Katavi: Wazazi watakiwa kuhakikisha wanawapeleka Shule Watoto wao

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987
Wazazi na Walezi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi wametakiwa kuwapeleka Watoto shule ili kuanza masomo kwa muhula wa kwanza ambao umeanza rasmi hii Januari 8, 2024.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Dkt. Alex Mrema amesisitiza Watoto wote wenye umri wa kuwa Shule kuanzia Elimu ya Awali, Elimu ya Shule ya Msingi na wote wanaopaswa kuripoti kuanza Kidato cha Kwanza kuhakikisha wanakuwa darasani ili kupata stahiki yao ya kufundishwa masomo husika.

Dkt. Mrema amesema Elimu ya Awali mpaka Sekondari tayari imelipiwa ada na Serikali ya Awamu ya Sita, kwa hiyo hakuna sababu ya Mwanafunzi kutofika shule na kufundishwa masomo husika.

Mbali na hayo amesisitiza Wazazi na Walezi kuchangia chakula cha Watoto wawapo shule ili waweze kupata chakula.

Gidioni Buntu ni Afisa Elimu Shule za Msingi katika Halmashauri ya Tanganyika amesema hali ya kuripoti kwa Wanafunzi wa Awali na Shule za Msingi zinaridhisha huku Roza Nabahani ambaye ni Afisa Elimu Shule za Sekondari katika Halmashauri hiyo amesema zaidi ya Wanafunzi 250 wameripoti shule huku akisisitiza kupelekwa Wanafunzi shule hata kama hana sare za shule.

Oswad Masawe, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya kutwa Mpandandogo amewaomba wazazi na Walezi kupeleka watoto shule hata kama hana vifaa stahiki huku baadhi ya wazazi wakifurahishwa na namna maandalizi yalivyo katika kuwafundisha wanafunzi sanjari na kuhimiza wazazi wenzao kupeleka watoto shule pamoja na chakula kwa ajili ya Wanafunzi.
 
Back
Top Bottom