Mchango kwenye Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Tarehe 16/08/2011
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nukushukuru kwa dhati kwa kunipa fursa hii. Lakini vile vile siungi mkono hoja si kwa sababu sina imani na Waziri wala Naibu Waziri, hapana. Ni kwa sababu licha ya wao kuwa na nia njema ya kufanya kazi mbali ya kuwa na fedha finyu. Lakini nadhani hapati ushirikiano wa kutosha kutoka Serikalini kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mzungumzaji mmoja nadhani ni mama Kikwembe if I am not mistaken wakati nimetoka akapiga mawe kidogo. Lakini nimhakikishie kwamba siwezi kuzungumza kitu ambacho sina ushahidi nacho. Aliniambia nimtajie majina ya Madiwani waliokwenda Marekani siku nne. Nitamtajia Kata, majina itakuwa kazi yake yeye kutafuta. Kuna Diwani wa Kata ya Magamba, kuna Diwani wa Kata ya Sitalike, kuna Diwani Viti Maalum Karema na kuna Diwani Viti Maalum Uruwira. Sasa majina akayatafute yeye.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini inasikitisha. Unapoona Mbunge mnajaribu kutetea eneo lake yeye, anakuja ana-crash down pasipo hoja za msingi na kwa sababu ya uvivu wa kusoma. Juzi kwenye SADC Forum iliyokwisha tu majuzi. Moja ya ajenda ilikuwa ni Land Crabbing Africa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wazungu huko walishamaliza kwao, wanakuja kurudisha ukoloni. Kibaya zaidi mtaalam wa Canada, mzungu huyo huyo akaenda na mikataba mizito hivi na mkataba uliotolewa mfano, kama West Case Scenario ni mkataba wa Agrisoil Tanzania. Nasikitika jana namsikia Mbunge mmoja kutoka Kigoma, anasema eti wenzake wa Kigoma wameshindwa kutumia ardhi, wakati kuna hekta 80,000 wameshindwa kutumia ardhi, kwa hiyo walete wawekezaji. Tena msomi mzuri, inasikitisha. Kwa hiyo, niseme hili la suala la Agrisoil mbali na
upungufu wake wote na upuuzi wake wote umekiuka Sheria ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria zetu ziko wazi kabisa na hii namwambia Mheshimiwa Waziri Mkuu asipoli-handle vizuri anaweza akaanguka nalo. Ataanguka nalo kabisa. Kwa sababu kuna ushahidi wa moja kwa moja unaoonyesha kwamba Ofisi yake ilihusika. Kwa hiyo tutumie busara tuokoe nchi. Sheria ya Ardhi iko wazi. Muwasaidie Mawaziri, mumsaidie Naibu Waziri. Sheria ya Ardhi iko wazi kabisa. Mgeni ama mwekezaji anapotaka kuja kumiliki ardhi ya nchi imeeleza wazi, kifungu cha 19, Kifungu cha 20(i) hadi 20(iv) mabadiliko ya 2004. Very clear na imesema wazi kabisa kama kuna joint venture inamhusu raia na Sheria ya Uraia haijatambua kampuni, haijatambua Halmashauri, haijatambua kitu kingine chochote raia mmoja mmoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mtuambie huko Rukwa ni raia gani anamiliki hekta laki mbili na kitu. Huko Lugufu Kigoma kuna raia gani anamiliki hekta 80,000 ambaye anaingia ubia sasa ili ule mchakato wa kufuata TAC usifuatwe. Naomba tuache ushabiki. Hii ni crisis?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza taarifa yake siitaki. Lakini pili, mimi mwenyewe hivi kiwanja changu sina Hati Miliki. Hati Miliki siyo issue.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tatu, kuna kitabu cha makubaliano waliyoingia baina ya Halmashauri na Agrisoil na mkitaka nitaleta kwenye Meza yako. Wao wenyewe hapa wamekiri, kuna hivyo vitu vinavyoendelea Bungeni. Kwa hiyo, kama nyinyi ambao ndiyo mnatakiwa mtekeleze Sheria mnakuja hapa mnatetea wahalifu, tunakoelekea kama nchi kunatisha. Hatutafuti umaarufu wa kisiasa, umaarufu upo tayari, tunataka kujenga nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nirudi Jimboni maana nilisimama kwa ajili ya Jimbo. Lakini alinivurugua system Mama Kikwembe ikabidi nirudi kule ambacho sikutaka kurudi.
Suala la kwanza?
