Elimu; Makabwela wameanza kuhoji
Na Maggid Mjengwa,
KUNA kisa cha mwandishi mmoja wa habari wa Kimagharibi aliyemwuliza swali gumu mkalimani wake wa Kihindi. Aliuliza wakati akiwaangalia watoto wa Kihindi waliokuwa kwenye jua kali wakihenyeka kupasua mawe.
"Je, ungeweza kufikiri kuwa mpasua mawe, ukae juani na kufanya kazi ngumu kama hii kama wafanyavyo watoto hawa?
-Ndio, kama ningekuwa mtu wa tabaka la watoto hawa? Alijibu Mkalimani yule.
Mzungu yule akabaini, kuwa Mkalimani wake hakuelewa swali lake. Akazidi kuuliza. "Lakini, jaribu kufikiri, kwamba wewe ndiye mmoja wa watoto hawa na unajisikiaje kuwa kama wao?
- Ndio, lakini kama ninavyokwambia, mimi si mtu wa tabaka la watu hawa.
Mzungu na Mhindi yule walikuwa wakipishana kifikra kama magari mawili yanavyopishana barabarani. Mwandishi yule wa Kimagharibi hakuelewa, kuwa Watu wa India wamegawanyika katika tabaka maalum, wenyewe wanaita kasti. Kwa Mhindi mfumo wa kasti ni kitu kilichoumbwa na Mungu wanayemwamini. Hakuna anayeweza kuubadilisha. Mhindi haelewi, kuwa mfumo huu wa Kasti ni kitu kilichoundwa na mwanadamu, na ambacho kinaweza kubadilishwa na mwanadamu huyo huyo.
Katika jamii yetu tumeanza kuona dalili za wananchi kuanza kuamka na kuhoji juu ya masuala mbali mbali yenye kuwahusu. Moja ya masuala hayo ni hili juu ya ubora wa elimu itolewayo kwa watoto wao. Tumewasikia wazazi kule Serengeti wakihoji; iweje watoto wao wafaulu darasa la saba ilihali hawajui kusoma na kuandika?! Inadaiwa, kuwa watoto hao wamefaulishwa na kwa kusaidiwa na uongozi wa shule zao kwenye kunakiri majibu ya mitihani. Na kwamba hali hiyo imeanza kuwa ya kawaida katika shule zetu.
Haya ni madai makubwa, kama hali ni hivi kweli, basi, ni kashfa kubwa. Ni aibu kubwa kwa taifa. Huku ni kufaulisha wanafunzi kwenye maana ya kulifelisha taifa. Tumewasikia pia wanafunzi wa chuo kimoja kikuu wakigoma kuingia kwenye vyumba vya mitihani kwa vile chuo hakikutimiza yale yote yanayotakiwa kufanywa kabla ya mtihani wao wa mwisho. Kinachoonekana hapa ni kwa watu kuanza kuhoji mfumo wetu wa elimu, wanataka mabadiliko ya kimfumo. Na hilo la mwisho hawawezi kusubiri kudra za mwenyezi Mungu, limo ndani ya uwezo wao, wana lazima ya kulifanya.
Na hakika, tofauti ya zamani na sasa katika mfumo wetu wa elimu na namna ya kuyashughulikia na kuyatatua matatizo yetu ya kielimu ni namna viongozi wetu wanavyohusika na matatizo yenyewe.
Zamani, Mawaziri wakikaa kwenye baraza la mawaziri kuzungumzia matatizo ya elimu; iwe kero za walimu, matatizo ya wanafunzi, upungufu wa vifaa vya kufundishia na mengineyo, kimsingi walikuwa wanazungumzia shule wanazosoma watoto wao pia. Shule wanazofundisha wake zao; iwe Shule ya Msingi Kinondoni, Temeke au Ilala. Iwe shule ya sekondari Kibasila, Azania au Tambaza.
Lakini, leo ikitokea kwenye Baraza la Mawaziri likazungumzwa tatizo la elimu, kisha atokee Waziri atakayetolea mfano shule ya msingi au sekondari ya Kijitonyama au Sinza anakosoma mwanawe, basi, hakika mawaziri wenzake watamtolea macho kwa kumshangaa.
