Huwezi Kuua Maiti -Erick Shigongo

Shunie

JF-Expert Member
Aug 14, 2016
153,008
453,976
SEHEMU YA 01...

Ingawa ilikuwa mchana hali katika msitu wa Kungoni nchini Kongo ilikuwa ya kiza nene! Mawingu yalitanda angani. Ni asubuhi ya siku hiyo tu ilinyesha mvua kubwa tena ya mawe na kusababisha baridi kubwa! Wanyama wengi walijikunyata sababu ya kulowa.

Milio ya ndege na wanyama mbalimbali ilisikika kila pembe ya msitu huo uliokuwa kilometa kama 520 kutoka Jiji la Kinshansa, ulikuwa ni msitu wenye tembo wengi kuliko msitu mingine yote barani Afrika na uliwavutia watalii wengi lakini waliogopa kuutembelea sababu tembo wa msitu huo waliua watalii.

Kila mtu aliamini hakuna mtu aliyeishi katika msitu huo jambo ambalo halikuwa sahihi hata kidogo, kwani mtu mmoja tena bibi kizee mwenye umri wa miaka 80 aliishi katika msitu huo kwa miaka mingi.
Alikuwa ameishi katika msitu huo kwa muda wa miaka isiyopungua thelathini akifanya utafiti wa maisha ya tembo na wanyama wengine kama ndege, Nzige na Mbungo! Alipofika Kongo kwa mara ya kwanza alikuwa na umri wa miaka 30, aliingia nchini humo akitokea Tanzania.

Kinshansa chini ya Patrice Lumumba ilimpokea mwanamke huyo kama mtafiti wa wanyama bila kudadisi sana kilichomfanya aondoke Tanzania na kumpa kibali cha kwenda kuishi msituni Kungoni.

Ni bibi huyo pekee aliyeishi katika msitu huo akizungukwa na wanyama wengi wao wakiwa ni tembo! Aliishi na wanyama hao kwa miaka thelathini mpaka wanyama wote wakamwona ni kama mnyama mwenzao, aliijua lugha za tembo, nzige, mbung’o na ndege mbalimbali! na kuwasiliana nao kama binadamu.

Kulipokuwa na hatari aliitambua kwa kuwasikiliza tembo, nzige, mbung’o na ndege! Alipohitaji kitu chochote porini alitoa mlio fulani mdomoni mwake na Tembo wote walikuja na aliwaagiza kufanya kitu chochote alichotaka! Kifupi wanyama wote walimwona kama malkia wao!

Itaendelea.
 
SEHEMU YA 02...

Kila sehemu aliyokwenda alizungukwa na tembo wakimlinda, ilikuwa si rahisi kwa wanyama wengine wa porini kama simba, chui, kumdhuru sababu ya ulinzi aliopewa na tembo alioishi nao kwa miaka mingi na aliwafahamu tembo kwa majina. Kila mtu aliyesikia habari za bibi huyo alishangaa na Wazungu wengi walikwenda msituni ili kumwona lakini hawakurudi salama, wengi walikufa kabla ya kumfikia. ****

Bibi huyu aliitwa Nyanjige Ndaki, hakuwa Mkongo bali Mtanzania tena kutoka Mkoani Mwanza, alikuwa msomi wa chuo kiku cha Edniburgh, nchini Uingereza alikopelekwa na gavana kama zawadi kwa mama yake aliyekuwa mpishi wa Gavanna huyo kwa kipindi kirefu!

Gavana alipotaka kuondoka chini alimchukua bibi Nyanjige wakati huo akiwa na umri wa miaka mitano tu ili akamsomeshe nchini Uingereza. Aliishi Uingereza kwa miaka karibu ishirini na tano bila kurudi Tanzania na aliporejea nchini mwaka 1967 alikuwa tayari ana digrii mbili za elimu ya viumbe badala ya kufanya kazi aliushangaza ulimwengu alipofanya mauaji ya watu 150 kwa mpigo na hakuna aliyeelewa sababu ya mauaji hayo!

Tangu siku ya kwanza aliyoingia Kongo na kupewa kibali cha kuishi porini Kungoni hakurudi tena mjini kwa kuogopa kukamatwa, siku zote aliishi na wanyama porini, akila matunda kama wanyama, wakati mwingine aliua swala na kula nyama! Hayo ndiyo yakawa maisha yake siku zote, hakutaka kabisa kukutana na binadamu yeyote.

