SEHEMU YA 08...
Siku ya kuondoka London ndiyo ilikuwa siku ya furaha zaidi katika maisha yake, alipanda ndege ya shirika la ndege la Alliance Airlines iliyoondoka London kuja Dar es Salaam kupitia Paris, Uturuki, Misri, Ethiopia, Nairobi na hatimaye kuingia Dar es Salaam. Safari hiyo ilimchukua masaa zaidi ya ishirini na nne, wakati anaingia Dar es Salaam saa nne ya asubuhi alikuwa amechoka kupita kiasi lakini hakutaka kulala Dar es salaam kabisa na kuamua kuunganisha siku hiyo hiyo kuelekea Mwanza ambako aliwasili saa 10 jioni.
Alikuwa na hamu kubwa ya kuonana na mama yake hivyo alikodisha teksi kutoka uwanja wa ndege ambao upo kama kilometa nane kutoka Mwanza mjini hadi kijijini kwao Usagara kilometa kama sabini kutoka Mwanza mjini, ambako mama yake aliishi baada ya kustaafu kazi ya upishi nyumbani kwa gavana.
Iliwachukua zaidi ya masaa mawili kufika kijijini Usagara, sababu ya ubovu wa barabara uliokuwepo mjini Mwanza. Alishangazwa na hali aliyoikuta nyumbani kwa mama yake, nyumba ya mama ilikuwa imebomoka na kuanguka upande mmoja, nyasi ziliota hadi mlangoni mwa nyumba hiyo iliyojengwa kwa udongo! Mlango ulikuwa wazi na ilikuwa rahisi sana kufikiri watu walioishi katika nyumba hiyo walihama miezi michache kabla.
Hali hiyo iliufanya moyo wa Nyanjige upige kwa nguvu na kasi ya ajabu alihisi kuna tatizo lilitokea ambalo hakuwa na habari nalo! Hakutaka kuteremsha mizigo yake ndani ya gari na kuamua kuusukuma mlango na kuingia hadi ndani ya nyumba ya mama yake ambako alianza kuita jina la mama yake lakini hakuitikiwa hatimaye aliamua kusukuma mlango wa chumbani na kukuta umefungwa kwa komeo kutoka ndani, alijua kwa hakika ndani kulikuwa na mtu!