Kuna wakati chepeo lazima iitwe chepeo na kijiko kiitwe kijiko. Kuna wakati ambapo mtu aliyechukua kitu kisichochake bila kuomba isiitwe kuazima bali iitwe wizi na kuna wakati ambapo viongozi wanapojigawia mali ya wananchi kama njugu tusiseme wamestaafu siasa bali tuwawajibishe hata kama hawatakikusikia. Binafsi leo nimeamua kuwatolea uvivu Rais Mstaafu Mkapa na Waziri wake wa Nishati na Madini Bw. Daniel Yona. Ndugu zetu hawa wametumia nafasi zao vibaya kujichukulia mali ya taifa hili na bila haya wala shaka wameliingiza Taifa kwenye mkataba mbovu kabisa kuliko yote iliyowahi kuingiwa na nchi yetu. Watu hawa wawili wanyanganywe mali hiyo na irudishwe kwenye usimamizi wa Taifa hadi mwekezaji makini atakapotokea.
Kwa muda mrefu gazeti dada la Kulikoni limekuwa likiandika habari kuhusu jinsi viongozi hawa walipokuwa madarakani walivyoweza kutumia nafasi zao kujichukulia kampuni ya Kiwira Coal Mine na kujimegea hisa nene kwenye kampuni hiyo wao wawili na familia zao wakishikilia karibu asilimia themanini na tano ya kampuni hiyo. Hakuna mtu ambaye yuko tayari kuelezea hadharani ilikuwaje Rais wa Jamhuri ya Muungano na Waziri wake wa Madini waweze kujipatia kampuni hiyo ya makaa ya mawe. Hivi ni nani anajua hizo hisa za asilimia 85 ziliuzwa kwa kiasi gani na kina Mkapa na Yona walilipa kiasi gani na toka wapi?
Wakati Waziri Daniel Yona akiwakilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2004/2005, alisema hivi kuhusu machimbo ya Kiwira juhudi za kumtafuta mbia ili aweze kuufufua mgodi huo zimekukuwa zikielekezwa kwa makampuni toka China. Hata hivyo, kwa kuwa jitihada hizo za muda mrefu hazijazaa matunda, sasa PSRC imefungua milango kwa wawekezaji wengine watakaojitokeza.. Kauli hiyo iliyotolewa Bungeni iliashiria kuwa kuna watu wengine wanaoangaliwa ili waweze kuchukua jukumu la kufufua mgodi huo ili hatimaye uweze kuchangia katika kuzalisha nishati ya umeme nchini. Tatizo ni kuwa, wakati anazungumza Bungeni Waziri Yona alijua kabisa watu hao wengine ni kina nani na kwa kweli hakukuwa na juhudi zozote zile za kutafuta mbia au wabwia wengine.
Tunachofahamu kwa uhakika sasa hivi ni kuwa wakati anazungumza Bungeni kuwakilisha makadirio hayo Bw. Yona alikuwa anafahamu kuwa yeye na Rais wake walikuwa mbioni kuingia katika ubia wa kuunda kampuni ya Tanpower Resources mwishoni mwa mwaka 2004 ambayo miezi sita baadaye (mwaka mmoja baada ya hotuba ya Yona Bungeni) ikajinafasi kuchukua kampuni ya Kiwira Coal Mine.
Wakurugenzi wa kwanza wa kampuni hiyo walikuwa ni mama Anna Mkapa, Waziri Daniel Yona (Waziri aliyeshughulikia Nishati na Madini), Nicholas Mkapa (mtoto wa Mkapa), Joseph Mbuna (Baba Mkwe wa Niko), na Evans Mapundi. Katikati ya mwaka 2005 timu ya watu hawa wawili wakaingia katika ununuzi wa hisa za Kiwira Coal Mine na kuchukua asilimia 85 na kuiachia serikali (ambayo wao ndio watendaji waandamizi wa serikali hiyo kwenye Nishati) asilimia 15 tu. Kwa mtindo wa kutoa mkono huu na kuchukua kwa mkono mwingine, wakaweza kujipatia Kiwira.
