Haya unipata hiyo wana JF ndo weshaanza kuendeleza ufisadi wao; kweli mchimba mgodi makaa ya mawe analipwa Shs 48,000 kwa mwezi halafu tena unamdhulumu kwa kutokumlipa??
Mungu atusaidie
Mgodi wa Kiwira kunafuka moshi
na felix mwakyembe, mbeya
Mtanzania Jan 22, 2008
UHUSIANO baina ya uongozi wa Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira mkoani Mbeya na jamii inayouzunguka pamoja na wafanyakazi wake unaonyesha wazi si mzuri, bali umetawaliwa na chuki na uhasama.
Hali hiyo ilijidhihirisha mwishoni mwa wiki, katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na Kamati ya Rais inayopitia sekta ya madini nchini, ambako wananchi na wafanyakazi walimshutumu hadharani Meneja Mkuu wa mgodi huo, Adam Abdu, kwa ufanisi duni wa mgodi na wafanyakazi kutolipwa haki zao.
Mchungaji Israel Mwakisabwe ni miongoani mwa wananchi ambao walijitokeza kueleza hali hiyo mbele ya wajumbe wa Kamati hiyo ya Rais, ambako alisema Meneja Mkuu huyo, ndiye kiini cha chuki na uhasama uliopo kati ya wananchi, wafanyakazi kwa upande mwingine dhidi ya uongozi wa mgodi huo, pamoja na wawekezaji wake kwa ujumla.
Wananchi na wafanyakazi wa Kiwira Coal Mine hawajakombolewa, wanahitaji ukombozi, kwanza huyu Meneja Mkuu ana lugha chafu, husikika akisema wazi kwamba hao Wanyakyusa waache tu, wajinga, alisema Mchungaji Mwakisambwe.
Madai ya wananchi hao yanalingana na yale ya wafanyakazi wa mgodi huo yaliyowasilishwa kwenye Kamati hiyo kwa maandishi, yakionyesha madai yao ya zaidi ya Sh bilioni 47 pamoja na mishahara duni. Kima cha chini cha mshahara mgodini hapo ni Sh 48,000.
Wafanyakazi wa mgodi huo walidai kuwa pamoja na Serikali kutangaza kima cha chini cha Sh 350,000 kwa wafanyakazi wa migodini, uongozi wa mgodi huo umekataa kulipa kiwango hicho na kutishia kufunga mgodi. Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Iddi Simba, alilazimika kumwita tena kiongozi wa Chama cha Wafanyakazi aliyefahamika kwa jina la Kibona, kusoma taarifa yao mbele ya mkutano huo, ili madai yaliyomo yathibitishwe na wafanyakazi wote na wananchi, baada ya kusomwa wote walikubaliana nayo.
Madai mengine yaliyotolewa na wananchi wa vijiji vinavyouzunguka mgodi huo ni kutonufaika kwao na uwepo wa mgodi huo, wakitoa mfano wa huduma za jamii kama vile kukosa umeme, japokuwa unazalishwa kwenye mgodi huo, na huduma nyingine za kijamii kama vile elimu, afya na maji.
Ilielezwa bayana kwenye mkutano huo uliohudhuriwa vile vile na uongozi na mwekezaji wa mgodi huo, kuwa miongozi mwa wafanyakazi 600 wa mgodini hapo, ni 10 tu ndio walioajiriwa, wanaobaki ni vibarua wanaojaza mikataba ya mwezi mmoja mmoja.
Awali Mkurugenzi wa Mgodi huo, Evans Mapundi, aliwaeleza wajumbe wa Kamati hiyo ya Rais kuwa Mgodi huo wa Kiwira, ni mradi wa wazalendo wenye shughuli kuu tatu ambazo ni uchimbaji mkaa, uzalishaji umeme na usambazaji umeme kuingiza kwenye mfumo wa taifa wa TANESCO.
Alisema kukamilika kwa mradi wa uzalishaji umeme kutawezesha kupatikana kwa megawatt 200 zaidi za umeme toka mgodini hapo, ambapo awamu ya kwanza wataingiza TANESCO megawatt 50 ifikapo mwezi Aprili mwaka huu na zinazobaki 150 zitaingizwa Septemba mwakani.
Wajumbe wengine katika kamati hiyo ni pamoja na Maria Kejo, Mugisha Kamugisha, Salome Makange, Dk. Harrison Mwakyembe, Ezekiel Maige, Edward Kihundwa na Katibu wa Kamati, Mathias Kabunduguru.
Jana asubuhi wajumbe wa kamati hiyo waliondoka mkoani hapa kuelekea Mchuchuma katika wilaya ya Ludewa, mkoani Iringa.