Kiwango cha Elimu Tanzania: Nani alaumiwe?

nmkenda

Member
Mar 6, 2006
12
60
Kama wazee wanapima vijana kwa kipimo walichopimiwa wao then kiwango kimeshuka, kama vijana wanaopata elimu wanaona wenyewe kuwa inawasaidia then hakijashuka.

Japo si mzee wala kijana najua kuwa watu wanakuwa wabinafsi zaidi kadiri siku zinavyoendelea. Asipotokea mtu wa kureverse hii (hopefully JK) tunaishia pabaya very soon.

Tatizo la elimu kama lipo kwa nini halishughulikiwi? Ina maana hakuna wataalamu? Mbona kila siku wanasomeshwa?

Tunasomesha wataalamu wengi sana hatutakiwi kuwa na sector isiyokuwa na wataalamu WA KU-SOLVE PROBLEMS. Sio kuandika mada.

Ni aibu kuzuzungumzia hili jambo miaka nenda rudi.

Let us do it, find a solution and stick to it.
 
Nionavyo mimi kiwango cha Elimu kimeshuka hasa ukizingatia sifa za walimu waliopo , miundo mbinu tuliyonayo na utekelezaji wa mipango tuipangayo kuhusu Elimu.

Kama vigezo vya kupanda kwa Elimu ni idadi ya wanaojiunga katika ngazi furani ya elimu basi Elimu ya Tanzania iko juu mno kulinganishana huko nyuma.

Angalia matokeo ya kidato cha nne kila mwaka tumekuwa na karibu asilimia 80 ya wanasemwa wamefaulu kuwa na daraja la nne.Daraja ambalo hata afanyeje labda ataenda ualimu kama ambavyo tumefanya miaka ya 90 na mwanzoni mwa mwaka 2000.

Madarasa yapo watoto hawasomi kwa kukosa walimu hiyo Elimu itapandaje, ili tendo la kujifunza liweze kufanyika ni lazima mwalimu awepo na mwanafunzi pamoja na mabo mengine kadha wa kadha wataalamu wa elimu wanaijua.

Tutaendelea siku nyingine.

Asante.
 
Elimu ya Tanzania haijashuka; imepanuka tu. Katika kupanuka huku, ziko shule nyingine ambazo hazifikii kiwango, na ziko shule nyingi zinapita sana viwango vilivyokuwepo zamani.

Hii leo, kufaulu kumeongezeka, sio kupungua. Mtoto anayemaliza kidato cha 4 katika moja ya shule 100 bora za leo ana elimu nzuri zaidi kuliko mtoto aliyemaliza kidato cha 4 katika shule 10 bora za miaka 15 iliyopita.

Watoto wanaohitimu masomo katika shule kama Mariam, Mzumbe, St. Joseph, Ilbouru, Maria Gorreti nk. wameelimika zaidi kabisa kuliko watoto waliohitimu miaka 15 ya nyuma.

Elimu ya Tanzania iko katika kipindi cha kupanda na kuongezeka kimapinduzi.

Augustine Moshi
 
Kabla ya kutoa hukumu kwamba elimu yetu imeshuka au kupanda, inabidi kwanza mtuelimishe imeshuka au kupanda kutoka wapi? Yaani kabla ya sasa tulikuwa wapi na sasa tupo wapi, hapo tutaweza kupima. Na wasiwasi bila kuweka vigezo thabiti tutaongozwa na hisia zaidi kuliko ukweli wa mambo.
 
Ni kweli wengi wetu hatuna takwimu za kufanyia utafiti juu ya kupanda au kushuka kwa elimu nchini Tanzania. Tunatumia hisia, na hisia zinatosha kutoa dira kiasi fulani. Maamuzi mengi yanayofanywa na waajiri yanategemea tu hisia vile vile. Kwa mfano, waaajiri wengi Tanzania kwa sasa wana hisia kwamba mtoto aliyesoma Kenya, Uganda au SA anakuwa ameelimika vizuri zaidi ya aliyesoma Tanzania.