Mwaka 2006 Machi, Serikali ya Rais Kikwete, ambayo ilichaguliwa kwa asilimia kubwa kuiamsha Tanzania kwa ahadi ya kutofanya mambo yale yale na kuanza kufanya mambo kwa kasi mpya, ari mpya na nguvu mpya huku ikijua dili hili ikaamua kuingia mkataba na kampuni ya kina Mkapa na Yona. Mkataba huo ambao kwa hela ya madafu unagharimu zaidi ya Bilioni 300 gharama yake inafanya ununuzi wa rada na mkataba wa Richmond kuwa ni mtoto! Inasikitisha kuona kuwa serikali iliyoahidi kuwa itapitia mikataba na kuhakikisha kuwa Taifa haliingii kwenye mikataba mibovu tena ndiyo imeliingiza Taifa kwenye mkataba mbovu kama wa Kiwira tena kiujanjaujanja kiasi kwamba hatukuambiwa wakati ule kuwa kampuni ya Kiwira ni ya kina Mkapa na Yona.
Kinachosikitisha zaidi ni kuwa hakuna mbunge wa CCM ambaye amekuwa na ujasiri wa kuhoji biashara hiyo na mkataba huo na kuwaachia jambo hilo wapinzani kana kwamba kuuzwa Kiwira kutawaathiri wapinzani tu. Sijui wako wapi wabunge wa Mkoa wa Mbeya ambao mgodi huu upo? Ni nani anatetea maslahi ya wananchi wa Ileje na Kyela? Leo hii tuna matatizo na Tanesco hadi Mkurugenzi wake anataka kujiuzulu kwa sababu ya mikataba mibovu ya nishati iliyosokomezwa kwenye koo la lake. Leo hii wanaundia tume suala la Richmond lakini wanakwepa hata kutamka Kiwira kwa sababu tu Rais Mstaafu anahusika. Woga huu wa uongoza, hofu hii ya kitoto, na mtazamo huu finyu wa kiuwajibikaji ndio kiini cha matatizo tuliyonayo kwenye mikataba hii ya nishati na madini.
Kuna maswali ambayo yana budi kujibiwa kuhusu suala hili zima na hatua muafaka kuchukuliwa. Swali la kwanza na la msingi ni kuwa PSRC iwaeleze Watanzania kuwa ilikuwaje kampuni ya Tanpower Resources kununua hisa za Kiwira na isiwe kampuni nyingine? Kama kulikuwa na tenda yoyote ile iliyotolewa ilitolewa lini na masharti yake yalikuwaje? Pia tunahitaji kuambiwa ilikuwaje Waziri aliyeko madarakani ajiundie kampuni na halafu kampuni hiyo hiyo ipate tenda kubwa toka serikalini? Je, hisa za Kiwira ziliuzwa kwa bei gani na kampuni ya Tanpower Resources ililipa kiasi gani na pesa zake zilitoka wapi? Kuna habari kuwa Rais Mkapa na Waziri wake walijipatia kampuni ya Kiwira bila kulipa hata senti moja na wakiitwa wezi watakataa? Iweje mtu achukue mali ya umma kinyemela huku anajikinga kwa kinga ya Urais?
Ndugu zangu kuna wakati siyo tu tuwakatalie watawala wetu bali pia tuwaoneshe kuwa hatuko tayari kuendelea kuburuzwa na kufanywa wajinga katika nchi yetu. Haiwezekani kikundi cha watu wachache kijiamulie kuwa kina uwezo wa kufanya lolote, wakati wowote, na kwa namna yoyote bila ya kuhojiwa na mtu yeyote yule. Ni lazima watanzania kupitia wawakilishi wao wawahoji kina Yona ili ukweli kuhusu Kiwira ujulikane.
Tusiendelee kuwaonea haya viongozi wanaotumia nafasi zao vibaya ambao kwa kiburi chao hawataki kuzungumzia tuhuma zinazowakabili. Kitendo cha Mkapa na Yona kujichukulia Kiwira kinyemela ni kitendo cha wizi wa mchana kweupe. Ni sawa na kitendo cha Mwenyekiti wa Kijiji kuiba kuku wa wanakijiji wenzake halafu akajitengenezea yeye mwenyewe banda kubwa ambako kuku wale wa wizi wanataga mayai ambayo atawauzia wanakijiji wale kwa bei ya juu. Hakuna kitu ambacho kinaweza kusemwa kuhusu Kiwira ambacho kinabeba mantiki.
