Na bado ludewa soon mgodi nako unaanza msongamano wa vyombo vya moto unaenda kuzidi miji ya makambako ,songea na njombe 👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇MALORI YA MAKAA YA MAWE 1000 YANAPITA SONGEA KWA SIKU,SERIKALI KUJENGA BARABARA YA MCHEPUKO
SERIKALI inatarajia kuanza kujenga barabara ya mchepuko kilometa 16 katika mji wa Songea ili kukabiliana na kero ya malori 1000 ya makaa ya mawe yanayopita mjini Songea kwa siku.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya wakati anajibu ombi la wananchi wa Kata ya Lilambo Manispaa ya Songea la kuomba kujengewa barabara itakayopita nje ya mji ili kuepuka kero ya malori ya makaa ya mawe.
Naibu Waziri huyo amekiri kuwa barabara ya Songea hadi Makambako hivi sasa inabeba mizigo mingi na mizito hivyo serikali mwaka huu imeamua kuifanyia matengenezo makubwa kwa kuijenga upya ili iwe barabara ya kisasa.
“Mwaka huu tutaanza kujenga barabara ya lami kuanzia Lutukira sehemu ambayo imechoka sana hadi Songea mjini,ikiwa ni Pamoja na kujenga barabara ya mchapuko Songea mjini yenye urefu wa kilometa 16’’,alisema Naibu Waziri.
Amesema barabara hiyo ya mchepuko itasaidia magari makubwa kupita nje ya nchi badala ya kupita katikati ya mji na kwamba barabara za mchepuko zitapita sehemu tatu ambazo amezitaja kuwa ni eneo la Namanditi,Msamala na Sogea .
Amesema serikali imefanya tathmini ya fidia kwa wananchi wote waliopitiwa na barabara ya mchepuko ambapo tayari serikali imeandaa fedha za kuwalipa fidia zaidi ya shilingi bilioni nne ambazo zipo tayari hazina.
Hata hivyo amesema wakati ujenzi wa kipande hicho unaendelea serikali itaendelea kutafuta fedha za ujenzi wa kipande cha barabara ya kutoka Lutukira hadi Makambako.
Amesema mwezi Septemba mwaka huu serikali italeta gari la kisasa za Zimamoto kwa ajili ya uwanja wa ndege wa Songea.
Mbunge wa Songea mjini Dkt.Damas Ndumbaro kwa niaba ya wananchi wa Songea ameishukuru serikali kwa kutenga bajeti katika mwaka huu wa fedha kujenga barabara ya mchepuko inayokwenda sanjari na ujenzi wa barabara mpya ya lami kutoka Songea hadi Lutukira kilometa 100.
“Kwa siku moja katika mji wa Songea malori 1000 yenye makaa ya mawe yanapita mjini Songea,barabara hii katikati ya mji wa Songea imekuwa kero na haiwezekani tena,tunaishukuru serikali kwa kutenga fedha mwaka huu ili kuanza ujenzi’’,alisema.