NADHARIA Iringa: Mzee Kiyeyeu alizikwa na mtu aliye hai na kaburi lake lilizuia umeme wa TANESCO kuwaka

Taarifa hii ni nadharia tu, tumeitolea ufafanuzi kwa kadiri ilivyowezekana
Source #1
View Source #1
Kando ya barabara ya Iringa - Mbeya maeneo ya Njia panda ya Mlolo kuna Kaburi la mtu aliyekuwa maarufu katika fani ya Uganga wa jadi mkoani Iringa na alifahamika kama Mzee Martin Kiyeyeu. Inaelezwa mzee huyu alifariki mwaka 1974 na kuzikwa lakini muonekano wa Kaburi hilo ni kama alizikwa hivi karibuni.

Inaelezwa baada ya kufariki, Mganga huyo alizikwa kwa kufuata taratibu na mira za Machifu ambapo alizikwa kwa kusindikizwa na mtu aliye hai, aliyejitolea kuzikwa naye akiwa hai ili kumsindikiza, ambapo inadaiwa mtu huyo alikaa na kumpakata Mganga huyo aliyezikwa huku akiwa amekaa.

Kaburi.jpg

Kaburi la Mganga Martin Kiyeyeu na nyanya za umeme zilizohamishwa upande
Inadaiwa kumekuwa na maajabu mengi yanayotokana na Kaburi hili ila moja maarufu ni kuzuia umeme wa TANESCO kuwaka;- nyaya za umeme zilizopita juu ya kaburi zilikosa umeme. Pale nyaya zilipotita juu ya Kaburi hilo zilikosa umeme huku zilipotokea kuna umeme hatua iliyolazimisha TANESCO kuhamishia nyaya hizo kwenda upende wa pili wa barabara na hapo ndipo umeme ulipopita na kuwaka.

Pia kaburi hilo linadaiwa kushindikana kuondolewa mara mbili na kusababisha vifo vya watu wawili akiwemo aliyeuawa kwa nyuki na mwingine kufariki ghafla akiendesha tingatinga alipokuwa akijaribu kuling’oa.
 
Tunachokijua
Mzee Martin Kiyeyeu alikuwa Mganga wa Jadi maufu katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini hususan mkoa wa Iringa. Mganga huyo alivuma miaka ya 1960 na alifariki mwaka 1974. Baada ya kufariki Mzee huyo alizikwa Njiapanda ya Mlolo pembezoni mwa barabara iendayo Mkoani Mbeya ukitokea Iringa lipo upande wako wa kulia, katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Tangu kutokea kwa kifo chake mazishi yake na kaburi lake vimezua maswali na hadithi nyingi kwa jamii nyingi za Watanzania.

JamiiForums imepitia vyanzo mbalimbali kujua nadharia mbalimbali zinazotokana na kifo, mazishi na kaburi la Mzee Martin Kiyeyeu kama ifuatavyo:

1. Mzee Martin Kiyeyeu alizikwa na mtu aliye hai
Kama alivyouliza mleta mada hii, zipo taarifa zinazodai kwamba Mzee Martin Kiyeyeu alizikwa kimila kwa kusindikizwa na mtu aliye hai. Mnamo Agosti 27, 2018 Mwanachama wa JamiiForums anayeitwa Kanungila Karim alileta uzi ulioeleza histori ya kaburi la Mzee Kiyeyeu. Akifafanua kuhusu suala la mzee huyo kuzikwa na mtu aliye hai anaandika:

Baada ya kufariki dunia mganga huyu, alizikwa kwa kufuata taratibu na mira za Machifu ambapo alizikwa kwa kusindikizwa na mtu aliye hai, aliyejitolea kwa ajili ya kuzikwa naye akiwa hai ili kumsindikiza, ambapo inadaiwa mtu huyo aliketi na kumpakata mganga huyo aliyezikwa huku akiwa amekaa.

Ufafanuzi huo uliotolewa na Kanungila Karim unafanana na ufafanuzi uliotolewa na Mtumiaji wa Facebook anayetumia jina la Makala Tamu za De Wise Man ambaye pia anaeleza kuwa Mzee Kiyeyeu alizikwa kwa kusindikizwa na mtu aliye hai kama sehemu ya kuzingatia mila za jamii yao. Vyanzo vingi vinavyoeleza tukio hili havitofautiani.

Je kuna ukweli juu ya mtu kuzikwa hai na Kiyeyeu?
Pamoja na kuwa vyanzo vingi vinasimuliakuwa Mzee Kiyeyeu alizikwa na mtu aliye hai bila kutofautiana lakini hakuna uthibitisho wa jina wala maelezo zaidi juu ya mtu huyo. Hata watu waliohusika kuhamisha kaburi la Kiyeyeu hawakueleza kukuta mwili zaidi ya mmoja ndani ya kaburi la Martin Kiyeyeu. Hivyo, JamiiForums inaona jambo hili ni nadharia.