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunilinda. Katika Jimbo langu na nadhani katika Majimbo ya Dar es Salaam ndiyo yanaongoza katika migogoro ya ardhi. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri na Mheshimiwa Waziri suala la Mabwepande. Miaka minne iliyopita mlikwenda pale, mkawaambia wananchi wasiendeleze maeneo yao. Mkawalipa wengine kama 160. Mheshimiwa Naibu Spika, namwonea huruma sana kwa sababu 2015 sijui kama atarudi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Mabwepande. Naomba na muda wangu huu pia uzingatiwe. Miaka minne iliyopita Serikali ilikwenda kufanya tathmini na ninavyozungumza hivi pia na katika mfumo huo huo nazungumzia eneo la Kwembe kwenye Jimbo la Mheshimiwa Mnyika. Nilikwenda kufanya tathmini, wananchi wakaambiwa wasiendeleze maeneo yao na kwamba Serikali ina mipango ya kuja kulichukua lile eneo kwa ajili ya matumizi mapya. Jimbo la Ubungo lilikuwa ni kwa ajili ya kujenga Chuo cha Muhimbili kwa mantiki ya Campus nyingine. Lakini vile vile Mabwepande kulikuwa kuna chuo cha IFM na miradi mingine 20,000 ya viwanja.
Mheshimiwa Naibu Spika, imepita zaidi ya miaka minne. Wananchi hawajui mustakabali wao. Waliolipwa ni wananchi 160 tu kwa kipindi hicho zaidi ya wananchi 600, hawajui mustakabali wao ukoje. Lakini vile vile kwa upande wa Kwembe Serikali iliwaahidi wananchi kuwalipa pamoja na thamani ya ardhi na siyo mimea, kwa sababu pia Sheria zinasema hivyo na wananchi wa Kwembe hawana tatizo la kuhama. Tatizo lao la msingi ni ile haki yao waliyokubaliana kimsingi walipwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mabwepande tunavyozungumza leo hii na nakumbuka wakati wa Kamati, nilivyokuja kwenye Kamati yao, nilimwambia kuna uvamizi wa hali ya juu unaendelea. Wananchi ambao waliiamini Serikali yao hawakulima, hawakujenga kwa sababu waliambiwa kwamba kuna mipango ya maendeleo, wakaa pembeni leo wamegeuka wakimbizi kwenye ardhi yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa namwomba Mheshimiwa Waziri kwa sababu nimeshapiga kelele katika Halmashauri, nimekwenda kwake kwa njia ya barua. Lakini hali kule ni mbovu. Naomba Serikali ichukue hatua. Mimi kama Mbunge wa Kawe silindi mvamizi hata mmoja. Wasije watu wakawa huko kwa maslahi yao, wanasema Mheshimiwa Halima Mdee anatuunga mkono. Sijatuma mvamizi yoyote akavamie eneo,nataka haki itendeke. Kwa hiyo, naomba suala la Mabwepande na suala la Kwembe naomba myafanyie kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine Mheshimiwa Waziri kuna hili suala la Boko Dovya katika Shamba la Bwana Somji. Kuna taarifa hapa kwa vyombo vya habari kutoka kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kipindi kile alipokuwepo Mheshimiwa Chiligati, alikiri kwamba hili tatizo limekwisha. Serikali itachukua lile eneo kwa ajili ya kugawiwa kwa wananchi. Mpaka leo hakuna kinachoeleweka Somji anaendelea kuwasumbua wananchi ambao wako kwenye maeneo hayo. Kwa hiyo, naomba tafadhali tafadhali niweze kupata ufafanuzi kwa haya masuala.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ni suala la Chasimba. Hili suala siyo dogo kama watu ambavyo wanataka walifikirie. Ni suala ambalo linahusisha wananchi zaidi ya 10,000. Ni suala ambalo ushahidi wake uko wazi na nimeeleza kwa kina sana kwenye hotuba yangu. Lakini nitalizungumza hapa. Inawezekana Serikali mkaja na scenario kwamba hili suala ni la zamani, lilienda Mahakamani na limeamualiwa Mahakamani. Kwa hiyo, wananchi waondoke, naomba mtumie busara. Nina hukumu ya Mahakama hapa. Nina documents hapa nitamletea Mheshimiwa Waziri zinazoonesha jinsi kijiji kilivyosajiliwa zinazoonesha kwamba mmiliki wa kiwanda hamiliki viwanja vyote vitatu kwa mantiki ya moja, nne na saba. Lakini nimesoma hukumu hapa, inasema naomba ninukuu kidogo: "It is the respondent case from a total twelve witnesses that the village officials of Boko". Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba muda wangu kidogo, kengele ya kwanza? It is the respondent case from a total of twelve witnesses that the village officials of Boko and Tegeta were contacted with the view of securing more land by organizing meetings with the villages. At the end of the day the respondent managed to buy a number of villages by wealth composition. Hukumu sababu katika hii kesi respondent alikuwa ni TUGHE. Kwa sababu ilikuwa ni Mahakama ya juu kabisa. Wanakiri kwamba walioweza ku-manage ni a number of villages sio all of the villages. Ndiyo maana nashukuru tu kwa maana ya Mheshimiwa Ole-Medeye. Nashukuru sana. Wananchi waliokuwepo pale ni watu wazima, tofauti na maeneo mengine ya uvamizi, unaona ni vijana vijana tu wamekuja juzi. Naomba Serikali iliangalie hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Lakini kesi ambayo ilikuwa inahusu watu takriban 1,000 ikaamuliwa on technical grounds kwamba linapokuja suala la ardhi, hatuangalii suala la representative's suit hairuhusiwi. Ikiwa ni Mahakama ya Rufaa Court of Appeal, haki za maelfu za wananchi zikaminywa simply because kwa uelewa wao labda mdogo waliamua wenzao 13 wakawakilishe Mahakamani na kati ya wenzao 13 waliokwenda kuwakilisha Mahakamani still walishindwa kuthibitisha wanne kati yao kwamba walilipwa fidia. Kwa hiyo, naomba Waziri asiwe mkali, naomba mtumie busara. Nawaombea wapiga kura wangu. Najua kuna haki imeminywa sehemu. Najua kuna interest za watu zinataka kuwaumiza watu maskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasikia wanataka kuhamishiwa Mabwepande. Sisi hili hatuliafiki. Tunajua eneo la kiwanda ni kubwa. Wakitaka kujipanua wataacha chenji. Tunaomba muwasaidie wananchi na niwaambie kwa hili, maana Madiwani wa Kata hizo mbili ni wa CCM. Moja, tumesema iwe jua, iwe mvua, sisi tutakufa na wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hatufanyi uchochezi. Lakini nadhani natumia lugha laini sana. Ukienda Chasimba mwenyewe, sijui! Ole Medeye, tulikwendanae na anajua zaidi, naomba tuwasaidie wananchi wetu. Kuna siasa hapa, kuna vyama vyote viko kule, tuweke utu kwanza; eneo lipo la kutosha, la msingi ni kwenda kufanya vikao na wananchi, kujua eneo la kiwanda liko wapi, wananchi wanaweza wakakaa wapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho, hivi viwanja 20,000. Kunakuwa kuna tatizo kwamba, Wizara kwa nia njema kabisa mnaandaa miradi mbalimbali. Lakini tatizo ni kwamba, miradi hiyo haimilikishwi kwa wananchi ili waweze kujua viwanja vya wazi ni vipi? Viwanja vya shule ni vipi? Viwanja vya huduma za jamii ni vipi? Matokeo yake viwanja hivi vimegeuka kuwa sehemu ya Wenyeviti wa Mitaa kupata kula yao! Kwa hiyo, naomba katika miradi yoyote ambayo mliifanya, mwende mkai-review, muangalie maeneo ya wazi, maeneo ya umma ni yapi? Myafanye yawe wazi, ili wananchi kwenye maeneo hayo wawe walinzi wa ile rasilimali. Bila kufanya hivyo!
Mheshimiwa Naibu Spika, leo sheria haitambui kama Mwenyekiti wa Mtaa, anaweza akagawa eneo, lakini nitakwambia huko Dar-es-Salaam, wanagawa kwa kwenda mbele! Wakati nyie mnatoa maagizo huku, Wenyeviti wa Mitaa na baadhi ya Madiwani ambao sio waaminifu wanaendelea kuuza maeneo kwa kushirikiana na watu wa Manispaa ambao sio waaminifu. Kwa hiyo, naomba haya myaangalie kwa makini.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa na ambalo pia sio la muhimu, ni viwanja vya wazi Mkoa wa Dar-es-Salaam. Tunajua mna changamoto kubwa kwa sababu, wengi ambao wamewahi kupewa hayo maeneo ya wazi, hususan katika maeneo strategic, ni wakubwa! Wengine wamejenga ma-bungalow yao! Sasa naomba leo mtuhakikishie wakati mnahitimisha, ile taarifa iliyotolewa na Kamati iliyoundwa na Mheshimiwa Lukuvi, mtaitekeleza kwa ukamilifu wake na ndani ya kipindi gani? Nakuhakikishia Mheshimiwa Tibaijuka, ukiniahidi hilo nitakuona kweli wewe ule moto wako unaendelea. Ukiwa unasitasita nitajua yale ambayo yanasemwa, ulianza kwa speed wenzio wakakuminya! Tunakuamini mama, namwamini Mheshimiwa Naibu Waziri sana kama ambavyo namwamini yeye sana, hii sekta ndio uhai wa nchi. Hii sekta tukiipuuza na naiambia Serikali, tukiipuuza watoto wetu, wajukuu zetu watakuja kuchinjana na hatutaki tutengeneze Tanzania ya kuchinjana!
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana.