MAENDELEO NI ZAIDI YA NYUMBA NA NDINGA:
Mfumo Wa Kujitathmini Mwenyewe
Yeah, ni wikiendi nyingine tena! Tunamshukuru Mungu bado tunaendelea kupumua na kukipigania kwenye hili tufe linaloitwa dunia.
Leo ikiwa ni Agosti Mosi... si unajua tena, mwaka tayari ushainama! Mara paap, Disemba hii hapa, na kabla hujakaa sawa, 2027 hiyo inagonga hodi!
Mtego Wa Maswali Ya Jamii
Siku moja, mdau mmoja akamwambia homeboy mmoja:
"Oi, mwaka ndio huo unaondoka, hivi umefanya nini la maana mwaka huu?"
Homeboy akatabasamu, kisha akacheka tu kifala.
Hivi wadau, haya mambo ya kuambiana "mwaka umeisha, umefanya nini la maana?" si ni kutaka kuchanganyana akili tu? hivi ina maana siku zote hatufanyi mambo ya maana?
Tunasomesha watoto na wadogo zetu.
Tunasaidia ndugu na jamaa wanaokwama.
Tunapambana kila siku kuhakikisha familia inapata chakula mezani na matibabu pindi wanapougua.
Halafu leo hii, kirahisi tu, anakuja mtu na kukuuliza kwa dharau: "Umefanya nini la maana mwaka huu?" Are you serious, homies?!
Kipimo Cha Mafanikio Ni Nini?
Maswali ya aina hii ndiyo yanayowafanya watu wengi wajione wamefeli maisha kwa sababu tu hawajajenga ghorofa au kununua ndinga. Hivi kweli kufanikiwa maishani ni kumiliki mjengo na gari pekee?
Ebwana eh, hebu mtuache kidogo! Kuna mambo ya msingi zaidi ya hayo.
Kikubwa na cha msingi ni kujiangalia wewe binafsi: Toka mwaka jana, kupitia mwaka huu, mpaka huo unaokujaāumepiga hatua kiasi gani kwenye mambo uliyotaka kuyabadilisha?
Kwenye Uraibu: Kama ulikuwa umenaswa na pombe, betting, au wanawake... je, ni kwa kiasi gani umepambana na kupunguza au kuyaacha kabisa?
Kwenye Tabia: Kama ulikuwa mtu wa kiburi, majivuno, na dharau... je, ni kwa asilimia ngapi umefanikiwa kubadilika na kuwa mtu mnyenyekevu? Na una mipango gani ya kujiweka mbali na tabia hizo siku zijazo?
Jitathmini Kwa Kipimo Chako Mwenyewe
Ukiangalia kwa umakini na kiundani zaidi, kuna mambo mengi madogo madogo ya kiroho, kiakili, na kitabia yanayoweza kuwa chachu ya kujitathmini. Hayo ndiyo yanayokuonyesha ni kwa kiasi gani maisha yako yamebadilika na ni jitihada gani unapaswa kuweka ili uwe mtu bora zaidi.
Tuache kuangalia vitu vikubwa vikubwa vya nje ambavyo jamii inatutaka tuamini ndio "maendeleo". Maendeleo ya kweli yanaanzia ndani yako.
Alamsiki!