2. Umeme kulishindwa kupitishwa eneo la kaburi
Katika nadharia hii hadithi zinaeleza kuwa miongoni mwa maajabu ya kaburi la Mzee Kiyeyeu ni tukio la TANESCO kushindwa kupitisha nyaya za umeme juu ya makaburi alipozikwa Mzee Kiyeyeu na kulazimika kupitisha nyaya hizo upande wa pili. Inadaiwa kuwa TANESCO walipolazimisha kupitisha umeme juu ya makaburi hayo umeme uligoma kupita hivyo wakalazimika kupitisha upande wa pili wa barabara.

b.jpg

Nyanya za Tanesco zikionekana kukwepeshwa kutokea upande mmoja wa barabara kwenda upande wa pili

Akifafanua zaidi jambo hili Kanungila Karim anandika
Kaburi hilo limekuwa liwashangaza watu waliowengi na hata ndugu wa marehemu huyo kutokana na kuwa na maajabu na miujiza isiyoisha kana kwamba mtu huyo amezikwa mahala hapo jana.
Moja kati ya maajabu makubwa yaliyowahi kutokea mahala lilipo kaburi hilo ni wakati Shirika la umeme lilipokuwa katika zoezi la kuweka Nguzo za umeme pembezoni mwa barabara hiyo na kutokana na kaburi hilo kuwa karibu kabisa na barabara kubwa. Ndipo ilipoamuliwa kuweka nguzo hizo na kupitisha nyaya za umeme kiubishi.Lakini baada ya kumaliza zoezi hilo walishangazwa kwa kuona kuwa eneo la juu ya kaburi hilo hapakuwa ukipita umeme hali ya kuwa ulipoanzia hadi kabla na baada ya kaburi hilo umeme umejaa tele, ila eneo la juu ya kaburi hilo tu hakuna umeme.
Jambo hilo liliwafanya Tanesco kukubali matokeo na kuamua kuchukua uamuzi wa busara kwa kuhamishia baadhi ya nguzo hizo upande wa pili wa barabara ili kukwepa eneo hilo, hivyo nyaya hizo zikavuka barabara kabla ya kufikia kaburi hilo.
Baada ya kulivuka kaburi hili, na baada ya kufanya hivyo ummeme huo uliwaka na hadi hii leo unaendelea kuwaka

Je upi ukweli wa hili?
Nadharia hii ina nguvu kutokana na kuwepo uthibitisho wa nyaya ya TANESCO hupitishwa upande wa pili wa barabara kukwepa eneo la makaburi hayo kama inayooneshwa kwenye picha hii hapo juu. TANESCO mkoa wa Iringa umeiambia JamiiForums kuwa kupitishwa nyaya kando ya makaburi hayo haikuwa sababu ya umeme kushindwa kupita katika eneo hilo bali Shirika liliamua kukwepa kuheshimu eneo hilo la makaburi.

Hivyo, hoja inayodaiwa TANESCO walipitisha nyaya kando ya barabara kwa sababu umeme ulishindwa kupita haina ukweli.

3. Nadharia nyingine ni kaburi la Kiyeyeu halihamishiki

Zilikuwapo imani zilizokuwa zikidai kuwa kaburi la Mzee Kiyeyeu haliwezi kuamishika. Taarifa zinadai kuwa watu wawili waliojaribu kuyaamisha makaburi hayo walifariki. Andiko la Kanungila Karim linaeleza kuwa katika watu wawili waliofariki kwa mmoja kushambuliwa na nyuki na mwingine alikufa ghafla wakati akiwa kwenye Katapila la kubomoa makaburi.

Inadaiwa kushindikana kuondolewa mara mbili na kusababisha vifo vya watu wawili akiwemo aliyeuawa kwa nyuki na mwingine kufariki ghafla akiendesha tingatinga alipokuwa akijaribu kuling’oa.

Ukweli wa makabuli haya kutohamishika ni upi hapa?
Mnamo Desemba 10, 2010 mchakato wa kuhamisha kaburi la Mzee Kiyeyeu ulifanyika na kutimia kwa ukamilifu. Tukio hili liliandikwa na picha zikawekwa kwenye kurasa mbalimbali za mtandao wa kijamii. Mathalani blogu ya Mwaikenda ilichapisha habari yenye kichwa Hatimaye kaburi la Kiyeyeu lang'oka akimnukuu mmoja ya waliohusika kuhamisha kaburi hili Mwaikenda aliandika:

Tumeondoa ‘kiulaini’, hakuna mila wala desturi iliyofanywa kabla ya kuliondoa, na ndugu wa Kiyeyeu wanasema watakuja kazi ikimalizika kwa ajili ya kumaliza mila zao,” alisema Gaitan Utenga.
Alisema kazi hiyo imefanikiwa kutokana na ushirikiano walioupata kutoka Tanroads ambao waligharamia shughuli nzima ya kuondoa kaburi hilo ilyowashirikisha vijana zaidi ya 30.
“Tumenunua sanda na masanduku kwa ajili ya mazishi na hatimaye kaburi limeondolewa tofauti na imani iliyokuwa imezagaa miongoni mwa wengi kwamba ingeshindikana,” alisema.
Alisema ugumu ulikuwa katika kulibomoa kutokana na aina ya ujenzi wake, lakini baada ya kubomolewa kazi ya kulihamishia upande wa pili wa barabara haikuwa ngumu.

IMG_9306.JPG

Mabaki ya mwili wa Kiyeyeu yakiwekwa katika jeneza tayari kwa kwenda kuzikwa upya baada ya eneo la awali kuchimbwa kaburi lake ili kupisha upanuzi wa barabara kuu ya Iringa -Mbeya

Hivyo kutokana na uthibitisho huu nadharia zilizobainisha kuwa ilikuwa haiwezekani kuhamisha kaburi la Mzee Kiyeyeu ni za uongo.

Hivyo, JamiiForums inaona kuwa kwa ujumla matukio na hadithi nyingi zinazohusiana na kifo, mazishi na kaburi la Mzee Kiyeyeu ni za kinadharia zaidi ambazo hazina vithibitisha. Zaidi ya hayo, madai ya kaburi la Mzee Kiyeyeu kutohamishika JamiiForums imethibitisha kuwa si ya ukweli.
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom