SoC02 Kilimo fursa kubwa

Stories of Change - 2022 Competition

Mbenero

New Member
Sep 12, 2022
3
7
KILIMO FURSA KUBWA.

Chanzo cha binadamu ni uumbaji wa Mungu. ‘’Mungu akasema , Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi...Mwanzo 1:26. Na pia, Biblia inathibitisha kwamba ‘’Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai… Mwanzo 2:7.

Mungu pia, kabla ya kuumba binadamu aliandaa mazingira wezeshi kwa binadamu kuishi. Moja ya maandalizi aliyofanya Mungu ili kuwezesha wanadamu kuendesha maisha ya kila siku‘’Bwana Mungu akamtwa huyo mtu, akammweka katika bustani ya edeni, ailime na kuitunza’’….Mwanzo 2:15.

Binadamu tumewekwa katika mazingira yanayotuwezesha kuishi kwa mafanikio anayoyatumaii Bwana, Mungu. Kazi ya kwanza kwa binadamu kuifanya ilikuwa ni kulima na kuitunza bustani ya Edeni. Hili lilikuwa agizo la Mungu kwa wanadamu wa Kwanza na pia kwa vizazi vyote. Bwana, Mungu aliaanda mazingira wezeshi kwa kizazi kilichopita, cha leo na vizazi vingi vijavyo; ‘’Mungu akasema, Maji yaliyo chini ya Mbingu na yakusanyike mahali pamoja, ili pakavu paonekane ikawa hivyo.

Mungu akapaita pale pakavu Nchi; na makusanyiko ya maji akayaita Bahari; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Mungu akasema, Nchi na itoe majani, mche utoao mbegu, na mti wa matunda uzaao matunda kwa jinsi yake, ambao mbegu zake zimo ndani yake, juu ya nchi, ikawe hivyo. Nchi ikatoa majani, mche utoao mbegu, na mti wa matunda uzaao matunda kwa jinsi yake, ambao mbegu zake zimo ndani yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema’’……Mwanzo1:9-12.

Bwana, Mungu aliumba eneo la Nchi kubwa ili likidhi mahitaji ya Mwanadamu ya kulima na kuotesha mazao ya aina mbalimbali kwa ajili ya kuishi na alitunze kwa ajili kuhakikisha manufaa yanaendelea kudumu kwa ajili ya vizazi vyote vya nyakati zote katika dunia hii. Kwahiyo, tangu mwanzo Mungu aliandaa mazingira na kumwambia binadamu ajihusishe na Kilimo.

Hata kwa sasa kilimo kimekuwa sekta muhimu kwa uchumi wa mtu mojamoja na kwa Taifa. Mazao ya kilimo yanatumika kwa chakula kwa binadaamu na wanyama na malighafi kwa viwanda vingi hapa duniani. Mazao ya chakula, mafuta ya kula, ya nazi, mawese, alizeti, karanga, mzeituni, mahindi, matunda ya kila namna, mpira wa miguu…..nk, vyote hivi chanzo chake ni kilimo. Mazao ya kilimo na kilimo ni FURSA KUBWA SANA YA UCHUMI NA MAISHA YA BINADAMU kwa sababu ya uimara wake katika soko-ni mahitaji yasiyoepukika kwa maisha ya binadamu, viwanda na wanyama. Ikiwa vijana na watu wa rika zote wakijihusisha na biashara ya mazao ya kilimo au kilimo biashara hata vyote kwa pamoja itakuwa ni daraja muhimu kwa ukombozi wa kilio cha ajira na uchumi wa mtu binafsi na Taifa.

Pamoja, na sekta ya kilimo kuwa tegemeo kwa Watanzania kwa zaidi ya asilimia 80+, Nchi ya Tanzania ina Ardhi kubwa yenye rutuba na mito inayotiririka maji na inapatikana kwa gharama nafuu sana hata mtu wa kipato cha chini anaweza kununulia ardhi. Tarehe 6 Aprili, 2019, Aliko Dangote, Tajiri Na.1 Africa analikuwa na Mahojiano na Mo Ibrahim juu ya Africa na Biashara, Uongozi na mambo mengine aliuzwa na Mo Ibrahim kwamba ‘’nini wafanye vijana ili waweze kuwa milionea katika umri wa miaka 20” Aliko Dangote alisema, vijana wakitaka kupata utajiri au kuwa milionea katika umri wa miaka 20 wanatakiwa kujihusisha na KILIMO NA TEHAMA. Katika mazungumzo hayo, Aliko Dangote alisema Analima Mpunga nchini Nigeria. Aliko Dangote ameona pia fursa kwenye Kilimo, wewe je? Tafakari.

Sasa kwanini kilimo kina fursa nyingi sana ambazo kijana na mtu wa rika yeyote anaweza kunufaika nazo, lakini hapohapo vijana wengi hawataki kujihusisha nacho na huku wanalalamika na ajira na maisha magumu, na wakijihusisha nacho wanachana nacho kabla ya mafanikio wanayotaka hawajayafikia.

Zifuatavyo ni moja ya sababu zinazopelekea wengi wasifikie mafanikio au wasijihusishe na kilimo;

  1. Dhana ya kutaka kupata bila ya kufanya chochote.
Siku hizi vijana na watu wa rika mbalimbali wanapenda kujihusisha na vitu vitakavyowapa fedha bila kufanya chochote, fedha ya haraka haraka –michezo ya bahati nasibu na kamari na utapeli imekuwa maarufu sana. Mifumo hii ya upataji fedha imekuwa laana na chanzo kikubwa cha kuwa na hali iliyopo kwa vijana na watu wanaopendelea kujihusisha navyo-umaskini na uvivu-ndiyo matokeo yako. Kuna usemi usemao ‘’Huwezi kuvuna Usichopanda’’maana yake chochote afanyacho mtu ndicho atakachopata matokeo yake.

Ukipanda vibaya utavuna matokeo mabaya, na ukipanda vizuri utavuna matokeo mazuri. Dhana hii imepelekea wengi wasijishughulishe na kilimo, kwani kilimo kinataka kuwekeza, uvumilivu, king’ang’anizi na muendelezo ili kufikia mafanikio ya kweli. Katika maisha halisi, Dhana ya kupata chochote bila kufanya chochote haipo. Kwa kitambo huonyesha kuna mafanikio lakini mwishowe ni anguko.

Biblia inasema, ‘’basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafanishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba….Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafanishwa na mtu mpumbavu,aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga…Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguke; nalo anguko lake likawa kubwa…Mathayo 7: 24-27.

Maana yake ni kwamba maisha au jambo lolote lina Kanuni na ili kuweza kufanikiwa na kudumu lazima kufuata kanuni zake, na kuzipuuza kanuni ni kujihahakishia anguko-lenye hasara kubwa. Kwa nini anguko, kwa sababu hakuna kanuni ambazo zitasaidia kuhimili changamoto zinapojitokeza. Kumbuka changamoto zitaendelea kuwepo mpaka mwisho wa dunia, kukabiliana nazo ni kwa kufuata KANUNI TU. KANUNI zinahitajika kwa ajili kuanzisha, kuendeleza na kutunza. Mafanikio ni kufuata kanuni na kufeli au kushindwa ni kutofuata kanuni. Mafanikio endelevu na kweli na yana gharama, gharama ya muda, fedha, kushindwa na kuanza upya, kushinda vikwazo vyote au uvumilivu. Maisha ni vita, unapaswa kushindana ili kushinda. Weka mpango mkakati vyema, ushindi ni hakika

  1. Madai ya kusema hakuna mitaji.
Ni kweli kilimo kinahitaji mtaji. Hoja ya msingi mtaji upi wa kwanza unahitajika katika kilimo. Naomba nikukumbushe kuhusu mtaji, eti mtaji nini? Mtaji ni rasilimali zinazotumika kuzalisha na kuongeza uzalishaji katika jambo linalofanyika. Aina ya mitaji; 1.Akili 2. Ardhi 3. Watu 4.Afya.. nk. Rasilimali fedha sio mtaji? Rasilimali fedha ni mtaji, wakati upi inahitaji? Kuna usemi usemao ‘’si fedha inatengeneza fedha’’ nini basi? Ufahamu wa kifedha (financial intelligency), ufahamu wa namna ya kutengeneza fedha, hata kilimo kinahitaji ufahamu badala ya kuwaza tu kwamba unahitaji kuwa na fedha ili ufanikiwe.