Tunawalinganisha watoto waliomaliza kidato cha 4 mwaka 1990 na wale wanaomaliza sasa. Tunaweza kuchukua shule moja na kulinganisha elimu (maarifa + good formation) waliopata watoto hapo 1990 na sasa, au tukachukua ujumla wa Tanzania na kufanya mlinganisho kama huo. Tatizo la kuchukua shule moja ni namna ya kuichagua. Ukichagua Ilboru kwa mfano, utakuta mhitimu (average) wa kiadato cha 4 pale mwaka huu ana elimu (again, elimu hapa ni maarifa +good formation) mara mbili au tatu ya mhitimu wa 1990.

Huenda ziko shule ambazo elimu yake imeshuka kati ya 1990 na sasa, lakini zitakuwa chache, na kwa kweli siwezi kutoa hata mfano mmoja.

Kwa hisia zangu, na kwa kuangalia takwimu za kufaulu, shule 100 bora za 2006 zinatoa elimu ya kiwango cha juu kuliko hata shule 10 bora za 1990. Tuwashukuru basi Mkapa na Mungai kwa kulivalia njuga swala la elimu.

Augustine Moshi
 
Ndugu Mwanasiasa,

Ulitaka kipimo cha kupanda au kushuka kwa elimu katika kipindi cha miaka 10 liyopita. Naweka hapa chini ripoti iliyotokea kwenye gazeti la Majira la Julai 6, 2005. Linatoa takwimu ulizohitaji.
=============================



WIZARA ya Elimu na Utamaduni, imejivunia mafanikio makubwa iliyoyapata katika kipindi cha miaka 10 ya utawala wa Rais Benjamin Mkapa, yakiwemo ya utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu.

Hayo yalisemwa bungeni mjini hapa jana na Waziri wa Elimu na Utamaduni, Bw. Joseph Mungai alipokuwa akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2005/06 kwa Wizara ya Elimu na Utamaduni.

Waziri Mungai alisema katika kipindi hicho cha miaka 10, Serikali imeweza kurekebisha mfumo wa uchumi na hivyo kutimiza masharti ya nchi tajiri kuweza kuifutia madeni na kuikopesha na kuipa misaada mingine ya maendeleo hatua iliyofanikisha kuanzisha Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES).

Alisema chini ya mafanikio hayo, shule za msingi zimeongezeka kutoka shule 10,927 mwaka 1995 hadi kufikia shule 14,257 mwaka 2005 ikiwa ni ongezeko la asilimia 30, wakati shule za sekondari zimeongezeka kwa asilimia 195 kutoka shule 595 mwaka 1995 hadi shule 1,755 mwaka 2005, zikiwemo 1,206 za Serikali na 549 za binafsi sawa na asilimia 31.

Waziri Mungai alisema wanafunzi wa shule za sekondari katika kidato cha kwanza hadi cha sita, wameongezeka mara dufu kutoka wanafunzi 196,375 mwaka 1995 hadi kufikia wanafunzi 524,325 mwaka 2005.

Alisema hata hivyo, chini ya utekelezaji wa mpango wa MMES, huu ukiwa ni mwaka wa pili, idadi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne itaongezeka na kufikia 2,000,000, sawa na asilimia 50 ya rika hilo na kidato cha tano na cha sita itaongezeka hadi kufikia wanafunzi 250,000 sawa na asilimia 25 ya rika hilo ifikapo mwaka 2010.

Alisema Wizara ya Elimu na Utamaduni, imeanzisha mtaala mpya ambamo masomo ya sekondari yamepunguzwa kutoka 13 hadi 8 kwa kuunganisha masomo ya mchepuo na ya kawaida, na kwamba mtaala huo utampatia mwanafunzi elimu bora zaidi ya sekondari yenye msingi imara wa kuendelea na elimu ya juu au kujifunza ufundi au kujiajiri.

Akizungumzia mafanikio ya elimu ya ualimu, Waziri Mungai, alisema walimu tarajali katika vyuo vya ualimu wameongezeka kutoka 12,417 mwaka 1995 hadi 29,952 mwaka 2004, ambalo ni ongezeko la walimu 17,535 ikiwa ni sawa na asilimia 141.

Alisema vyuo vya ualimu vimeongezeka kutoka 34 mwaka 1995 hadi kufikia vyuo 52 mwaka 2005, vikiwemo vyuo 18 vya Serikali, sawa na asilimia 35.

Kuanzia mwaka huu shule ya sekondari ya Mkwawa na Chuo cha Ualimu cha Dar es Salaam, vinakuwa vyuo vishirikishi vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Aidha Waziri Mungai alisema Chuo cha Ualimu cha Mtwara kitakuwa Chuo cha Elimu Ambata cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kitaanza kutoa Stashahada ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Pia mafunzo ya Kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEKNOHAMA), yanaanzishwa katika vyuo vyote vya ualimu na litakuwa somo la lazima kwa kila mwalimu tarajali.

Kwa upande wa ubora wa elimu, Waziri Mungai alisema kumekuwepo na ongezeko la ubora wa elimu itolewayo katika shule kwa vipimo vya mitihani ya Baraza la Mitihani Tanzania. Asilimia ya kufaulu darasa la saba imeongezeka kutoka 15 mwaka 1995 hadi 49 mwaka 2004.

Alisema asilimia ya kufaulu kidato cha Nne katika daraja la I-III imeongezeka kutoka 25 mwaka 1995 hadi 39 mwaka 2004 kwa shule zote kwa pamoja na asilimia 53 kwa sekondari za Serikali pekee.

Asilimia ya kufaulu Kidato cha Sita katika Daraja la I-III imeongezeka kutoka 71 mwaka 1995 hadi 94 mwaka 2005.

Katika hatua nyingine, Waziri Mungai ameliomba Bunge kupitisha makadirio ya matumizi ya sh. 175,434,506,800 ili kuwezesha Wizara ya Elimu na Utamaduni kutekeleza mipango yake ya mwaka 2005/06.
 
Ndugu Augustine,

Unaposema kiwango kimeongezeka inabidi tuangalie matunda mazuri yenye faida usihesabu hata yale yaliyooza.

Hizi takwimu za waziri zinapingana na ukweli ambao wewe mwenyewe husisitiza kwamba wanafunzi wengi siku hizi humaliza kidato cha nne wakiwa watupu hata kunyoosha lugha iwe kiingereza ama kiswahili hawawezi... sii ktk kusoma wala kuandika.

Haya, hilo ongezeko la shule za msingi kutoka shule 10,927 mwaka 1995 hadi kufikia shule 14,257 mwaka 2005 limechangia pia ongezeko la wananfunzi mara tatu ya mwaka 1995 ambao walikuwa wakisoma shule zote hizi kwa kulipia. Miaka ya 1972 hadi 1982 kulikuwa na wanafunzi wengi shule za msingi kuliko mwaka 1995. Kwa hiyo ongezeko la shule ni fidia ya mapungufu ya elimu ktk miaka kumi ya kwanza ya Mkapa. Vilevile hata hivyo ongezeko la shule za secondary bado matunda yake ni yaleyale kwani asilimia ya wanafunzi kuingia shule hizo ni chache kulingana na hesabu ya wanafunzi waliomaliza mwaka huo.

Hapa nikiwa na maana lengo ni kuwepo na wahitimu wengi kuliko washindwa. Ikiwa mwaka 1995 wanafaunzi 200,00 tu ndio waliingia shule ya msingi huwezi kupima mafanikio ya kuwepo wanafunzi millioni 2 mwaka 2000 hali kati ya hao millioni mbili ni robo yake tu wameweza kwenda secondary sawasawa na nafasi zilizokuwepo mwaka 1995 kwa watoto laki mbili.

Kisha kumbuka hapo mwisho Mungai katoa estimate tu kwamba ifikapo mwaka 2010 kutakuwa na ongezeko la sijui 50% na 25 bila kutupa ongezeko la washindwa kuingia shule hizo.

Mshikaji unapokuwa bachelor nadhani hupika chakula kwa kiwango cha kukutosha wewe na upimaji wa shibe lazima uwe kwa mtu mmoja, lakini huwezi kuhesabu mafanikio kwa kupika chakula kingi wakati hali halisi inasema umepika chakula hicho kwa sababu ya ongezeko la wageni...La muhimu ni kupima malengo ya ongezeko lenyewe kama watu wote wamekula na kushiba. Ikiwa utapima mafanikio kwa sababu tu umeweza kupika Ugali mwingi jambo ambalo hujawahi kulifanya basi subiri ukija pata msiba, utawaacha wengi njaa hali ukijisifia.
 
Mkandara,

Sijasema watoto wanaomaliza kidato cha 4 hawajui lolote. Don't put words into my mouth.

Takwimu zinaonyesha elimu yetu imeongezeka ubora na wingi. Hizo takwimu za NECTA za kuongezeka kufaulu kidato cha 4 ni za ubora. Hizo za maongezeko maradufu ya idadi ya wanafunzi ni za wingi. Statistically speaking, our education has grown, by leaps and bounds, qualitatively and quantitatively.

Augustine Moshi
 
Augustine,

Mbona ndugu yangu mgumu kuelewa?

Mara ngapi umesisitiza kuhusu kujua kusoma na kuandika kiingereza?.. Hilo neno hawajui lolote ni lugha umeitumia mwenyewe lakini kwa msomaji yeyote unaposema mtu hajui kusoma wala kuandika ina maana moja tu!...

Pili, Nimekupa mifano mingi sana kukuonyesha upotofu wa hizo takwimu bado unavuta uradi kumpongeza Mkapa.

Nitarudia tena labda safari hii kwa kuomba unieleweshe wapi takwimu zinaonyesha UBORA wa hiyo Elimu. Mimi sijaona zaidi ya mifano yangu. Nitarudia tena ukiwa na wanafunzi 10 mwaka jana wameshinda 2 hapa hakuna sifa ya ubora. Na mwaka unaofuatia ukiwa na wanafuzi 30 wakashinda 5 bado hapa hakuna Ubora wa aina yeyote iwe quantative au qualitative. Na sababu ni hii. Ukihesabu ushindi wa watoto toka 2 kwenda 5 kuwa ni ongezeko la qauntitative basi tumelost kwa sababu kuna watoto 25 wameshindwa kwenda mbele! Hii kitakwimu
ni ongezeko kubwa sana toka watoto 8 hadi 25 yaani mara tatu hali watoto 2 kufikia 5 sii mara tatu... na hata kama ingekuwa mara tatu badi kabisa haitupi Quality kwa sababu watoto 5 kati ya 30 ni aibu tupu ikiwa wenzetu majirani wanashinda watoto zaidi ya 10 kwa kila 30. Ati shule zimeongezeka, sijui walimu n.k. yote haya ni sifa ambazo tulimpa Mkapa hali budget yake ilizidi kupungua mwaka hadi mwaka na kutegemea misaada. Yaani hesabu zake zinakwenda hata mifukoni mwa watu wengine ambao wapo nchini kufanya biashara. hali nzuri ya biashara ya shule hakuianzisha yeye ilikuwepo toka Mwinyi na kina Filbert Bey walishtuka long! Sii Mkapa wala Sumaye aliyewashtua wafanya biashara bali policy alizozikuta yeye Mkapa.

Ningependekeza sana sheria ya takwimu hizi itumike kama ile inayotumika nchi za magharibi ya unemployment - hapo watapima kutopkana na wanafunzi waliokuwa tayari kuingia shule toka shule za msingi hadi chuo kikuu na nafasi ngapi wamekosa shule hali wakiwa tayari kwenda mbele.
 
Mkandara, naona unakataa kuelewa.

Mwaka 2000, 19% ya watoto waliokuwa darasa la saba walifaulu mtihani wa kuinga kidato cha kwanza. Mwaka 2005, hio asilimia ya kufaulu mtihani wa kuingia kidato cha kwanza iliongezeka ikakafika 48% . Sasa unataka kusema huko sio kuongezeka kwa ubora wa elimu?

Asilimia ya kufaulu kidato cha nne imekuwa ikiongezeka vile vile. Angalia website ya NECTA.

Augustine MOshi
 
Augustine,

Hiyo hesabu yako ni ya wale watihaniwa yaani waliokaa ktk mtihani, Hapa hakuna hesabu ya wanafunzi wote waliojiandikisha toka darasa la kwanza, kumbuka hawa watoto wote nia yao ni kufika hatta hilo la saba. Kuna asilimia isiyopungua 30 hawakukaa kufanya mitihani ama kumaliza darasa la saba. WHY? Hii ni idadi kubwa kulinagana na hao walioshinda...Je, kuna kati yenu kajaribu kupata ufumbuzi?...hakuna kati yenu anayeweza kujibu isipokuwa HILO SHAURI LAO!
Kwa hiyo jumlisha hesabu hiyo na wale walioshindwa kupata hesabu kamili.

Brother, hawa watoto ni taifa la kesho, viongozi wa kesho na kama hamtafanya utafiti kufahamu wapi wanakwama hata sielewi ubora huo unatoka wapi ikiwa 2002 drop out ilikuwa ndogo zaidi ya mwaka 2005.

Mwisho, Ukitoka darasa la saba ukienda kidato cha nne mchezo ni huohuo! Ukichukua hesabu ya walioanza darasa la kwanza miaka kumi na nne iliyopita na wale waliofaulu mwisho wa kisafari hiki kidogo (Form IV) utakuta hesabu hazipandi!
 
A.Mushi,

Statistically ukiangalia final %, hesabu zinaweza zisiwe na ukweli ndani yake, kwani kwenye statistics kuna vipengele vingi vya kuangalia kujustify maendeleo ya kielimu. Maendeleo yeyote hupimwa kutokana na malengo,viwango(standards), and measurable indicators, statistically valid tests should be done for one to conclude hayo maendeleo kielimu.

Mzee Mushi ukiwa one of the University Lecturers naamini hayo ni mambo mnayofanya kila siku kukicha kwenye research zenu. Just put down those figures zinazotolewa na wizara ya elimu utaona kuwa zina walakini.

Just a simple mfano. Hivi sasa ku-rank performance za shule hawajumuishi seminari tena, wame-categorize. kwa sababu kila mwaka ilionekana kuwa seminari zinakuwa bora kwa performance!! WHY? chunguza utaona ninachozungumzia hapo juu. BUT yet still wizara haifanyi homework yake sawasawa kutoa takwimu zinazoonyesha maendeleo kielimu

next time
 
Elimu; Makabwela wameanza kuhoji

Na Maggid Mjengwa,

KUNA kisa cha mwandishi mmoja wa habari wa Kimagharibi aliyemwuliza swali gumu mkalimani wake wa Kihindi. Aliuliza wakati akiwaangalia watoto wa Kihindi waliokuwa kwenye jua kali wakihenyeka kupasua mawe.

"Je, ungeweza kufikiri kuwa mpasua mawe, ukae juani na kufanya kazi ngumu kama hii kama wafanyavyo watoto hawa?

-Ndio, kama ningekuwa mtu wa tabaka la watoto hawa? Alijibu Mkalimani yule.
Mzungu yule akabaini, kuwa Mkalimani wake hakuelewa swali lake. Akazidi kuuliza. "Lakini, jaribu kufikiri, kwamba wewe ndiye mmoja wa watoto hawa na unajisikiaje kuwa kama wao?
- Ndio, lakini kama ninavyokwambia, mimi si mtu wa tabaka la watu hawa.

Mzungu na Mhindi yule walikuwa wakipishana kifikra kama magari mawili yanavyopishana barabarani. Mwandishi yule wa Kimagharibi hakuelewa, kuwa Watu wa India wamegawanyika katika tabaka maalum, wenyewe wanaita kasti. Kwa Mhindi mfumo wa kasti ni kitu kilichoumbwa na Mungu wanayemwamini. Hakuna anayeweza kuubadilisha. Mhindi haelewi, kuwa mfumo huu wa Kasti ni kitu kilichoundwa na mwanadamu, na ambacho kinaweza kubadilishwa na mwanadamu huyo huyo.

Katika jamii yetu tumeanza kuona dalili za wananchi kuanza kuamka na kuhoji juu ya masuala mbali mbali yenye kuwahusu. Moja ya masuala hayo ni hili juu ya ubora wa elimu itolewayo kwa watoto wao. Tumewasikia wazazi kule Serengeti wakihoji; iweje watoto wao wafaulu darasa la saba ilihali hawajui kusoma na kuandika?! Inadaiwa, kuwa watoto hao wamefaulishwa na kwa kusaidiwa na uongozi wa shule zao kwenye kunakiri majibu ya mitihani. Na kwamba hali hiyo imeanza kuwa ya kawaida katika shule zetu.

Haya ni madai makubwa, kama hali ni hivi kweli, basi, ni kashfa kubwa. Ni aibu kubwa kwa taifa. Huku ni kufaulisha wanafunzi kwenye maana ya kulifelisha taifa. Tumewasikia pia wanafunzi wa chuo kimoja kikuu wakigoma kuingia kwenye vyumba vya mitihani kwa vile chuo hakikutimiza yale yote yanayotakiwa kufanywa kabla ya mtihani wao wa mwisho. Kinachoonekana hapa ni kwa watu kuanza kuhoji mfumo wetu wa elimu, wanataka mabadiliko ya kimfumo. Na hilo la mwisho hawawezi kusubiri kudra za mwenyezi Mungu, limo ndani ya uwezo wao, wana lazima ya kulifanya.

Na hakika, tofauti ya zamani na sasa katika mfumo wetu wa elimu na namna ya kuyashughulikia na kuyatatua matatizo yetu ya kielimu ni namna viongozi wetu wanavyohusika na matatizo yenyewe.
Zamani, Mawaziri wakikaa kwenye baraza la mawaziri kuzungumzia matatizo ya elimu; iwe kero za walimu, matatizo ya wanafunzi, upungufu wa vifaa vya kufundishia na mengineyo, kimsingi walikuwa wanazungumzia shule wanazosoma watoto wao pia. Shule wanazofundisha wake zao; iwe Shule ya Msingi Kinondoni, Temeke au Ilala. Iwe shule ya sekondari Kibasila, Azania au Tambaza.

Lakini, leo ikitokea kwenye Baraza la Mawaziri likazungumzwa tatizo la elimu, kisha atokee Waziri atakayetolea mfano shule ya msingi au sekondari ya Kijitonyama au Sinza anakosoma mwanawe, basi, hakika mawaziri wenzake watamtolea macho kwa kumshangaa.

Tofauti na zamani, siku hizi watoto wa Mawaziri na viongozi wetu waandamizi , kuanzia shule za awali hadi Chuo Kikuu, wanasoma kwenye shule zenye hadhi nyingine kabisa tofauti na zile wanazosoma watoto wa Makabwela wanaowaongoza.

Tujiulize; hivi kweli waziri angelala usingizi huku akifahamu, kuwa shule ya sekondari ya kata anayosoma mwanawe ina walimu wawili, haina maktaba, chumba cha maabara na mengineyo? Je, waziri huyu angepata usingizi kama mtoto wake angesona kwenye sekondari ya kata mbali na kijiji alichozaliwa na isiyo na mabweni. Kwamba mtoto wake wa miaka 16 angeishi kwenye chumba cha kupanga kijijini bila ndugu na jamaa wenye kumhusu?

Baadhi ya watoto wa Waheshimiwa hawa wanaosoma kwenye shule za kimataifa za ndani na nje ya nchi, ndio watakaokuja kuwaongoza Makabwela wa nchi hii. Ndio hawa, watakapoulizwa na wanahabari wa kimagharibi; wangejisikiaje kama wangekaa kwenye darasa lenye wanafunzi mia moja na mwalimu mmoja? Kama mkalimani yule wa Kihindi, jibu lako litakuwa jambo hilo haliwezekani kwa vile wao sio watu wa tabaka la Makabwela. Na zaidi ya hapo, watakaojibu swali hilo watakuwa ni watu ambao mfumo wetu wa elimu wameusikia tu, hawajaupitia.