Ni kwa sababu hiyo basi wakati umefika wa kiongozi kuonesha umakini na uthabiti wa vitendo. Wiki karibu mbili zilizopita maamuzi mawili yalifanyika. Bunge la Muungano liliamua kuunda Kamati Teule ya kuangalia mazingira yote yaliyosababisha Taifa kuingia mkataba wa Richmond, tume inayoongozwa na Dr. Harrison Mwakyembe. Wakati huo huo Rais wa Jamhuri ya Muungano aliunda Kamati yake ya kupitia mikataba mikubwa na sheria ya Madini. Maamuzi hayo ambayo yameonekana yamekuja wakati muafaka ni maamuzi ambayo yalikuwa yanasubiriwa kwa hamu na Watanzania.
Licha ya kuwa Kamati ya Rais haina nguvu kubwa kama ile ya Bunge, ni matumaini ya Watanzania wengi kuwa endapo itabadilishwa na kufanywa Tume ya Rais au itatenganishiwa majukumu basi kuna makubwa ambayo yanaweza kufanyika. Kati ya mikataba mikubwa ambayo Kamati hiyo haina budi kuipitia na mazingira yake ni mkataba huu wa Kiwira na kuangalia ilikuwaje kina Mkapa na Yona wajipatie mkataba wa mabilioni ya shilingi wakitumia ofisi zao kwa kisingizio cha ujasiriamali. Vinginevyo, umefika wakati wa Rais Kikwete kwa kutumia mamlaka aliyonayo Kikatiba kuingilia kati na kuwanyanganya wajanja hawa kampuni hiyo na kuirudisha mikononi mwa PSRC ili muwekezaji mwingine au mbia mwingine ajitokeze.
Inapotokea mtu amekwapua kitu na ameanza kukitumia kama cha kwake basi hatuhalalishi na kusema tumuonee haya kwa vile tu kinapendeza mikononi mwake. Wakati mwingine inabidi kitu hicho anyanganywe kwani amejipatia kwa njia isiyo halali au ya udanganyifu.
Rais Mkapa na Daniel Yona pamoja na familia zao na washirika wao wa Tanpower Resources wamejipatia mgodi wa Kiwira kinyemela, wametumia nafasi zao vibaya na wamewarubuni wananchi wa Taifa hili na wakati umefika walipe kwa makosa hayo. Katika Taifa letu na ijulikane sasa na milele kuwa hakuna mtu aliye juu ya mwingine hata kama ana bendera mia zina pepea; ni lazima watambua kuwa hakuna kiongozi ambaye yuko juu ya sheria hata kama anajisikia hivyo; na ya kuwa hakuna Mtanzania mwingine ambaye kutokana na nafasi yake anaamini kuwa anastahili au ana haki zaidi ya Mtanzania mwingine kwa sababu tu ana nafasi fulani! Tunawakatilia watawala wetu uwezo huo, tunawakatilia watawala wetu haki hiyo, na ndiyo! tunawakatalia watawala wetu nafasi hiyo. Kiwira irudishwe kwa wananchi, Mkapa na Yona wanyanganywe ili liwe fundisho kwa viongozi wengine walafi na wenye uroho wa mali ya umma na wanaotumia madaraka yao vibaya. Kufa kwa Nyerere kisiwe kisingizio cha watu wachache kujifanya miungu watu!
Muwanyanganye sasa ama sivyo watanyanganywa siku moja wakiwa na pingu kizimbani. Ni lazima turudishe nidhamu ya utumishi wa umma kwani kuendelea kuwafumbia macho watawala kama kina Mkapa na Yona ni kukaribisha uporaji wa mali ya umma na ni kuwapa kibali cha ufisadi. Hata kama hawataki kusema sasa na wakae kimya lakini Kiwira itolewe midomoni mwao kama tonge la ugali kabla hawajaanza kutafuna na kumeza fedha za wananchi. Ama zao ama zetu, Mkapa na Yona rudisheni mali zetu. Vinginevyo, mtanyanganywa na kuachwa na roho zenye kutu. Na viongozi wanaoogopa kuwachukulia hatua watu hawa na wenyewe watambue siku moja na wao watanyanganywa madaraka hayo na waliowalinda na wenyewe watalipa uzembe huo wa kiuongozi.