Maana wapo wengi wana fedha lakini kwenye kilimo hawana mafanikio. Mafanikio katika sekta ya kilimo ufahamu unakuja namba moja, na rasilimali fedha au pembejeo vinafuata ili kufanikisha. Hatahivyo, mtaji ni kile ulichonacho ambacho unaweza kuanza nacho katika kilimo. Mfano, vijana wengi wana simu janja (smartphone) za gharama kuanzia 150,000.00 hadi 2,000,000.00 kwa ajili ya mawasiliano yasio na faida huko wanalalamika maisha magumu na hawana mitaji. Kumbe, fedha zinazotumika kununua simu na vocha zikitumika kama mtaji wa kilimo baada ya miaka 5,10,15 watakuwa mbali kimtaji na maendeleo.

Hii, ni sawa na Mungu alipomuuliza Musa, una nini mkononi?, wakati walipotaka kuvuka bahari ya Shamu kwenda Kanaan. Musa akasema fimbo, na Mungu akamwambia nyosha fimbo na njia ikapatikana, watu wakapita. Lakini kabla ya tukio hilo, watu walikuwa wanalalamika wasijue kuwa fimbo ya Musa ilikuwa mtaji kwao kutengeneza njia ya kwenda ng’ambo ya bahari ya Shamu. Ujumbe, sawa mtaji unahitajika lakini anza na ulicho nacho katika kilimo.

  1. Kusikiliza maneno ya kutatisha tamaa.
Katika maisha, maneno Hasi yamekuwa kikwazo kikubwa katika kufanikisha mambo. Mfano wa Maneno Hasi ni ‘’wewe huwezi kilimo’’,’’alishindwa Fulani sembuse wewe’’, ‘’kilimo kinahitaji gharama kubwa’’, ‘’sina mtaji’’, ‘’Siwezi’’. Maneno haya yakikubalika mtu hawezi kufanya chochote. Maneno haya na ya namna hiyo hayapaswa hata kutamkwa bali tamka maneno haya ‘’Nifanyeje’’, ‘’Nitaweza’’, ‘’Nitafanikiwa, ‘’Nitashinda’’……nk. Haya ni maneno ya Ushinde na Mafanikio, yanafungua ubongo kuwa na mtazamo wa mafanikio ya kila unachotaka kufanya. Kumbuka kwamba,’’awazacho mtu ndicho kimeujaza moyo wake’’waza mafanikio, sikiliza mafanikio, kaa na zungumza na walifanikio katika kilimo nawe utafanikiwa tu.\

  1. Kutokuwa na mipango yakufanisha kilimo.
Watu wengi wanashindwa katika kilimo kwa sababu wanafikiri kuwa na fedha tayari wamefanikiwa. La, Kufanikiwa hakuhitaji mitaji tu bali pia mipango yakuweza kufanikiwa katika kilimo. Wakulima wengi na wale wanaotaka kujihusisha na kilimo huwa hawana mipango yakufanikisha. Mipango ni hatua, mwelekeo, inaanisha mambo ya kufanya na muda utakaotumika, gharama za kufanikisha, inatumika kufanya tathmini ya kinachofanyika, inaonyesha maeneo ya kuboresha kwenye mpango wakati wa utekelezaji, ni jicho na ni njia sahihi ya mafanikio. Kutokuwa na mipango ni kujihahikishia kushindwa katika kilimo. Panga namna utakavyofanya kilimo chenye mafanikio, hakika utafanikiwa.

  1. Kutokuwa na taarifa sahihi za kilimo.
Kufanikiwa katika kilimo, taarifa sahihi ni muhimu sana, ingawa baadhi ya watu huwa hawana taarifa sahihi ama kwa kupuuza au kutojua kwamba kuwa taarifa ni jambo muhimu kwa maendeleo yao.

