[TABLE="width: 879"]
[TR]
[TD="bgcolor: #ffffff"][TABLE="width: 599"]
[TR]
[TD]
LOWASSA, CHENGE WAIVURUGA CCM
na Mwandishi wetu
[/TD]
[/TR]
[/TABLE]
[/TD]
[TD="width: 140, bgcolor: #FFFFFF"][/TD]
[/TR]
[TR]
[TD][TABLE="width: 599"]
[TR]
[TD]
HATIMA ya Chama cha Mapinduzi (CCM), sasa inaonekana kuwa mikononi mwa vigogo wawili wa chama hicho, Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, na Andrew Chenge, ambaye ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, baada ya kubainika kuwepo kwa kundi kubwa la viongozi na makada maarufu walio tayari kuwaunga mkono katika jambo lolote watakaloamua.
Habari za uhakika zilizolifikia Tanzania Daima, zimeeleza kuwa kundi hilo ambalo ndani yake wamo wenyeviti kadhaa maarufu wa CCM wa mikoa, limekuwa kwa siku mbili likifanya mikutano ya siri na kuonana na baadhi ya wajumbe ambao wanaonekana kukosa msimamo wa dhati katika kuamua kuwaondoa wabunge hao katika uongozi wa juu wakidaiwa kuwa magamba yanayotakiwa kuvuliwa.
Mmoja wa viongozi wanaowaunga mkono wabunge hao ameliambia Tanzania Daima kuwa wataungana na wabunge hao katika maamuzi yao, kwa madai kwamba wako viongozi wengi wanaotakiwa kuwafukuza kwa kukivuruga chama hicho.
Ubovu ndani ya chama chetu hauwezi kubebeshwa watu wawili tu, kana kwamba wao ndio waamuzi wa mwisho. Kama ni kutota tutatota nao, na wala hatuoni aibu katika hilo, alisema kada huyo ambaye jina lake linahifadhiwa.
Taarifa zimebainisha kuwa mbali na ajenda nyingine zinazotarajiwa kujadiliwa, inayoonekana kukamiwa kwa nguvu kubwa ni ile ya utekelezaji wa dhana ya kujivua gamba ambayo Katibu wa Halmashauri Kuu ya Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, amesikika mara nyingi akiwalenga wabunge Lowassa, Chenge na Rostam Aziz kama magamba yanayotakiwa kuvuliwa.
Ni kauli hiyo iliyomfanya aliyekuwa mbunge wa Igunga na mjumbe wa Kamati na Halmashauri Kuu ya CCM, Rostam Aziz, kujivua nyadhifa zote za uongozi pamoja na ubunge baada ya kuchoshwa na kile alichokiita siasa za maji taka alizodai zinafanywa na Nape na Naibu Katibu Mkuu (bara), John Chiligati.
Hata hivyo, taarifa za kina zinaonyesha kuwa kundi linalotaka wabunge hao kuondoka limeapa kupigana kwa nguvu zote kuhakikisha watuhumiwa wote wa ufisadi wanaodaiwa kuchafua jina na heshima ya CCM, wanavuliwa nyadhifa zao hata kama hatua hiyo itasababisha chama hicho kugawanyika.
Nani kakuambia maneno hayo
sisi hatujapanga kumwondoa Lowassa wala Chenge
hizo ni njama zenu waandishi wa habari, alisikika akisema mjumbe mmoja wa Halmashauri Kuu ya CCM kwa mwandishi wa habari hizi alipotakiwa kutoa maelezo ya yeye na wenzake kuwa miongoni mwa watu walio katika kundi linalotaka wabunge hao watimuliwe.
Hata hivyo, bila kujua kuwa alikuwa akifuatiliwa kwa makini, mjumbe huyo dakika chache baadaye alisikika akizungumza na mtu mwingine kwa njia ya simu, akimtaka kuwa makini na waandishi wa habari kwa madai kuwa siri zao zinavuja hovyo kwani habari zinasema kuwa kundi linalotaka Lowassa na Chenge wangolewe limeamua kutumia kwanza njia za kistaarabu za kuwatuma wazee mashuhuri wa CCM kuonana na wabunge hao na kuwaomba waondoke kistaarabu ili kunusuru uhai wa chama hicho.
Hoja nzito inayotakiwa kutumiwa ni kuwataka watambue hali ngumu ya kisiasa ilivyo nchini, hususan upinzani mkubwa unaokipata kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho kimekuwa kikiwanyima usingizi.
Jana wajumbe wa Kamati ya Maadili walikutana kwa siku nzima katika kikao cha siri kilichoketi makao makuu ya chama hicho maarufu kama White House chini ya Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais Jakaya Kikwete.
Rais Kikwete, aliwasili eneo hilo majira ya saa tano na kuungana na viongozi wenzake kuanza kikao hicho, na zilikuwepo taarifa zisizo rasmi za kuhojiwa kwa baadhi ya makada wakongwe wa chama hicho pamoja na wale wa Umoja wa Vijana (UVCCM), wanaotuhumiwa kuzua mtafarufu wa ndani uliokigawa chama katika makundi ambayo sasa yanapingana hadharani.
Makada wengine waliotarajiwa kuhojiwa na kamati hiyo kwa mujibu wa chanzo chetu ni watuhumiwa wa ufisadi ambao wameshindwa kutekeleza maagizo ya NEC ya kujivua gamba kwa kuachia nyadhifa zao kwenye chama ndani ya siku 90 ambazo kimsingi zimehitimishwa kwa kada mtuhumiwa mmoja, Rostam Aziz, kuachia ngazi zote ukiwemo ubunge wa Igunga.
Tayari kumekuwa na lawama kutoka kwa vigogo wengi wa chama hicho za kumshtumu Nape na Naibu Katibu Mkuu, Kapteni mstaafu John Chiligati, kuwa walibeba na kutekeleza agizo hilo la falsafa ya kujivua gamba kwa malengo yao binafsi.
Akizungumza kwa kifupi majira ya saa 11 jioni wakati wa mapumziko, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Chiligati, alisema Kamati ya Maadili ni sehemu ya CC na hivyo walikuwa wakiandaa ajenda za mkutano wa leo. Hapa tunapumzika hadi saa moja jioni, tutarudi kuendelea na kikao chetu.
Hata hivyo, alipobanwa zaidi kuhusu taarifa za baadhi ya makada kuhojiwa na kamati hiyo, Chiligati alionekana kusita na kukwepa kulitolea ufafanuzi wa kukiri ama kukataa.
Wewe hata kama kuna watu waliohojiwa na kamati...tusubiri maamuzi yatatolewa kwenye kikao cha NEC, alisema Chiligati kwa kifupi.
[/TD]
[/TR]
[/TABLE]
[/TD]
[/TR]
[/TABLE]