Bunge sasa kuchunguza Kiwira na Bulyanhulu
2008-10-30
Na Abdallah Bawazir, Dodoma
Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imekuja juu na kutaka ufanyike uchunguzi jinsi serikali ilivyouza hisa zake katika migodi ya Kiwira, Bulyanhulu na Mwadui na mahali fedha hizo zilipokwenda kutumika na taarifa yake itolewe bungeni.
Akisoma taarifa ya Kamati hiyo kuhusu yaliyomo katika taarifa ya Kamati ya Rais ya Kuishauri Serikali Kuhusu Usimamizi wa Sekta ya Madini nchini, bungeni mjini hapa jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, William Shellukindo, alisema pamoja na kukubaliana na mambo mengi yaliyomo katika mapendekezo ya kamati ya Rais iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Mark Bomani, lakini kamati yake inataka ufanyike uchunguzi wa kina katika migodi hiyo ili kuondoa utata uliopo.
Alisema kwa kuwa kumekuwa na matatizo na malalamiko mengi katika umiliki wa hisa katika migodi hiyo na jinsi hisa hizo zinavyouzwa na haijulikani fedha za mauzo zilipokwenda, kamati yake inaona ni vema ufanyike uchunguzi na kisha matokeo ya uchunguzi huo yasomwe mbele ya wabunge ili kujua ukweli wa mambo.
Wakati kamati hiyo ikitaka uchunguzi ufanyike katika migodi hiyo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, ametaka uchunguzi huo usiishie katika migodi hiyo tu, bali pia ufanyike katika mgodi wa Buhemba ili kujua uhusiano wake na kampuni ya Meremeta.
Mbunge huyo pia alitaka uchunguzi mwingine ufanyike kuhusu malalamiko ya wananchi kuwa kuna watu waliofukiwa wakiwa hai katika mgodi wa Bulyanhulu, mkoani Shinyanga.
Akitoa maoni yake kuhusu hoja hiyo, Zitto ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati ya Rais, alisema anaunga mkono pendekezo hilo la Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini la kutaka ufanyike uchunguzi huo, akieleza kuwa uuzwaji wa Buhemba unatia shaka kwani umeikosesha serikali fedha nyingi.
Alidai kuwa mgodi huo ulinunuliwa na mwekezaji kwa Dola za Marekani milioni 20, lakini mwekezaji akauuza kwa Dola za Marekani milioni 348 huku serikali ya Tanzania ikiambulia patupu.
Kuhusu mgodi wa Buhemba, alitaka uchunguzi wa ufanyike kwani mwekezaji aliyekuwa akiumiliki ameondoka katika mazingira yasiyojulikana tena bila ya kuwalipa wafanyakazi haki zao na kukiuka makubaliano mengi ya mkataba na baadaye kuuza kinyemela mgodi huo kwa kampuni ya Maremeta.
Awali, Shellukindo alisema kuwa kutokana na matatizo yaliyojitokeza, kamati yake pia inapendekeza usitishwaji wa serikali kumiliki hisa katika migodi na badala yake shughuli hiyo ihamishiwe kwenye Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na kutekeleza jukumu hilo kitaalamu kwa niaba ya serikali.
Pia aliitaka isitishe mipango yake ya kuendelea kuuza hisa zake katika migodi ya Buckcreef Gold Mine (Geita), Kiwira Coal Mines, Williamson Diamonds na mingineyo, mpaka hapo itakapojipanga vizuri zaidi kwa njia ya kuiwezesha STAMICO kusimamia hisa na kuiwezesha kushiriki katika kutoa maamuzi endelevu ya migodi hiyo.
Shellukindo alisema Kamati yao imeishauri serikali iangalie kwa makini uwakilishi wake katika bodi za madini ambazo ina hisa kwa kuteua wawakilishi wenye uwezo wa kutetea maslahi ya serikali na kushauri kuwa uteuzi huo uzingatie vigezo vya weledi, uadilifu na uzoefu katika nyanja za uchumi, fedha, madini na sheria.
Awali akisoma taarifa ya mapendekezi ya Kamati ya Rais, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alisema kuwa kamati hiyo imeishauri serikali ifanye marekebisho katika sera na sheria za madini nchini ili sekta hiyo iweze kutoa mchango wake mkubwa katika uchumi wa nchi.
Alisema kuwa kwa sasa sekta ya madini inachangia asilimia 3.5 tu ya pato la taifa kiasi ambacho ni kidogo ikilinganishwa na kukua kwa sekta hiyo nchini, hivyo kamati hiyo imependekeza kuwa serikali kwa sasa isiingie mkataba wowote mpya wa madini hadi hapo sheria mpya ya madini itakapopitishwa na Bunge na kuanza kutumika.
Ngeleja alisema kamati hiyo pia imependekeza kuwa sheria ya sasa ya uchimbaji wa madini aina ya vito ambayo inatoa nafasi kwa Watanzania kuwa na hisa za asilimia 25 tu na nyingine kumilikiwa na wageni ifanyiwe marekebisho ili madini hayo yachimbwe na Watanzania wenyewe kwa asilimia 100.
Wakichangia taarifa hiyo ya Kamati ya Rais, wabunge walipongeza kazi nzuri iliyofanywa na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ya kuleta mabadiliko katika sekta ya madini ili taifa liweze kunufaika zaidi na rasilimali hiyo.
Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango, aliunga mkono ushauri wa Kamati hiyo ya Rais kutaka madini ya vito yachimbwe na Watanzania kwa asilimia 100, akisema kuwa madini hayo hayahitaji mitambo mikubwa ya uchimbaji hivyo Watanzania hawatashindwa kuyachimba.
Mbunge huyo alikwenda mbali zaidi na kushauri kuwa kampuni moja ya kigeni ambayo ipo Mererani (hakuitaja jina) mkataba wake usitishwe mara moja na ikiwezekana ilipwe fidia ya kuvunja mkataba huo ili uchimbaji wa madini hayo yafanywe na Watanzania pekee.
Alitahadharisha kuwa endapo kampuni hiyo itaachiwa iendelee kuchimba madini hayo na huku ikijua kuwa kuna sheria inayokuja ya kuzuia wageni kuchimba madini hayo, inaweza kuongeza kasi ya uchimbaji ili iweze kupata madini mengi zaidi kabla ya sheria kuanza kutumika.
``Tunamuomba Rais achukue uamuzi huu mgumu maana wakati mwingine ili uendelee unahitaji kuchukua maamuzi magumu na sisi wabunge tutakuwa nyuma yake tunamuunga mkono,`` alisema mbunge huyo machachari katika kutetea hoja zake.
Naye Mbunge wa Busega, Dk Rafael Chegeni, alisema Tanzania haistahili kuwa ombaomba bali tatizo imeshindwa kutumia vizuri rasilimali zake ilizonazo kama madini na wakati mwingine kufanya maamuzi ya papara yasiyo na faida kwa taifa.
Alisema wachimbaji wadogo wamekuwa kama wakimbizi katika nchi yao kwani hawajawekewa utaratibu maalumu wa kuendesha shughuli zao, hata pale wanapoendesha shughuli zao za uchimbaji huondolewa na serikali na eneo hilo kupewa wageni.
Naye mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrodi Mkono (CCM), amehoji fedha zilizotokana na mgodi wa Buhemba ambazo zimehifadhiwa nchini Mauritius kutorejeshwa nchini.
Mkono alihoji suala hilo wakati akichangia mjadala kuhusu ripoti ya Kamati ya Rais ya kuchunguza mikataba ya uchimbaji wa madini, bungeni, mjini Dodoma jana.
Alisema anashangazwa kuona suala la fedha hizo limekuwa likipigiwa kelele nje ya Bunge, lakini wabunge wanapofika bungeni hawalizungumzii kabia suala hilo.
``Hivi wamepewa nini kinachowanyamazisha? Nataka kujua kuna nini Buhemba?,`` alihoji Mkono.
Alisema Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa wakati akiwa Waziri Mkuu, aliwahi kumkabidhi kwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha kutembelea mgodi huo, lakini hakuna tija yoyote iliyopatikana.
Mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM), Chrisant Mzindakaya, alishauri ripoti za tume zinazoundwa zitekelezwe, badala ya serikali kuendelea kuunda tume kila siku bila kutekeleza ripoti zake.
SOURCE: Nipashe