Tofauti na zamani, siku hizi watoto wa Mawaziri na viongozi wetu waandamizi , kuanzia shule za awali hadi Chuo Kikuu, wanasoma kwenye shule zenye hadhi nyingine kabisa tofauti na zile wanazosoma watoto wa Makabwela wanaowaongoza.
Tujiulize; hivi kweli waziri angelala usingizi huku akifahamu, kuwa shule ya sekondari ya kata anayosoma mwanawe ina walimu wawili, haina maktaba, chumba cha maabara na mengineyo? Je, waziri huyu angepata usingizi kama mtoto wake angesona kwenye sekondari ya kata mbali na kijiji alichozaliwa na isiyo na mabweni. Kwamba mtoto wake wa miaka 16 angeishi kwenye chumba cha kupanga kijijini bila ndugu na jamaa wenye kumhusu?
Baadhi ya watoto wa Waheshimiwa hawa wanaosoma kwenye shule za kimataifa za ndani na nje ya nchi, ndio watakaokuja kuwaongoza Makabwela wa nchi hii. Ndio hawa, watakapoulizwa na wanahabari wa kimagharibi; wangejisikiaje kama wangekaa kwenye darasa lenye wanafunzi mia moja na mwalimu mmoja? Kama mkalimani yule wa Kihindi, jibu lako litakuwa jambo hilo haliwezekani kwa vile wao sio watu wa tabaka la Makabwela. Na zaidi ya hapo, watakaojibu swali hilo watakuwa ni watu ambao mfumo wetu wa elimu wameusikia tu, hawajaupitia.
Hakika ni makosa kufikiri, kuwa hali tuliyo nayo ni ya kimfumo, kuwa haiwezi kubadilika. Kule Ujerumani kuna mwanafalsafa aliiyeitwa Jurgen Harbermas, katika maandiko yake, Harbemas amezungumzia dhana nzima ya maarifa ya ukombozi. Kuwakomboa wanadamu kutoka kwenye fikra na mifumo yenye kuwafanya kuwa katika hali ya ufungwa. Hali ya utumwa. Fikra zenye kuwafanya waaminini kuwa hali walizo nazo zitabaki kuwa hivyo daima milele.
Katika kundi la akina Harbermas nawaingiza wanafalsafa Julius Nyerere, Kwame Nkrumah, Nelson Mandela, Frantz Fanon na wengineo. Hawa ni wana wa bara hili, wamepigania ukombozi wa Mwafrika. Katika utumishi wao kwa bara hili, kupitia kauli na matendo yao, wamejenga misingi ya maarifa ya kuwakomboa Waafrika, wanyonge walio wengi. Kuwaenzi wanamapinduzi hawa, ni kupigania yale waliyoyapigania, kwa vitendo.
Ili kuibadili hali tuliyo nayo ni vema tuanze sasa kudadisi na kuhoji. Tanze sasa kuhimiza kujenga mazingira ya kuwa na shule zenye kuwafunza watoto wetu kudadisi na kuhoji; kuuliza swali la "kwanini" bila hofu ya kuadhibiwa.
Fikra tofauti na huru ni jambo la heri kwa jamii yeyote yenye kutaka kupiga hatua za dhati za maendeleo. Jamii isiyorutubishwa na fikra tofauti na huru, daima itakuwa na ustawi duni.
Tukumbuke, binadamu ni kiumbe mwenye kufikiri, awe tajiri au masikini. Tujipe nafasi ya kufikiri, mara nyingine sio tu tuishie kwenye kufikiri, bali tufikiri kwa bidii zaidi. Na kwa hili la elimu, tuna lazima ya kuutafuta ukweli mzima wenye kutujibu ni kwa nini hali yetu ya elimu inazidi kuwa mbaya? Inahusu watoto wetu hata kama hawasomi shule za Makabwela, inahusu mustakabali wa nchi yetu.
Source: RAI