Ajabu kweli, dunia ya leo ina vyanzo vingi vya taarifa lakini kwa bahati mbaya wengi hawanufaiki navyo, tuna fursa ya kupata taarifa lakini muda mwingi tunapoteza kwenye vitu ambavyo havina manufaa katika maisha. Unaweza kupata taarifa za kilimo kupitia; vipindi vya TV, You Tube, Instagram, Google, Facebook, wazoefu na wakulima wenye mafanikio……nk. Hivi vyanzo ni mtaji mkubwa maana vinatoa ufahamu unaohitajika wa kuanzisha biashara ya kilimo na kilimo.

Katika kilimo tunapaswa kuwa na taarifa ya soko ya mazao unataka kulima, uhitaji wa mazao, udongo, aina ya mbolea, msimu sahihi na aina ya zao, mbegu bora kwa kila zao-inayovumilia magonjwa na mazao bora na mengi. Tafuta taarifa kabla hujaanza kilimo cha zao lolote, itakuwa na manufaa sana kwako.

  1. Kutokuwa na ufahamu na ujuzi sahihi wa kilimo.
Ufahamu unapelekea kuwa na ujuzi wa namna ya kufanya mambo. Ufahamu na ujuzi, ni mitaji inayokuja katika nafasi ya kwanza ambayo kila mjasiriamali au mkulima anatakiwa kuwa nao. Ukiwa na fedha na unajaribu kufanya jambo na huku huna ufahamu na ujuzi wake-samahani naomba nikwambie ukweli kwambo jambo hilo umefeli kabla hujaanza. Tena naomba niseme ufahamu na ujuzi unapima matokeo ya jambo, yaani mwenye ufahamu na ujuzi mdogo matokeo yake yatakuwa madogo na mwenye ufahamu na ujuzi mkubwa matokeo yake yatakuwa makubwa. Mfano, wacheza mpira, chukulia Cristiano Ronaldo na Jado Sancho pale Man. United wote washambualiaji-forward, Cristiano Ronaldo analipwa Pound 515,385.00 (£515,385) na Jado Sancho analipwa Pound 350,000.00 (£350,000) kwa wiki (Chanzo: Man. United website). Tofauti ya wachezaji hawa wawili ni kwamba Cristiano Ronaldo ana ufahamu na ujuzi na uzoefu mkubwa wenye mchango wa matokeo kwa asilimia 50+ katika mechi za mpira, inamfanya kuwa na dhamani kuliko Jado Sancho. Ninachojaribu kuwasilisha hapa ni kwamba ufanamu na ujuzi unapotumika utazaa uzoefu wenye kuhakikisha matokeo yanatakiwa katika kilimo na jambo lolote unalopanga kufanya.

Jambo jema kwa dunia ya leo, kama ilivyo kwa taarifa, ufahamu na ujuzi unapatikana kilahisi na kwa gharama wezeshi kwa mwenye nia ya kuzipata. Kupitia makala kwenye TV, You Tube, Google, wazoefu na wakulima wenye mafanikio, mafunzo ya kilimo…..nk.

  1. Kukosa imani na kilimo
Imani, Biblia inasem; Basi Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana…..Waebrania 11:1. Ni hakika ya mambo yatarajiwayo, yaani unakuwa na uhakika ya mambo unayoyategemea. Mfano, kilimo cha Mpunga, unategemea kupata gunia 100 za mpunga kwa ekari tano. Kwahiyo, unapaswa kuwa na imani kwamba umepata gunia 100 za mpunga kwa ekari tano. Imani inakupa msukumo wa kufanya. Imani ipi? Ni Imani na Matendo…..amini kwamba umepata gunia 100 za mpunga kwa ekari tano na lakini lazima ufanye jambo kuhakikisha unapata gunia 100 za mpunga. Hebu sikia hii, Biblia inavyosema ‘’Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo?Je!Ile imani yaweza kumwokoa?....Yakobo 2:14, na Yakobo 2:17 anatoa jibu anasema …‘’vivyo hivyo na Imani, isipokuwa ina matendo, imekufa, sikia hii tena, Yakobo 2:26 anakazia umuhimu wa Imani na Matendo ili kufanikisha anasema..

Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa. Sasa turudi kwenye mfano wetu, ni kweli una imani ya kwamba umepata gunia 100 kwa ekari tano (imagination-cha kufikirika), ni jambo jema na hongera sana kwa hatua nzuri uliyofikia lakini kuhakikisha unapata gunia 100 kwa ekari tano (outcome-Matokeo halisi) unapaswa kufuata hatua zote (Kanuni) zote za kulima Mpunga; Andaa shamba kwa wakati, Lima kwa wakati, Panda mpunga kwa wakati na Tunza kama inavyotakiwa, Hakika utapata Mavuno uliyotarajia. Kuwa na imani kunafanya mkulima kuwa na uvumilivu au king’ang’anizi na kuwa na muendelezo wa kilimo. Hii, inachochea tena kuwa na tathmini ya kile kinachoendelea kwenye kilimo. Tathmini huonyesha mahali pa kuboresha.

Basi imani, chanzo chake ni kusikia….Warumi 10:17. Je unamsikia nani kuhusu kilimo?tahadhari, ukimsikia mtu anayekuvunja moyo kuhusu mambo ya kilimo huwezi kujihusisha nacho na ukihusisha nacho utafanya bora liende yaani upate usipate kwako ni sawa tu. Ndugu yangu Nakushauri tafuta watu watakaokushauri na kukutia moyo kuhusu kilimo. Kwa kufanya hivyo, utaongeza ari na imani kwenye kilimo.

Hapo juu nimeeleza sababu saba (7) ambazo zimekuwa kikwazo kwa wengi kuwa na mafanikio wanatarajia katika kilimo japokuwa kwenye kilimo kuna fursa ambazo zinaweza kummwezesha mtu yeyote anayejihusisha nacho kupata utajiri au mali. Japo katika sababu nilizoeleza hapo juu nimetoa kinachopaswa kufanyika. Hatahivyo, naomba nikupe hatua nne (4) ambazo zitakusaidia kufanikiwa kwa jambo lolote unalotaka kufanya pamoja na Kilimo;

  1. Lenga jambo ambalo unataka kufanya, kuwa na dhumuni.
Mwanzo wa kutenda jambo lolote ni kuwa na dhumuni ya jambo ambalo unataka kulifanikisha katika safari yako ya maisha. Dhumuni au lengo hupelekea msukumo wa kufanya. Watu mashuhuri na waliofanikiwa duniani, wote walikuwa na msukumo au lengo. Lengo lenye kuleta mabadiliko kwa manufaa ya binadamu. Mfano, Tajiri namba moja duniani, Elon Musk, ana lengo la kurahisisha usafiri wa kwenda anga za juu kutoka duniani-lengo hilo limemsukuma kutengeneza Roketi za kwenda anga za juu, kupitia Kampuni ya SpaceX, lengo hili litampa fedha kwa kutoa huduma ya usafiri ya kwenda sayari za juu. Pia, ana lengo la kurahisisha usafiri kwa ustarabu wa binadamu na kupambana na madhara ya tabia nchi, ili kutimiza hilo mwaka 2004, alianzisha Kampuni ya Tesla Motors kwa ajili ya kutengeneza magari yanayotumia umeme. Kampuni ya SpaceX, SolarCity, Boring, OpenAI, Neuralink na Tesla Motors alizozianzisha kwa manufaa ya binadamu zimempa utajiri wa Trillion 612 (Chanzo; Bloomerg Billionaires Index na Forbes, Agosti 17,2022). Mfano unatupa funzo kuwa lengo hupatikana ukiwa na dhumuni la kutatua matatizo ya binadamu hapa duniani, na utatuzi wake hupelekea kupata utajiri au mali.

Sasa, naomba nikwambie, hata wewe huwa unaliona na kusikia tatizo la uhaba wa chakula hapa duniani. Uhaba wa chakula ni tatizo lenye athari kwa maeneo mengi ya maisha ya binadamu, uhaba wa chakula kwa Taifa lolote unatishia usalama na amani, njaa na vifo, mfumuko wa bei ya bidhaa na kusababisha kupanda kwa gharama za maisha. Uhaba wa chakula husababishwa na uzalishaji mdogo wa chakula ambao pia husababishwa pengine na mvua chache ama kukosa pembejeo muhimu za kilimo. Umuhimu wa chakula kwa maisha ya binadamu unafanya kilimo kuwa fursa kubwa sana ya uchumi wa mtu mmoja mmoja, kaya na taifa. Dhumuni ni kuongeza uzalishaji ili kukabiliana na uhaba wa chakula. Kijana, baba, mama jihusishe na kilimo ili uwe sehemu ya suluhisho la uhaba wa chakula na vilevile uboreshe maisha yako kwa kujiongezea kipato cha fedha.