Patrick Lumumba alipokufa serikali ya Kongo chini ya Mabutu Seseko ilimsahau kabisa bibi huyo, hakuna mtu aliyetaka kujua habari zake. Serikali ya Tanzania nayo baada ya kumtafuta kwa muda mrefu bila mafanikio iliamua kuachana na swala hilo ikiamini bibi Nyanjige alikufa! Ingawa msako wa chini chini uliendelea kwa usaidizi wa nchi nyingine kama Marekani, Ufaransa, Ujerumani ambazo pia Raia wake walikufa katika tukio la mauaji hayo.
 
SEHEMU YA 03...

Ilikuwa si rahisi kumwona bibi Nyanjige kwa ulinzi mkali uliokuwepo nyumbani kwake porini, nyumba yake ilizungukwa na Tembo wasiopungua kumi, waliomlinda usiku na mchana! Wazungu wengi waliojaribu kumfikia ili kupata picha yake waliuawa kwa kunyangwa na Tembo!

Mzungu mmoja aliyekwenda porini kwa helkopta alifanikiwa kuipata picha ya bibi Nyanjige akiwa katikati ya tembo!
Ni picha hiyo iliyoleta matatizo kwani ilipochapishwa katika magazeti na majarida mbalimbali nchini Uingereza na Marekani serikali ya Tanzania ilishtuka na kuamini kuwa mtu aliyekuwa akitafutwa alikuwa porini nchini Kongo.

Bila kuchelewa ilituma wanajeshi wapatao ishirini waliopewa msaada na askari wengine kumi wa Kongo! Walifika hadi msituni lakini hawakufanikiwa kumkamata bibi Nyanjige na pia hawakufanikiwa kurudi salama nyumbani! Wote walikufa kifo hichohicho cha kukanyagwa na Tembo!

Mpaka mwezi moja baada ya askari hao kuondoka hapakuwa na mawasiliano yoyote kutoka msituni, simu zao za upepo ziliendelea kuita bila majibu! Hilo lilionyesha wazi watu hao hawakuwa hai!

Ilibidi serikali za Tanzania na Kongo kwa kushirikiana ziandae jeshi kubwa lenye askari wasiopungua elfu tano waondoke kwenda msituni kumsaka bibi Nyanjige!
Maaskari wote 5000 walilizunguka pori wakiwa na silaha kali mikononi mwao na ndege za kivita zilipita angani!

Askari ndani ya ndege hizo walipoangalia chini ka kutumia viona mbali waliziona maiti za askari wenzao zikiwa ardhini na tembo wengi wakiwa wamezunguka kibanda kidogo kilichoonekana kuwa kama nyumba.

Ghafla mamia kwa maelfu ya ndege walionekana angani, hawakujulikana walikotokea! Wengi walitua kwenye vioo vya mbele vya ndege hizo na kuwafanya marubani washindwe kuendesha ndege zao vizuri kwa sababu hawakuona mbele.
“Tufanya nini sasa?”

“Turudi tukatue kwanza, vinginevyo hawa ndege watasababisha tuangushe ndege ni wengi mno na sielewi wametoka wapi!”
“Sawa geuza basi!”

Wakati wanageuza ndege nyingine ilishafika karibu yao ikipita katikati ya makundi ya ndege, zote mbili ziligongana na kuwaka moto zikiwa angani! Askari waliokuwa wakitembea kwa miguu walishangaa kuona ndege zikigongana.

Inaendelea.
 
SEHEMU YA 04...

“Tusongeni mbele! Mpaka tumtie nguvuni huyu bibi, kazi hii tumepewa na serikali zetu ni lazima tumkamate na kumfikisha Tanzania akiwa hai, ajali hii imeniongeza hasira zetu unanipata lakini, ovaaa!”
“Ndiyo ninakupata mkuu! Hata sisi tumeishuhudia ajali hiyo na tunazidi kusonga mbele ila kuna kitu cha ajabu kidogo kimetokea hapa!”

“Kitu gani?”
“Kundi kubwa sana la mbung’o na nzige wamejitokeza na wanatuuma sana! Maaskari wengi wameshindwa kabisa kuendelea wa safari na wameanguka chini! Hivi ninavyoongea wanashambuliwa na mbung’o hata mimi mwenyewe mwili wangu wote umezingirwa na mbung’o pamoja na nzige wanakula magwanda yangu!”
“Kweli?” Aliuliza Meja Jenerali Job Lupilya aliyekuwa mkuu wa operesheni hiyo, hakupata jibu kutoka upande wa pili!

Alizidi kuita kwa muda mrefu bila kutikiwa, hali ilimtisha na kumwamuru mmoja wa wapiganaji wake awashe kifaru cha vita na wakaondoka kuelekea upande wa pili kulikokuwa na kikosi alichowasiliana nacho!

Iliwachukua kitu kama dakika ishirini kufika eneo hilo, hawakuamini walichokiona walipofika, miili ya zaidi ya maaskari mia moja ililala chini ikiwa imeliwa nyama zote na Nzige pamoja na Mbung’o! Ilikuwa ni mifupa tupu iliyolala chini ambayo wazungu huiita Skeleton! Nzige na Mbung’o wengi wasio na idadi walitapakaa kila mahali wakiendelea kula miili ya maaskari waliokufa.

“Hivi hawa ni Nzige gani yaani wamewaua askari wetu wote?” Aliuliza mwanajeshi mmoja na kabla hajafanya lolote walishangaa kuona kundi kubwa la Nzige kama wingu au kundi la nyuki wakihama kutoka sehemu moja hadi nyingine likiwafuata!
“Ina maana wanatufuata sisi?”
“Inavyoonekana!”

“Hebu ngoja!” Alisema mkuu wa kikosi na kutoa baruti na akawalipulia, nzige wengi walikufa lakini dakika moja tu baadaye kundi jingine la Nzige na Mbung’o lilitokea upande wa pili na kuanza kuwashambulia! Yalikuwa ni maumivu makali mno, magwanda yao ya jeshi yalitafunwa na kujikuta wakiwa uchi katika muda wa sekunde chache ndipo minofu yao ilipoanza kuliwa kwa kasi ya ajabu.
 
SEHEMU YA 05...

Ghafla Meja Jenerali Lupilya akiwa amekata tamaa kabisa alisikika kitu kama mluzi ukipigwa pembeni yake
“Pswiiiiiiiiiiii!” Kufuatia mluzi huo Nzige wote wakasimamishwa zoezi lao la kula minofu yake! Mluzi mwingine tena ulifuata lakini katika mtindo tofauti kidogo! Kufuatia mluzi huo Nzige wote waliruka na kuondoka zao.

Meja jenerali Lupilya alipogeuza uso wake na kuangalia pembeni alikiona kibibi kizee kikitembea taratibu kuelekea mahali alipolala, Tembo wengi walikizunguka na mmoja wao alipomfikia alizungushia mkonga wake shingoni mwa Meja jenerali, alimnyanya na kuanza kumzungusha hewani, Lupilya alipiga kelele na kulia.

“Wiiiiii!” Bibi alitoa mlio mdomoni kwake na Tembo akamweka chini Lupilya, alikuwa akitoka jasho mwili mzima na mkojo ulimpenya! Tembo wote walikaa chini na kulaza vichwa vyao ardhini kama ishara ya kuonyesha heshima kubwa kwa bibi Nyanjige.

“I’m the queen of the forest who are you?”(Mimi ni malkia wa msitu wewe ni nani?)
“I’m ...ma...jor gene...ral Lupi...lya fro..m Tan..zania!”(Mimi ni Me...ja jene....rali Lupil....ya natoka Ta....nzania)
“Tanzania? From what tribe are you?”(Tanzania? Wewe ni kabila gani?)
“Su…ku..ma!” Alijibu Lupilya huku akilia na kutetemeka! Hakuamini kulikuwa na binadamu aliyekuwa na uamuzi mkubwa kiasi hicho mbele ya wanyama wa mwituni!

“Ule Nsukuma getegete?”(Wewe ni Msukuma kabisa?) Bibi Nyanjige alimuuliza meja kwa kabila ya Kisukuma, Lupilya alibaki mdomo wazi akishangaa.
“Ngh’ana gete mama! Nu bebe gashi uli wa Kukaya?”(Kweli kabisa bibi kumbe na wewe ni mtu na nyumbani!) Alijibu Lupilya huku akiendelea kulia machozi, mwili wake wote ulimuuma sababu ya kuliwa na Nzige, alipomwangalia mwenzake alikuwa kimya nyama zote hazikuwepo mwilini!Alibaki mifupa.

“Mnataka nini hasa nyinyi?” Bibi aliuliza kwa kiswahili.
“Nduhu mhayo mama! Nilekejage natalashogeja kabili!(Hakuna neno bibi nisamehe sitarudia tena) Meja Lupilya aliendelea kuongea kwa Kisukuma.
“Ongea kiswahili mpumbavu wewe! Unafikiri Kisukuma kitakusaidia HAPA?”
“Nisamehe bibi na mimi nilitumwa tu!” Lupilya alibadilisha lugha.
 
Back
Top Bottom