SoC02 Ipo haja ya kuirejeshea Tanganyika uhai wake

Stories of Change - 2022 Competition
Sep 12, 2022
9
8
Ipo haja ya kuirejeshea Tanganyika uhai wake


Na Tanganyika Leo.

Mara kadhaa nimekuwa nikijiuliza ni kwanini muungano wetu sio wa serikali moja yenye mamlaka kamili kama ilivyo kwa nchi na serikali nyingine duniani zilizoamua kuungana na kukasimisha nguvu na mamlaka yake kwa serikali moja inayoongoza taifa moja.

Ni kweli maono na matazamio ya waasisi wa Taifa hili Tanzania Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume walipendelea muungano wenye serikali mbili ile ya mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Bila shaka na pasipo kupepesa macho nawasifu kwa mawazo yao chanya ya kuyaunganisha mataifa haya mawili (Tanganyika na Zanzibar). Hakika zipo sababu kadhaa zilizowasukuma kutekeleza muungano huu, ikiwa ni pamoja na udugu (muingiliano wa Watanganyika na Wazanzibar) hali kadhalika ulinzi wa mipaka yetu kwa kuzingatia kwamba ipo mianya mingi kwa Zanzibar n ahata ukanda wa pwani ya Tanganyika.

Lakini nisiwe mnafiki katika hili maana ukweli wangu leo ni bora kuliko maisha yetu sisi Watanzania wa sasa na wa baadae.

Ukiutazama mfumo wa muungano wetu hii leo utagundua kuwa yapo makosa kadhaa ambayo Mwl J.K. Nyerere na Sheikh Karume waliyafanya aidha kwa kujua ama kwa kutokujua.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sura ya Kwanza inazungumzia, “Jamhuri ya Muungano, Vyama vya siasa, watu na siasa ya ujamaa na kujitegemea. Sehemu ya kwanza katika sura ya kwanza imejikita kuzungumzia 'Jamhuri ya Muungano na Watu' ambapo hapo ndipo kusudio langu lilipo.

Kipenge 1 kinatamka "Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano. Kipengele cha 2 (1) kinatamka "Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar, na ni pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzania inapakana nayo".

Kwa ajili ya kuweka sawa hoja yangu kwanini katiba haikutamka 'Tanganyika' kama ilivyo kwa 'Zanzibar' badala yake inasema 'Tanzania Bara'? kwa maneno mengine kama Tanganyika ‘ilikufa’ na kuwa Tanzania Bara ni wazi ingekuwa na Tanzania Visiwani.

Nachelea kusema tumepoteza utambulisho wa watu wa Tanganyika maana bado naiona nafasi ya kuirejeshea Tanganyika uhai wake uliopotea kwa miongo sita sasa.

Mapendekezo katika hoja ya msingi 'ni vyema katika mchakato huu wa katiba mpya Tanzania kama nchi moja ikaundwa na kusimamiwa na serika tatu; serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikisimamia masuala yote ya Muungano ikiwemo kero za muungano, Serikali ya Tanganyika hali kadhalika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Muundo huu wa serikali tatu katika taifa moja lenye muungano wa mataifa mawili utasaidia mgawanyo wa majukumu na kuondoa kero zinazoukabili muungano tangu 1964, kero zinazojitokeza sasa na zile zitakazojitokeza katika miaka ijayo.

Mathalani, moja kati ya kero kubwa inayolitafuna taifa na Watanganyika wengi wananung'unika kwa zaidi ya miaka 50 ni kipengele cha katiba kinachompa nafasi raia wa Zanzibar kugombea kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na katiba hiyo hiyo inamnyima mzawa wa Tanganyika kugombea nafasi ya kiti cha urais Zanzibar.

Kama leo tutabadili katiba na kukubali serikali tatu maana yake raia wa Tanganyika na raia wa Zanzibar wote watapata haki sawa ya kuongoza serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumpa nafasi kila mmoja kugombea (urais) na kuongoza kutokana na asili na silika yake, raia wa Tanganyika kwa Tanganyika na raia wa Zanzibar kwa Zanzibar vivyo hivyo.

Katiba ya sasa ya mwaka 1977 imeminya uhuru wa Tanganyika kujitawala na kufanya mambo yake yenyewe na badala yake imebebeshwa jukumu zito la Muungano kwa mambo ya maendeleo upande wa Tanganyika na upande wa Zanzibar na kuiacha Zanzibar ikifanya mambo yake yenyewe tena ikiwa na rais wake kwa kipindi chote cha muungano, hakika hii sio sawa.

Ni bora na heri sana Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikawa na serikali na katiba yake, Tanganyika nayo ikaundiwa serikali na katiba yake kama ilivyo kwa Zanzibar.

Nyakati za mashaka hizi na kukosa imani ni rahisi kutokana na namna na uhalisia wa mambo ulivyo na swali la msingi ni 'kwanini Tanganyika ipotezwe kwenye ramani ya dunia chini ya muungano na Zanzibar kutambulika duniani kote?'

Mara kadhaa kila ifikapo Desemba 9 kwa makusudi tumewaona na kuwasikia viongozi, hali kadhalika waandishi na vyombo vya habari vikiandika na kutamka mbele ya hadhara ya watu kuwa "leo tunaadhimisha miaka kadhaa uhuru wa Tanzania badala ya Tanganyika".

Makosa ya waasisi wa Muungano yanaweza kurekebishwa leo kwenye katiba mpya bila mabomu wala kumwaga damu na kutoa uhuru wa kila nchi (Tanganyika na Zanzibar) kujitegemea kidola, uchumi, siasa na kijamii.

Tusipoziba ufa itatulazimu kujenga ukuta mpya na tayari tutakuwa tumeshachelewa, katiba mpya yenye muundo wa serikali tatu kwetu iwe muongozo, kutoka kwenye ukungu na fungu la matatizo ya muungano.

Hali ya sasa inatisha kana kwamba tunakosa ujasiri, nchi imegubikwa na matendo yasiyo haki, siasa imefunikwa hatuwezi wala kufikiri, wananchi wanalia umaskini umekithiri na vijana tunasema juu ya nchi ilivyokosa utawala bora.

Inafaa tutatue tatizo mapema, tutubu na kuenenda katika usawa kwa pande zote za muungano kutokana na rasilimali zinazopatikana eneo husika, muda haurudi tena na makosa hayatasameheka.

Jambo linalotakiwa ni kuurudisha uhai wa Tanganyika na hilo litaondoa malalamiko na minong’ono kwamba imemezwa au kunyang’anywa uhai wake.

Mwisho
 
Back
Top Bottom