  1. Weka mpango.
Watu wengi wana doto za kupata au kufanya mambo makubwa hapa duniani, na bahati mbaya huishia kuwa na doto na hata kufa bila kutimiza doto zao. Sababu kubwa ya watu wenye doto kubwa na kutokutimiza ni kushindwa kuweka mipango ya kutimiza. Nakusihi weka mipango kwa ajili ya maisha yako, weka mipango ya namna ya kutekeleza kilimo. Mpango unatoa muongozo wa kipi kifanyike kwa muda upi na gharama ipi na pia kukuzua kufanya vitu ambavyo havipo kwenye mpango. Maisha bila mipango ni maisha yasiyo na mafanikio. Mipango hutoa mtitiriko wa kutekeleza jambo kwa muda maalumu, pia hutoa fursa ya kufanya tathmini ya kinachofanyika na kilichofanyika. Naomba tuone Mpango wa Mungu wa Uumbaji, Biblia katika kitabu cha Mwanzo 1,2 kinasema Mungu aliumba Mbingu na Nchi na vitu vyote kwa muda wa Siku Sita tu na ya saba akapumzika, na kila alipoumba kitu alimalizia kwa maneno “……Mungu akaona ni vyema”…..Mwanzo 1,2. Haya, Mungu hapa anatufundisha nini? Kwanza tuelewe Mungu anauwezo wa kuumba vitu vyote kwa kufumba na kufumbua. Na pia tuelewe kuwa Mungu hakosei, sasa kwa nini alimalizia kwa kusema “……Mungu akaona ni vyema”? Fundisho 1. Mungu anatufundisha kwamba tunapaswa kuweka mipango ya kutekeleza mambo yetu kwa mtiririko mzuri wenye kutuwezesha kufanya tathmini. Fundisho 2. Tunapaswa kufanya tathmini kwa kila hatua tunayoifanya kwenye mpango. Hatimaye, itatusaidia kufanikisha malengo kwa kiwango tunachokitarajia.

  1. Jitenge na watu wenye maneno yanayokatisha tamaa, maneno Hasi.
Maneno Hasi na yakukatisha tamaa ni kikwazo cha kupiga hatua ya maendeleo ya kwa watu wengi (nimeeleza hapo juu, rudia kusoma). Sasa ukitaka kufanya jambo lolote jiepushe na maneno hasi na yakukatisha tamaa. Fanya kilimo au lolote kwa kutazama mafanikio unayotaka bila kuyumbishwa na chochote, songa mbele bila kutazama nyumba, ukijua kuwa katika kufanya jambo kuna matokeo mawili tu yaani kuna kufanikiwa ama kujifunza.

  1. Kuwa na watu wa kujifunza kwao (Mentor).
Katika dunia ya leo kwenye kilimo, kila unachofikiria kufanya kuna mtu fulani katika mahali fulani amewahi au wanafanya aina kilimo unachotaka kufanya. Pata watu walifanikiwa katika kilimo na ujifunze kwao. Pata taarifa muhimu kwa zao ambalo unataka kulima. Pata pia vitabu vya wakulima walifanikiwa na vya tafiti ili kupata ufahamu na ujuuzi na taarifa za kilimo. Kwa kufanya hivi, itakusaidia kuepusha hasara zisizo za lazima na kukuhakikishia kupata mafanikio katika kilimo.

Mwisho, nimatumaini yangu kuwa makala hii itakusaidia kuwa na mtazamo mpya wa kilimo na kujihusisha nacho na kuboresha kipato chako kubadilisha kabisa maisha yako ya kila siku. Hatahivyo, makala hii itakubadilisha kabisa mtazamo wako namna ya kufanya mambo yako. Naomba Mungu awe pamoja nawe unaposoma na kuchukua hatua.
 
Back
Top Bottom