Hakika ni makosa kufikiri, kuwa hali tuliyo nayo ni ya kimfumo, kuwa haiwezi kubadilika. Kule Ujerumani kuna mwanafalsafa aliiyeitwa Jurgen Harbermas, katika maandiko yake, Harbemas amezungumzia dhana nzima ya maarifa ya ukombozi. Kuwakomboa wanadamu kutoka kwenye fikra na mifumo yenye kuwafanya kuwa katika hali ya ufungwa. Hali ya utumwa. Fikra zenye kuwafanya waaminini kuwa hali walizo nazo zitabaki kuwa hivyo daima milele.

Katika kundi la akina Harbermas nawaingiza wanafalsafa Julius Nyerere, Kwame Nkrumah, Nelson Mandela, Frantz Fanon na wengineo. Hawa ni wana wa bara hili, wamepigania ukombozi wa Mwafrika. Katika utumishi wao kwa bara hili, kupitia kauli na matendo yao, wamejenga misingi ya maarifa ya kuwakomboa Waafrika, wanyonge walio wengi. Kuwaenzi wanamapinduzi hawa, ni kupigania yale waliyoyapigania, kwa vitendo.

Ili kuibadili hali tuliyo nayo ni vema tuanze sasa kudadisi na kuhoji. Tanze sasa kuhimiza kujenga mazingira ya kuwa na shule zenye kuwafunza watoto wetu kudadisi na kuhoji; kuuliza swali la "kwanini" bila hofu ya kuadhibiwa.

Fikra tofauti na huru ni jambo la heri kwa jamii yeyote yenye kutaka kupiga hatua za dhati za maendeleo. Jamii isiyorutubishwa na fikra tofauti na huru, daima itakuwa na ustawi duni.

Tukumbuke, binadamu ni kiumbe mwenye kufikiri, awe tajiri au masikini. Tujipe nafasi ya kufikiri, mara nyingine sio tu tuishie kwenye kufikiri, bali tufikiri kwa bidii zaidi. Na kwa hili la elimu, tuna lazima ya kuutafuta ukweli mzima wenye kutujibu ni kwa nini hali yetu ya elimu inazidi kuwa mbaya? Inahusu watoto wetu hata kama hawasomi shule za Makabwela, inahusu mustakabali wa nchi yetu.


Source: RAI
 
Mjengwa,
Nafahamu kuwa unatumia nafasi hii kutuvuta ktk toviti yako, jambo ambalo sii baya wala halina makosa ila mwenzangu kumbuka kitu kimoja tu. Sii wote wanaopenda kuzunguka huku na huko kutafuta habari na vizuri sana kama ukichapia kidogo kuhusu habari hii.

Nimeisoma habari nzima ktk blog yako na kusema kweli hii habari ni nzito sana! nimependezewa sana na mtazamo wako na ndio ukweli unaojitokeza kwa haraka sana.
Nakuomba tu, Please jaribu kuwa unaziweka hapa habri nzito kama hii ili wachangiaji wapate kuzisoma na kutoa michango yao sehemu zote mbili.
 
i) Ni ni vigezo vya elimu kushuka au kupanda? Kumekuwa na kilio kwa muda sasa kuwa elimu yetu imeshuka sana; nimkewa najiuliza na nakuulizani nanyi pia, imeshuka kutoka wapi?

Naona kile kilio cha wananchi wa Serengeti kama kilivyonukuliwa katika makala ya Maggid kimeanza kutupa mwanga.Kwamba wazazi wamekataa watoto wao waende shule wakati hata kusoma na kuandika hawajui. Kumbe kigezo kimoja hapa cha chini kabisa ni kujua kusoma na kuandika . Je, katika hili tulikuwaje huku nyuma na sasa tupo wapi. Nafikiri kuna waja wenzetu kina Maggid katika makala zao zijazo kuainisha vizuri zaidi katika haya majambo.

ii) Je, Wizara ya Elimu imechukua hatua gani baadhi ya kupewa ushahidi na wazazi kuwa watoto wao waliibiwa mitihani? Hivi kweli ni sawa wizara ikae kimya tu katika jambo zito la namna hii?

iii) Kuna hoja kubwa zaidi. Kwamba watoto wa viongozi wetu hawasomi katika shule za serikali. Japokuwa Maggid hakutoa takwimu katika kushibisha hoja yake, napenda niamini hivyo. Na tunaweza kujumuisha na kusema kuwa wakubwa hawatumii huduma za jamii za serikali wanayoiongoza.Je, hili nalo ni sawa? Ni haki kweli viongozi wetu kukataa kutumia mahospitali na shule zetu halafu wakati huohuo tuwatarajie kuboresha hizi huduma? Inakuja kweli hii?

