JE, SERIKALI ILIKOSEA WAPI KUFUTA KANISA LA UFUFUO NA UZIMA?
Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Richard Hananja, ametumia ukurasa wake wa Facebook kueleza maoni yake juu ya sakata la Kanisa la Ufufuo na Uzima. Yeye anaunga mkono serikali kufuta Kanisa akipingana na wanaoipinga serikali kwa hoja kuwa hoja ya Askofu Gwajima ilikuwa hoja binafasi na hivyo Kanisa lisingeguswa!
Hata hivyo, hoja ya Mch. Hananja ni msimamo wake binafsi, hawakilishi msimamo wa KKKT pamoja na kuwa tumemtaja kama Mchungaji mstaafu wa KKKT. Katika kuijibu hoja, Askofu Mwamakula ameandika andiko lifuatalo:
Hatufurahii watu wanaokutukana Baba Mch. Richard Hananja! Inatakiwa wajibu hoja zako na wewe ujibu hoja zao. Sisi tunataka kujadili hoja yako kama hatuwezi kuijibu!
Askofu Josephat Gwajima anazo kofia tatu - ni kiongozi (askofu) wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, ni Mbunge na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM.
Kanisa lililosajiliwa ni Bodi ya Wadhamini ya Kanisa analoliongoza ambalo lina nguzo mbili - Bodi ya Wadhamini na Halmashauri Kuu ya Kanisa.
Matatizo yaliyopo yalianza baada ya Askofu Gwajima kuita vyombo vya habari na kuhoji yale aliyoyahoji kuhusu utekaji, nk.
Hakuna ushahidi wowote kuwa Askofu Gwajima alitumwa na Bodi ya Wadhamini ya Kanisa au Halmashauri Kuu ya Kanisa kuhoji yale aliyoyahoji. Pia, hakuna ushahidi wowote wa Halmashauri Kuu ya Kanisa kuitishwa na kuketi, kujadili, kuazimia agenda na kumtuma Askofu Gwajima kutoa kauli zile.
Kama kungekuwa na ushahidi huo, basi hapo ndipo serikali ilikuwa na wajibu wa kuchukua hatua hizo. Lakini kabla serikali haijachukua hatua hizo, ingeweza kutoa barua kadhaa za kiutawala kwa Kanisa hilo kama vile ambavyo ilivyotoa kwa KKKT wakati lilipotoa Waraka wa Pasaka wakati wa utawala wa Magufuli. Barua zile zilisambaa mitandaoni kwa hiyo halikuwa jambo la kificho.
Kama hayo yangetokea hapo ndipo hoja yako ya kulifungia na kulifuta Kanisa ingekuwa na mashiko.
Lakini sasa hakuna ushahidi wa hayo na hivyo inabakia hoja kuwa Askofu Gwajima alifanya yale kama mwanachama wa CCM, Mbunge wa Kawe na pia Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM. Haijalishi kikao hicho alifanyia ndani ya jimbo lake la Kawe, Bungeni Dodoma, hotelini au pia katika moja ya kumbi za makanisa yake kwa kuwa haijazuiwa kwa wanasiasa kufanyia vikao katika majengo yamilikiwayo na Kanisa.
Hoja ya kufungia Kanisa kwa kauli za Askofu Gwajima ina matatizo mengi. Hii ni kwa sababu tukikubaliana nayo itabidi pia tukubaliane na hoja kuwa Bodi ya Wadhamini ya Kanisa hilo na Halmashauri Kuu ya Kanisa hilo pia walimtuma kuchukua kadi ya CCM na kuwa mwanachama, kugombea Ubunge kwa tiketi ya CCM na hata kugombea Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, hivyo kufanya yeye kuwa mwakilishi wa Kanisa ndani ya Halmashauri Kuu ya CCM na ndani ya Bunge.
Kama vyombo hivyo havikumtuma na kama yeye sio mwakilishi wa Kanisa ndani ya Bunge na ndani ya Halmashauri Kuu ya CCM, basi ni wazi kuwa kauli za kisiasa za Gwajima haliwezi kubebeshwa Kanisa.
Kitendo cha kumkubali Askofu kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na kuwa Mbunge wa CCM, ina maana kuwa serikali na CCM kwa ujumla wao walikuwa tayari kuwa na mtu huyo na kumvumilia.
Mwisho, katika wasilisho lake, hakuna mahali po pote ambapo Askofu Gwajima alitamka ya kuwa alikuwa anawakilisha ujumbe ule kwa niaba ya Kanisa lolote lile iwe Ufufuo na Uzima au Kanisa kwa ujumla wake!
Uongozwe vema Baba Mchungaji hasa katika kujenga hoja zako kuhusu suala hili la Kanisa la Ufufuo na Uzima kwani linabeba hisia kali sana katika mwili wa Kristo!
Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula
Itunge, Dar es Salaam; 6 Julai 2025; saa 3:43 usiku