Parabolic
JF-Expert Member
- Dec 3, 2013
- 2,914
- 3,243
Unapoitazama nchi ya Rwanda leo huwezi kuamini kwamba kuna wakati ilitawaliwa na Wahutu tangu ilipopata uhuru mwaka 1962.
Nchi hiyo iliyokuwa koloni la Ubeligiji ilipata uhuru wake na kukabidhi kwenye utawala wa kiraia chini ya Rais Gregoire Kayibanda aliyekuwa mwanamapinduzi kupitia vuguvugu la Parmehutu.
Kayibanda aliangusha utawala wa Watutsi waliokuwa wakipewa kipaumbele na Wakoloni na akaweka mfumo wa chama kimoja.
Tangu wakati huo, Watutsi wakawa hawana sauti serikalini, hivyo wengi walihofia usalama wao na kukimbilia uhamishoni hasa nchini Uganda na wengine Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo).
Kayibanda alichaguliwa tena kuwa rais mwaka 1969, lakini mwaka 1973, aliyekuwa Waziri wake wa Ulinzi, Meja Jenerali Juvenal Habyarimana alimpindua.
Habyarimana pia alikuwa Mhutu, mwenye msimamo mkali. Hivyo aliongoza utawala wa kijeshi akipiga marufuku ufanyaji siasa hadi mwaka 1975 alipoanzisha chama cha National Revolution Movement for Development.
Alirejesha utawala wa kidemokrasia mwaka 1978 kupitia mabadiliko ya Katiba ambapo aligombea urais na kushinda akiwa mgombea pekee.
Aliendelea kugombea urais mwaka 1983, 1988 na kushinda. Wakati wakati wote huo, utawala wake ulikuwa na nguvu na hakukuwa na namna yoyote ya kuupinga.
Wakati wote huo, Watutsi waliendelea kulalamika kunyimwa haki kama raia halali wa nchi hiyo. Wengi waliokimbilia uhamishoni waliomba waruhusiwe kurudi nchini mwao, lakini Rais Habyarimana hakuyatilia maanani, maana yake aliendelea kuendesha nchi kwa kuegemea kwa kabila la Wahutu tu.
Kuelekea mwaka 1990, malalamiko ya Watutsi yalizidi kushika kasi na safari hii, vuguvugu la vita vya wenyewe kwa wenyewe likaanza.
Kundi la wakimbizi wa Kitutsi (Rwanda Patriotic Front) likiongozwa na Fred Rwigyema lilifanya shambulio la kwanza Kaskazini ya Rwanda Oktoba Mosi 1990 likitokea nchini Uganda na liliingia hadi umbali wa kilometa 60.
Hata hivyo, RPF walikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa majeshi ya Serikali ya Rwanda yaliyokuwa yakisaidiwa na jeshi la Ufaransa.
Hivyo walirudishwa nyuma, huku Rwigyema akiuawa kesho yake.
Paul Kagame aliyekuwa mafunzoni nchini Marekani wakati huo alilazimika kukatisha safari yake na kurejea kwenye uwanja wa mapambano.
Aliliondoa jeshi la RPF na kulipeleka milima ya Virunga (nchini DRC) kujipanga upya.
Baada ya miezi kadhaa walirudi tena na kuanza kushambulia upya na hapo vita vikakolea hadi mwaka 1992.
Vita hivyo vilimlazimisha Rais Habyarimana kukubali kufanya mazungumzo ya amani na RPF. Tanzania ndio ilikuwa kitovu cha mazungumzo ya amani, vikao vikifanyika jijini Arusha na vingine Dar es Salaam, wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere na Rais Ally Hassan Mwinyi walikuwa wasimamizi wakuu wa vikao hivyo.
Hata hivyo, wakati mazungumzo hayo yakiendelea, wapambe wa Rais Habyarimana ambao ni Wahutu wenye msimamo mkali walipinga kabisa wazo la kuunda Serikali ya umoja na Watutsi.
Wapambe hao ambao leo tunaweza kuwaita chawa walimchochea Rais Habyarimana wakitaka asiwasikilize kabisa RPF, walipinga kufanya nao suluhisho. Wao waliamini Rwanda ni nchi yao na wao ndio wenye haki kuliko Watutsi.
Naweza kusema, wapambe hawa ndio waliokuwa wakichelewesha kupatikana kwa amani nchini humo, kwani Rais Habyarimana alishaanza kulainika na kukubali kuunda Serikali ya umoja na Watutsi maana mambo yalishaanza kumwelemea.
Mazungumzo yaliyofanyika Arusha Tanzania mwaka 1993 yalipitisha makubaliano kuanzisha Serikali ya umoja, lakini kutokana na maneno ya wapambe, Wahutu wenye msimamo mkali, makubaliano hayo yalichelewa kutekelezwa, hivyo vita vikaendelea.
Januari 1994 kikaitishwa kikao kingine jijini Dar es Salaam, ambapo Rais wa Burundi, Cyprien Ntaryamira naye alialikwa.
Inaelezwa kuwa kikao kilikuwa kikali mno, kwani viongozi wa usuluhishi akiwamo Rais Mwinyi walimkemea Rais Habyarimana kwa kuchelewesha utekelezaji wa makubaliano ya Arusha.
Baada ya kikao kile, Rais Habyarimana na mwenzake wa Burundi, Ntaryamira walipanda ndege moja na kurejea Rwanda. Kumbe ule ndio ulikuwa mwisho wao, maana baada ya saa nzima ya kuwa angani, ndege waliyokuwa wamepanda ilikuwa ikikaribia uwanja wa Kigali Rwanda, hapo ndipo iliposhambuiliwa kwa mabomu na kuuwa watu wote waliokuwemo.
Ajali hiyo ambayo mpaka leo imebaki kuwa kitendawili cha nani aliyehusika, ilikuwa kama kiberiti kilicbowasha moto wa mauaji, ambapo inakadiriwa watu zaidi ya 800,000 waliuawa wengi wakiwa Watutsi.
Baada ya mauaji hayo, jeshi la RPF liliingia na kuchukua madaraka chini ya Paul Kagame.
Kisa hiki ni somo tosha kwa Tanzania. Japo hakuna ukabila nchini, lakini kuna kundi kubwa la Watanzania wamekuwa likidai mabadliko ya Katiba na mfumo wa uchaguzi.
Tangu mwaka 1992 baada ya mfumo wa vyama vingi kurejeshwa nchini, vuguvugu la mabadiliko lilianza, ambapo Tume ya Jaji Francis Nyalali iliyoundwa na Rais Ally Hassan Mwinyi, ilipendelekeza kufanyike mabadiliko ya Katiba ili iendane na mfumo wa vyama vingi.
Mabadiliko ya Katiba yalikuwa ni madogo mno, kiasi cha kumwachia Rais wa Jamhuri ya Muungano madaraka makubwa ya kuendelea kuusimamia mfumo mzima wa uchaguzi.
Madai ya Katiba mpya yameendelea kupigwa danadana na kila rais anayeingia madarakani. Tangu alipoingia Rais Benjamin Mkapa mwaka 1995, hakutaka kuyatilia maanani, lakini alipoingia madarakani Rais Jakaya Kikwete, angalau aliunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuanzisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba.
Hata hivyo, mchakati ule haukukamilika hadi inafika mwaka 2015 alipoingia madarakani Rais John Magufuli, ambaye aliuzima kabisa mchakato huo.
Sasa ameingia Rais Samia Suluhu Hassan, naye anaendeleza danadana. Mara mchakato ukubaliwe, mara wameahirisha baada ya miaka mitatu. Hali inazidi kuwa mbaya, mfumo wa uchaguzi haueleweki, kwani unapendelea upande mmoja ytu wa CCM.
Hali hii mpaka lini? Mpaka yatokee machafuko?
Laiti Rais Habyarimana angekubali kufanya mabadiliko ya Serikali na kuwahusisha Watutsi kwenye Serikali yake, bila shaka, joto la vita lingepungua, bila shaka hata ndege yake isingelipuliwa, bila shaka yasingetokea mauaji ya kimbari vile.
Yote hayo ni kwa sababu ya kiburi cha madaraka, jeuri ya kuwa na cheo, bila kujua kwamba kila lenye mwanzo lina mwisho
Leo CCM wanajiona wako madarakani, wana Serikali, wana Rais ambaye ni pia ni Amiri Jeshi wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama. Hiyo inawapa jeuri na kiburi kiasi cha kukataa kusikiliza maoni ya wengine wanaotaka mabadiliko ya Katiba, wanaotaka mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi.
Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi wa hesabu za Serikali (CAG) kila mwaka zinaonyesga upigaji wa fedha serikalini, hakuna anayewajibishwa. Kashfa za upigani wa fedha Serikali zipo, lakini tunachoona ni kuundwa kwa vikundi vya kumsifu rais, ndio wanaitwa chawa.
Chawa hawa ndio waliomchelewesha Rais Habyarimana kufanya mabadiliko ya serikali yake na hatimaye kifo kikamkuta mlangoni.
Waswahili wanasema, “Mchelea mwana kulia, hulia mwenyewe,” ipo siku watalia.