Wakati umefika tuanze kuhoji uhalali wa viongozi wetu kutokutumia huduma za jamii za serikali na wakati huohuo wakidai kuwa huduma hizo sasa zimeboreka na zimepata mafanikio makubwa.

Kama alivyosema Maggid, akili mkichwa!
 
Hivi system yetu ya elimu ya chini (Primary and Secondary Level) imeshafanyiwa marekebisho yoyote miaka ya hivi karibuni? Ninauliza kwa sababu kuna conditions (kama bado zipo) zinawaumiza wanafunzi kwa kuwakatisha tamaa na kuendelea na elimu.

Mfano, condition ya kuzuia kutofanya mtiani wa Form VI mpaka mwanafunzi awe amepata at least 3 credits (minimum C’s) imepitwa na wakati. Kwa maoni yangu, ikiwa Form VI exam ni main door ya higher education, then kumzuia mwanafunzi kufanya huo mtiani ni kumkatisha tamaa ya kujiendeleza kielimu, and ultimate career goals.

Napenda kuwakilisha
 
Hivi ni kwanini Tanzania bado wanafunzi kuanzia shule ya msingi mpaka vyuo vikuu bado wanasoma masomo ya zamani ya miaka ya 1960,utamkuta mwanafunzi kamaliza chuo kikuu,lakini anakuwa upeo wake ni mdogo sana,mimi nadhani muda umefika sasa kubadilisha mfumo wetu wa elimu kwani umepitwa na wakati,tusome kutokana na mazingira ya sasa.
 
ni mambo mengi sana yanahitajika kubadilishwa kuanzia mitaala hadi ufundishaji. Ila watanzania wengi nao huwa hawapendi kujisomea na elimu inawaforce wasomee mitihani na si kuelewa. Lakini pia elimu yetu sio mbaya kiasi hicho bali inahitaji some marekebisho kuendana na wakati.
 
Nimeona hii institute haya ndio wanafanya na wana wafanyakazi wengi tuu,at least kumbe kuna chombo kinachoshughulika mitaala yetu lakini sijui kama wanafanya kazi nzuri

Institution Name: Institute of Curriculum Development; ICD.
Address: P.O. Box 35094. Dar Es Salaam. Tel: (255-51) 72765.
Country: United Republic of Tanzania, The. République-Unie de Tanzanie.
Contact: Director.
Geographical Coverage: national
Staff: 170; PROFESSIONALS: 70.
Working Languages: English; French
Activities Undertaken: biology education; chemistry education; physics education; integrated curriculum; mathematics education; general technical education; health education; training; educational materials; school industry relationship; rural areas; womens education; teaching guides.
Groups Covered: primary education; secondary education; post secondary education; teachers pre-service; teachers in-service; technicians; youth out-of-school; researchers; education policy planners; teachers associations
Publications: Text books and Teacher's Guides in all subjects (Pre-school, Primary, Secondary ('O' & 'A' level)
Periodicals: Tanzania Education Journal; Studies in Curriculum Development; Eastern and Southern Africa Curriculum Organization Journal; Kunguru (Kiswahili magazine on Environment)
Organization of Meetings: local; national; regional; international
Additional Information: Improvement of primary science; introduction of unified science and technology in secondary schools and teachers' college; introduction of computer science course at secondary school level; vocationalization of primary school curricula; introduction of special curricula for talented students in maths, science; exchange visits and lectureship. International co-operation in improving content and teaching methods in primary science, (integrated science, technology education, vocationalisation of the curriculum, computer science); educational technology; twining with other institutions of education (curriculum development).
 
20 Reactions
Reply
Back
Top Bottom