hii

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom